Bakwata: Sikukuu ya Eid El-Fitri Machi 20–21

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) limetangaza rasmi Sikukuu ya Eid El-Fitri mwaka huu itasherehekewa Machi 20 au 21, 2026, kutegemea mwandamo wa mwezi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Machi 12, 2026 na Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Mruma, sherehe za kitaifa zitaongozwa na Baraza la Eid litakalofanyika jijini Dar es Salaam.

Alhaj Mruma amesema:“Sherehe za Eid El-Fitri mwaka huu zitaanza kwa Swala ya Eid itakayofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI, Makao Makuu ya Bakwata, Kinondoni kuanzia saa 1:30 asubuhi.”

Ameongeza kuwa, “Baada ya swala hiyo, kutafanyika Baraza la Eid katika Ukumbi wa Julius Nyerere Convention Centre kuanzia saa 9:00 alasiri. Tunawaomba Waislamu wote kuhudhuria kwa wingi na kwa wakati.”

Aidha, Alhaj Mruma amebainisha kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Eid atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye atashiriki katika sherehe hizo kama ishara ya mshikamano na jamii ya Waislamu nchini.

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Bakwata amewatakia Waislamu wote swaumu njema katika kumi la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhani na maandalizi mema ya Sikukuu ya Eid El-Fitri.

Sherehe hizi za Eid El-Fitri ni fursa muhimu ya kuimarisha umoja, kuadhimisha mafanikio ya kiroho baada ya mwezi wa Ramadhani na kuendeleza mshikamano miongoni mwa Waislamu nchini.