Jamii yatakiwa kupaza sauti kukomesha ukatili wa kijinsia

Dodoma. Jamii imetakiwa kuvunja ukimya na kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyowakumba wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, ili kusaidia kukomesha vitendo hivyo na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Machi 12, 2026, jijini Dodoma na Mkuu wa Dawati la Jinsia, Wanawake na Watoto Mkoa wa Dodoma, Christer Kayombo, wakati akizungumza na makundi ya wanawake kutoka wilaya za Chamwino na Dodoma Mjini katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).

Kayombo amesema kesi nyingi za ukatili wa kijinsia huishia kwenye vikao vya kifamilia, hali inayosababisha wahanga kukosa haki zao huku watuhumiwa wakiepuka kuwajibishwa kisheria.

“Lakini, pia kesi nyingi huharibiwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi au kushughulikiwa ndani ya familia badala ya kuripotiwa kwa vyombo vya sheria. Hivyo, ninawaomba mpaze sauti na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia badala ya kuvinyamazia,” amesema Kayombo.

Ametaja aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia ikiwemo ukatili wa kiuchumi, ambapo wanawake hunyimwa haki ya kumiliki mali au kufanya maamuzi kuhusu fursa za kiuchumi, mara nyingi kwa kuzuiwa na wenza wao.

Kayombo amesema pia kuna ukatili wa kimwili unaojumuisha vipigo, ukeketaji, mauaji na matendo mengine yanayosababisha majeraha au hata vifo.

Baadhi ya washiriki wa mdahalo wa kupinga ukatili wa kijinsia ulioandaliwa na chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) leo Machi 12, 2026 Jijini Dodoma

Akizungumza katika mdahalo huo, Mkurugenzi wa Tamwa, Dk Rose Reuben, amesema wanawake na watoto ndio wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia, akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kukomesha vitendo hivyo.

Amesema Tamwa inaendelea kutetea haki za wanawake, wasichana na watoto kupitia vyombo vya habari pamoja na kuhamasisha wanawake kujitokeza na kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili.

“Wakati mwingine mtu anaweza kuzoea kufanyiwa vitendo fulani kama kupigwa au kudhalilishwa na kuona ni jambo la kawaida, ilhali tayari ni ukatili. “Ndiyo maana tunasisitiza kufungua vinywa na kuzungumza wazi ili kuondoa ukimya unaolinda ukatili,” amesema Dk Reuben.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Wakulima Wadogo Wilaya ya Chamwino (Juwacha), Janeth Nyamayahasi, amesema wanawake wengi hukumbana na ukatili wa kunyimwa haki ya kumiliki ardhi, hali inayowafanya kukosa makazi hasa baada ya kufiwa na waume zao.

“Unakuta mwanamke hana ardhi kwao kwa sababu anaambiwa yeye ni wa kuolewa. Lakini, akiolewa na baadaye ndoa ikavunjika au mume akafariki, ndugu wa mume humnyang’anya mali na kumfukuza, hivyo anakosa mahali pa kuishi,” amesema Nyamayahasi.

Ofisa Uchechemuzi na Habari wa Tamwa, Florence Majani, amesema mradi wa ‘Sauti Zetu’ unaotekelezwa katika mikoa ya Tanga, Dodoma na Dar es Salaam unalenga kuwafikia wanawake, watoto na watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Amesema wanawake wengi hukutana na vitendo vya ukatili wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya masoko, stendi na hata majumbani, jambo linalowakatisha tamaa na kuathiri maendeleo yao.