Bandari, Planet kinapigwa fainali ya pili

JOTO la fainali ya pili ya Dunda Swish Tournament linazidi kuzikumba timu za Bandari Mwanza na Bugando Planet.

Fainali hiyo itafanyika Machi 15, 2026 katika Uwanja wa Mirongo mjini Mwanza, ikitanguliwa na mchezo wa fainali ya wanawake kati ya Eagle Queens na Court Queens.

Nyota wa Bandari Mwanza, Alphonce Kasekwa alisema timu yake imekuwa ikirekebisha makosa waliyofanya katika robo tatu za mchezo wa fainali ya kwanza.

“Tumerekebisha makosa yote na wachezaji wameahidi kushinda katika fainali ya pili,” alisema Kasekwa ambaye pia ni kiongozi wa timu hiyo.

Aliongeza kuwa ushindi utaifanya timu yao iweze kuivua ubingwa Bugando Planet na kwamba wachezaji wako tayari kwa ajili ya kuhakikisha hilo linafanyika.

Aliwataja wakali wa Bandari Mwanza watakaokuwepo kuwa ni Christian Cimanuka, Zakayo Obeid, Basilius Mageni, Isack Ntruminadi, Daniel Elia, Ramadhani Babili, Bryan Yegela.

Naye nahodha wa Bugando Planet, John Sapa alisema nyota wao Romanus Kisia aliyekuwa majeruhi katika fainali ya kwanza amepona.

“Nachosema timu ya Bandari Mwanza wasiuchukulie mchezo huo mwepesi, kwa kweli tumejipanga kulipa kisasi,” alisema Sapa. Katika fainali ya Jumapili, endapo Bugando Planet itashinda, fainali ya tatu itapigwa na timu itakayoshinda itakuwa bingwa kutokana na ushindi wa michezo 2-1.