Hili ndilo soko la mafuta na bei zinapangwa hivi

Vita inayoendelea katika ghuba ya Uajemi tayari vimesababisha bei ya bidhaa muhimu ya mafuta kuongezeka, na ikiwa vita hiyo itaendelea ni dhahiri dunia inaweza kuangukia kwenye mgogoro wa kiuchumi unaosababishwa aidha uhaba wa mafuta au kupanda kwa gharama za maisha kutokana mfumuko wa bei na kuongezeka gharama za uzalishaji.

Mafuta ndicho chanzo kikuu cha nishati duniani, asilimia 33 ya nishati inayotumika kuendesha sekta mbalimbali na maisha ya binadamu inatokana na bidhaa hiyo, kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Nishati la Umoja wa Mataifa (IEA).

Vyanzo vingine vya nishati mathalan gesi asilia, nyuklia, jua, na nishati nyengine mbadala zinafuatia. Uhusiano mafuta na uchumi ni kuwa bidhaa hiyo inachangia sehemu kubwa ya mahitaji ya nishati, ni kama makaa mawe ilivyokuwa katika karne mbili zilizopita.

Mafuta yanaweza kuuzwa ghafi kutoka kwa wazalishaji kwa kipimo cha pipa. Pipa moja ni sawa lita za ujazo 159 ambayo ni galoni 42 (1ltr/3.7 US gallon). ukisikia “bei ya pipa moja imeongezeka” hiyo ndiyo maana yake.

Wanunuaji wa mafuta ghafi wanaweza kuwa makampuni makubwa yenye viwanda vya kusafisha, nchi zenye uchumi mkubwa zinanunua kwa wingi na kuweka akiba yakiwa ghafi. Mafuta pia yanaweza kuuzwa kama bidhaa iliyo tayari moja kwa moja kwa matumizi, mfano kuagiza petroli, dizeli, ni tofauti na kuagiza mafuta ghafi.

Biashara ya mafuta inafanyika kupitia masoko maalumu ya kimataifa ambapo wazalishaji na wanunuzi hupanga bei na mikataba ya uuzaji kwa mfumo wa mikataba ya moja kwa moja kati ya nchi au makampuni makubwa ya mafuta, au kupitia masoko ya fedha ya bidhaa.

Masoko maarufu ya kimataifa ya mafuta ni pamoja na New York Mercantile Exchange (NYMEX) nchini Marekani, na Intercontinental Exchange (ICE) mjini London, Uingereza.

Sokoni mafuta huuzwa kwa mikataba ya aina mbili; kwanza, kwa bei ya sasa, mafuta yanauzwa na kununuliwa kwa ajili ya kufikishwa kwa mnunuzi mara moja au ndani ya muda mfupi.

Pili, mauziano kwa bei ya baadaye, mikataba inafanywa leo kwa ajili ya kununua au kuuza mafuta katika tarehe fulani mbeleni kwa bei iliyokubaliwa sasa. Nchi na makampuni makubwa wanatumia mtindo huu kujilinda na mabadiliko ya ghafla ya bei endapo ikitokea baadaye.

Bei za mafuta sokoni zinategemea kiwango cha ubora wa mafuta ghafi na ndio zinatumika kama rejea, ishara, kuonesha mwenendo wa bei ipoje kwa sasa sokoni, Faharisi mashuhuri zaidi kueleza mwenendo wa bei ya mafuta sokoni ni zifuatazo;

Brent crude; aina ya mafuta ghafi yanayotumika kupima bei ya mafuta duniani (global oil benchmark). Brent pia hutumika kama bei rejea kuongoza upangaji wa bei ya mafuta katika nchi nyingi za Ulaya, na Asia. Jina Brent kiasili ni visima vya mafuta vilivyopo katika eneo la Bahari ya Kaskazini (North Sea) kati ya Uingereza na Norway.

West Texas Intermediate (WTI), aina nyengine ya mafuta ghafi yanayotumika kama kipimo cha bei hasa katika soko la Marekani. Mafuta haya huzalishwa zaidi katika maeneo ya Texas na majimbo mengine ya Marekani. Katika soko la kimataifa, bei ya WTI hutumika kufuatilia mwenendo wa bei ya mafuta hasa Amerika Kaskazini, mara nyingi hulinganishwa na bei ya Brent ili kuelewa mabadiliko ya soko la mafuta duniani.

Aina nyingine ni Dubai/Oman crude, aina ya mafuta ghafi yanayotumika kama kipimo cha bei hasa katika soko la Mashariki ya Kati na Asia. Hutumika pia kama bei rejea katika nchi za Asia Mashariki na Mashariki ya Kati, hulinganishwa pia na Brent na WTI ili kufuatilia mwenendo wa soko la dunia.

Na aina nyengine za bei rejea za mafuta ghafi ni kama OPEC basket, wastani wa bei ya mafuta ghafi kwa nchi mbalimbali zinazozalisha mafuta wanachama wa OPEC. Bei ya mafuta ghafi Iran heavy (Iran), Arab light (Saudia arabia), Urals (Urusi), nk.

Ikumbukwe kuwa bei ya mafuta inayotajwa katika vyombo vya habari hutokana na viwango hivyo vya kimataifa, ukiongeza na ushuru, ushafirishaji, faida (ndio unapata bei ya mafuta kwenye pampu).

Tanzania huagiza mafuta yaliyosafishwa kama petroli, dizeli na mafuta ya taa, si ghafi, kutoka kwenye viwanda vya kusafisha mafuta vya nchi za Kiarabu kama Saudi Arabia, UAE na Oman. Hivyo, upangaji wa bei nchini unafuata mwenendo wa bei za marejeo ya mafuta yaliyosafishwa katika masoko ya Arabuni na Uajemi.

Kwa mfano, ikiwa bei ya mafuta kwenye Ghuba ya Uajemi itapanda kwa 5%, bei ya kikomo inayopangwa na EWURA kwa wauzaji nchini lazima iongezeke mwezi unaofuata. Upangaji wa bei unazingatia pia ushuru, tozo na mabadiliko ya thamani ya sarafu ili kupata bei ya mlaji.