Anayedaiwa kutapeli watalii kupitia mitandao atiwa mbaroni 

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa KDC, Kata ya Mbokomu, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Musa Mushi (40), kwa tuhuma za kujihusisha na udanganyifu wa kutapeli watalii wanaoingia nchini wakiwamo wanaokuja kutalii kwenye Mlima Kilimanjaro.

Taarifa ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, imetolewa leo Machi 12, 2026 na Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simoni Maigwa ambapo amesema amekuwa aliwatapeli watalii hao fedha kwa njia ya mtandao  kwa nyakati tofautitofauti wanapoingia nchini.

“Mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kufungua akaunti zenye kujinasibisha na biashara ya utalii na kufanya udanganyifu kisha kuwaibia fedha wageni wanaopanga ama wanaoingia nchini kwa shughuli za utalii, “amesema Kamanda Maigwa 

Amesema baada ya Jeshi la Polisi  kupata taarifa za utapeli huo, waliweka mtego na kufanikisha kumtia nguvuni mtuhumiwa huyo Machi 11, mwaka huu.

“Akaunti ambazo mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia kutapeli fedha katika mtandao wa Instagram ni pamoja na footonkilitanzania na tovuti ya www.footonkilitanzaniaadventure.com,”amesema Kamanda Maigwa 

Aidha, amesema uchunguzi zaidi unaendelea ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi ili hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Kamanda Maigwa, amewataka wananchi na raia wa kigeni wenye malalamiko ya kutapeliwa fedha na mtuhumiwa huyo kufika Kituo cha Polisi kati Moshi ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linatoa onyo kwa yeyote mwenye tabia kama hizo kuacha mara moja, kwani mkono wa sheria hautaacha kumfikia kama alivyofikia huyu Musa Mushi,”amesema Kamanda Maigwa.