Arusha. Zikiwa zimepita siku 17 tangu agizo la Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba la kurejeshwa mali za mfanyabiashara wa Arusha, Josephine Shirima, mali hizo bado hazijarudishwa huku Jeshi la Polisi likimshikilia dalali wa Mahakama anayedaiwa kuhusika katika kuchukuliwa kwa mali hizo.
Aidha, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Arusha, Dominic Mollel, aliyekuwa anashikiliwa na polisi kwa siku kadhaa, ameachiwa kwa dhamana.
Februari 24, 2026, mbele ya Waziri Mkuu, Josephine alidai kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Morris Makoi pamoja na Mollel walihusika kumdhulumu mali zake zilizokuwa dukani.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 12, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema kwa sasa wanamshikilia dalali wa Mahakama (jina halikutajwa) huku Mollel akiachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea.
“Tunamshikilia dalali wa Mahakama na tunaendelea kuwatafuta wengine wanaodaiwa kushirikiana naye katika suala hilo,” amesema Mkude.
Kuhusu Mbunge huyo, Mkude amesema suala hilo linashughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu hivyo hawezi kulizungumzia kwa sasa.
Amesema lengo kuu ni kuhakikisha mali za mfanyabiashara huyo zinapatikana licha ya mgogoro huo kudumu zaidi ya miaka minne.
Awali, Februari 24, 2026, Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Josephine kudai katika mkutano wa hadhara jijini Arusha kuwa duka lake lilivunjwa usiku na mali zake kuchukuliwa. Waziri Mkuu alimuagiza Mkude kuhakikisha mali hizo zinarejeshwa haraka kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa Josephine, mgogoro huo unatokana na maduka ya stendi ndogo ya Arusha yaliyokuwa yamejengwa kwa mkataba wa miaka 10, ambapo baada ya mkataba kuisha walipaswa kuyarejesha kwa halmashauri lakini baadhi ya watu waliendelea kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mollel alidai Josephine alikuwa mpangaji ambaye hakuwa analipa kodi, na walifuata utaratibu wa kuwachukulia hatua wapangaji waliokuwa wanadaiwa, kwa ushirikiano na askari pamoja na dalali wa Mahakama.
Hata hivyo, viongozi wa Serikali wamesisitiza kuwa mali hizo zilichukuliwa bila kufuata taratibu za kisheria na uchunguzi utaendelea huku jitihada za kuzitafuta mali hizo zikiendelea.
