Kauli ya Mojtaba Khamenei Yazua Taharuki Mashariki ya Kati, Taarifa yake Yasomwa Runingani

Taarifa inayodaiwa kutolewa kwa niaba ya kiongozi mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei, imesomwa kupitia televisheni ya taifa huku kukiwa na tetesi zinazoendelea kuhusu hali yake ya afya.

Taarifa hiyo ilitangazwa na mtangazaji wa habari katika televisheni ya serikali ya Iran, lakini Khamenei mwenyewe hakuonekana hadharani. Kutokuwepo kwake kwenye matangazo ya moja kwa moja kumezidisha uvumi kuwa huenda ni mgonjwa sana, amejeruhiwa vibaya au hata kufariki kufuatia mashambulizi ya anga yaliyotikisa nchi hiyo hivi karibuni.

Katika ujumbe huo ulioandikwa, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 56 alisema Iran haitasita kulipiza kisasi kwa damu ya mashujaa wake waliouawa.

Khamenei alichukua nafasi ya uongozi baada ya baba yake, Ali Khamenei, kuuawa katika shambulio la anga tarehe 28 Februari.

Katika taarifa hiyo, Khamenei alisisitiza kuwa Iran ina nia ya kudumisha uhusiano wa kirafiki na nchi jirani za Ghuba ya Uajemi, lakini akaonya kuwa mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo yataendelea.

“Hatuna uadui na nchi jirani. Tunacholenga ni kambi za Wamarekani,” alisema katika ujumbe huo.

Kiongozi huyo pia aliwataka viongozi wa nchi za eneo hilo kufunga mara moja kambi za kijeshi za Marekani, akisema uwepo wa kambi hizo na matumizi yake kushambulia Iran hauwanufaishi mataifa ya eneo hilo.

Aidha, alisema Iran itadai fidia kutoka kwa maadui wake au kuchukua hatua za kulipiza kisasi kwa kuharibu mali zao. Wakati huo huo aliahidi msaada wa kifedha kwa wananchi wa Iran waliodhurika kutokana na machafuko ya kijeshi yanayoendelea.

Mojtaba Khamenei, amesisitiza kuwa nchi yake itendelea kutumia njia ya kuzuia usafirishaji wa mafuta kupitia Strait of Hormuz eneo la kimkakati linalosafirisha asilimia kubwa ya mafuta duniani.

Khamenei pia alidokeza uwezekano wa kuungwa mkono na makundi yenye silaha katika eneo la Mashariki ya Kati, akidai kuwa makundi yaliyopo Iraq yako tayari kuisaidia Iran, huku yale ya Yemen yakitarajiwa pia kushiriki katika mapambano dhidi ya Marekani na Israel.

Katika sehemu ya ujumbe wake, alizungumzia pia majonzi ya familia yake kufuatia mashambulizi yaliyomuua baba yake. Alisema alipoteza baba yake, mke wake na ndugu wengine wa karibu katika mashambulizi hayo.

Hata hivyo, licha ya kutolewa kwa taarifa hiyo, vyanzo kutoka Tehran vinadai kuwa Khamenei anadaiwa kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sina, huku eneo la hospitali likiwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama.

Bado haijafahamika iwapo alijeruhiwa katika mashambulizi yale yale ya anga yaliyosababisha kifo cha baba yake.