Tabora. Serikali kupitia kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania Tanesco), Tanzania Concrete Poles Manufacturing Company (TCPM), imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege kilichogharimu zaidi ya Sh8 bilioni mkoani Tabora.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha zaidi ya nguzo 100 za zege kwa siku.
Ujenzi wa kiwanda hicho ulianza Oktoba 2024 na sasa umekamilika kwa asilimia 100.
Hatua iliyobaki ni ukaguzi wa mwisho wa mkandarasi kabla ya kuanza rasmi uzalishaji wa nguzo hizo nchini.
Leo Machi 12, 2026, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilitembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda hicho ikiongozwa na mwenyekiti wake, Subira Mgalu.
Akizungumza baada ya ukaguzi, amesema kamati imeridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa na kuwataka wahusika kuhakikisha uzalishaji unaanza kwa ufanisi ili kufikia malengo ya Serikali.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo mara baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala cha RAFIKI Brikets na Kiwanda cha kutengeneza Nguzo za Zege Tabora
“Tumeridhishwa na maendeleo ya kiwanda hiki na tunapongeza Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha hakuna vikwazo vinavyoweza kuchelewesha uzalishaji ili wananchi wapate huduma bora ya umeme,” amesema Mgalu.
Ameongeza kuwa mahitaji ya nguzo za zege nchini ni makubwa, hivyo aliishauri Serikali kupitia Wizara ya Nishati kuendelea kujenga viwanda vya kikanda pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa nguzo hizo, hasa kwa ajili ya kubadilisha nguzo za miti katika maeneo yenye unyevunyevu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema kiwanda hicho kitaongeza uwezo wa uzalishaji wa nguzo za zege nchini.
Amebainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina viwanda vitatu vya kutengeneza nguzo hizo, lakini bado kuna haja ya kuongeza vingine ili kukidhi mahitaji.
Ndejembi amesema licha ya nchi kuwa na umeme wa kutosha, kukatika kwa umeme mara nyingi husababishwa na hitilafu kwenye miundombinu ya nguzo, ikiwemo kuungua moto au kuanguka kutokana na kuoza.
“Tumebaini changamoto kubwa kwenye nguzo za miti. Serikali imeamua kuchukua hatua ya kudumu kwa kuanzisha matumizi ya nguzo za zege ili kumaliza kabisa tatizo hili,” amesema.
Nguzo za Zege zinazozalishwa na kampuni Tanzu ya Tanesco ya TCPM iliopo Kiloleni manispaa ya Tabora
Katika ziara hiyo, Kamati pia ilitembelea kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala cha Rafiki Briquets kilichopo eneo la Kiloleni, Manispaa ya Tabora.
Mgalu ameelekeza kiwanda hicho kuanza uzalishaji haraka ili kupunguza ukataji wa miti unaotumika kukaushia tumbaku.
Amesema uzalishaji wa mkaa mbadala utasaidia kulinda mazingira na kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida.
Aidha, amesisitiza kuwa maono ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia badala ya kuni, ambazo zimekuwa zikichangia uharibifu wa mazingira na madhara kwa afya.
Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa, amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza uzalishaji ndani ya wiki mbili zijazo baada ya kukamilisha maandalizi machache yaliyobaki.
“Kwa sasa tumebakiza mambo machache ya mwisho kukamilisha, hivyo ndani ya wiki mbili zijazo tunatarajia kiwanda kitaanza uzalishaji na wananchi wataanza kunufaika na mkaa huo mbadala,” amesema.
