ALIYEKUWA Kocha wa viungo na utimamu wa mwili wa Yanga raia wa Bosnia-Herzegovina, Adnan Behlulovic ameanza mazungumzo ya kujiunga na Azam FC kwa ajili ya kuongezea nguvu ndani ya kikosi hicho.
Chanzo kutoka ndani ya Azam, kimeliambia Mwanaspoti kwamba, Behlulovic, yupo katika mazungumzo hayo kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa, kwa ajili ya kumrejesha tena kocha huyo nchini.
“Hakuna muafaka wowote uliofikiwa hadi sasa, ingawa ni kweli dili hilo lipo, kwa kiasi kikubwa tumevutiwa na uwezo wake japo hatuwezi kufanya uamuzi bila ya kuzingatia ridhaa kutoka katika benchi letu la ufundi,” kilisema chanzo hicho.
Behlulovic alifanya kazi Yanga chini ya Kocha Mkuu, Mjerumani Sead Ramovic aliyeondoka Februari 4, 2025, kwa makubaliano ya pande zote mbili, tangu atambulishwe kikosini humo Novemba 15, 2024, akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini.
Ujio wa Behlulovic katika kikosi cha Yanga, ulikuja haraka baada ya Ramovic kumpendekeza licha ya kumkuta kocha wa mazoezi ya viungo, Taibi Lagrouni.
Behlulovic aliyezaliwa Januari 5, 1981, kwa sasa anafundisha timu ya vijana chini ya miaka 19 ya FK Zeljeznicar Sarajevo ya kwao Bosnia-Herzegovina, ambapo uwezo wake na mbinu za kisasa za maandalizi ya kimwili, ndio jambo kubwa linalombeba.
Mbali na hilo, Behlulovic anasifika pia kwa ufuatiliaji mzuri wa takwimu za utimamu wa mwili na uwezo mkubwa wa kufanikisha urejeshaji wa wachezaji waliotoka majeruhi haraka, kutokana na uzoefu wake aliokuwa nao.
Wakati hayo yakijiri, kocha wa sasa wa viungo wa Azam FC, Mtunisia Mehdi Marzouki mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, ingawa mtaalamu huyo aliyefanya kazi US Monastir, CS Sfaxien na Esperance zote za Tunisia, anafanya pia mazungumzo ya kuuongeza.