Bilioni 388.8 kujenga Afcon City Unguja

WAKATI Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imejiandaa vizuri kupokea ugeni huo kwa kuanzisha mradi wa michezo uliopewa jina la Afcon City.

Mradi huo unaojengwa Fumba kisiwani Unguja, unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 150 (Sh388.8 bilioni za Tanzania) ambao unalenga kuvutia watalii watakaofika kushuhudia mashindano hayo.

Hayo yamebainishwa Machi 12, 2026 na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma kuelezea mafanikio ya siku 100 za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Waziri huyo alisema mradi huo upo katika hatua ya ujenzi wa muundo Mkuu ikijumuisha uwekaji wa nondo, ujenzi wa beam, kumwaga zege na ujenzi wa kuta.

“Hadi kufikia sasa mradi huo umefikia asilimia 35, na hiyo inadhihirisha namna ambavyo Serikali imejipanga kupokea ugeni huo,” alisema Pemba. 

Pia, alisema kwa timu ambazo zitachaguliwa kucheza kisiwani hapa, zitatumia viwanja vya New Amaan Complex na Suluhu Academy kwa ajili ya kufanyia mazoezi.

Hivyo, Serikali inayatazamia mashindano hayo kuwa fursa ya kuitangaza Zanzibar na utalii.

Waziri huyo aliwataka wananchi wa Zanzibar kujipanga na kuzitumia fursa za kibiashara zitakazojitokeza baada ya kukamilika kwa ujenzi huo, akisisitiza kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Ikumbukwe kuwa, Tanzania pia ilikuwa mwenyeji wa CHAN 2024 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda ambapo mechi za Kundi D lililoundwa na Sudan, Senegal, Nigeria na Congo zilitumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, huku zile za Kundi B ikiwamo mwenyeji Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati, zikichezea Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kuelekea AFCON 2027 itakayochezwa Juni 19, 2027 hadi Julai 18, 2026, Tanzania, Kenya na Uganda zitashirikiana kuandaa fainali hizo ambapo kwa Tanzania, baadhi ya mechi zitachezwa Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.