KUNA suala huwa linatukera sana hapa katika maskani yetu nalo ni tabia ya wachezaji au timu fulani kupenda kupoteza muda pindi wanapocheza baadhi ya mechi.
Imeshaanza kuwa tabia sugu katika ligi yetu ambayo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya IFFHS, inashika nafasi ya sita katika viwango vya ubora vya ligi za Afrika.
Ni mbinu ambayo mara nyingi hutumika pale timu hasa zile za kati na za chini kwenye msimamo wa ligi zinapokuwa zinacheza dhidi ya timu zili juu pale kunapokuwa na matokeo ya sare au timu zinaooonekana kubwa zimetanguliwa kufungwa bao.
Lakini, wakati mwingine hutumiwa na timu pale inapojiona haina wachezaji wazuri au kikosi bora cha kuweza kupishana au kuhimili makali ya upande wa pili.
Sio mbinu nzuri na ya kiungwana kwa sababu inawapunja mashabiki ambao wanalipa viingilio vyao ili kupata burudani ya soka ambayo inategemewa iwe kwa dakika 90 na sio pungufu na hapo.
Hata hivyo inaonekana kwa hapa nchini wanaochangia kwa kiasi kikubwa timu na wachezaji wapoteze muda ni marefa. Wanaonekana kuwa na hofu ya kuwapa adhabu wahusika wa tabia hizo.
Kwa kutowapa kadi wachezaji wanaopoteza muda iwe nyekundu au njano, inachangia kuwapa nguvu ya kuendelea kufanya hilo wakiamini kuwa wao au timu hawawezi kuadhibiwa.
Lakini iwapo waamuzi watawashughulikia kwa usahihi wanaopoteza muda katika mechi, timu na wachezaji wataanza kuheshimu muda uwanjani na kujiepusha na vitendo vya upotezaji wake.
Wanasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Marefa wetu wamechagua kuwalea wachezaji katika upotevu wa muda na inaonekana ni jambo la kulifurahia wakati linashusha hadhi timu na ligi yetu.