KUNA msemo wa kiuanamichezo unasema kwamba: “Usajili wa kwanza bora zaidi katika timu ni ule wa kumbakisha mchezaji wako tegemeo.”
Simba imeshutukia jambo mapema na imeamua kupita na msemo huo kwa kuanza kuwapa mikataba wachezaji inaohitaji kuendelea nao ikifanya hivyo kwa beki wa kati, Rushine De Reuck na kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma.
Nyota hao ambao mikataba yao ilikuwa inafikia tamati mwisho wa msimu huu, wameongeza Machi 8, 2026 ambapo Kagoma amesaini miaka miwili hadi 2028, huku Rushine akipewa mwaka mmoja utakaomalizika 2027.
Kitendo cha Rushine na Kagoma kuongezea mikataba kuendelea kusalia klabuni hapo, uamuzi huo umemkosha zaidi kocha wa kikosi hicho, Steve Barker.
Kama ambavyo awali Mwanaspoti liliandika juu ya wekundu hao kukoshwa mapema na ubora wa Rushine aliyesajiliwa msimu huu, mabosi wa Simba walishtuka mapema juu ya ubora wa beki huyo raia wa Afrika Kusini.
Akizungumzia kuongeza mkataba Rushine, Barker alisema: “Nikweli nimefurahia hiyo hatua. Nadhani kwa muda ambao amekuwa hapa kila mmoja ameona namna ambavyo amekuwa kiongozi mzuri kwenye eneo la ulinzi, lakini pia akiwaongoza wenzake kuhakikisha timu inafanya vizuri.
“Timu bora inatakiwa kuwabakisha wachezaji wake bora na Rushine ni mmoja wa wachezaji bora ambaye anastahili kubaki hapa. Nadhani sasa ataendelea kucheza kwa juhudi kuisaidia timu kwenye mechi zake.”
Barker aliongeza: “Kagoma pia ni mchezaji mzuri mwenye nguvu za kutosha. Ni mmoja kati ya wachezaji bora ambao niliwakuta hapa. Ni hatua nzuri kuhakikisha uongozi unaendelea kumuacha akiichezea timu hii kubwa.”
Kagoma alitua Simba Julai 8, 2024 akitokea Singida Fountain Gate ambayo sasa ni Fountain Gate. Katika kipindi cha miaka miwili akiwa Simba, amekuwa mchezaji muhimu eneo la kiungo licha ya kusajiliwa viungo wengine wakabaji akiwamo Babacar Sarr aliyekaa kwa miezi sita pekee, akaondoka.
Kiungo huyo wa zamani wa Geita Gold, ubora wake ulimfanya Kocha Fadlu Davids ambaye waliingia wote Simba msimu wa 2024-2025 kumtumia zaidi kikosi cha kwanza sambamba na Fabrice Ngoma na kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huo.
Kwa upande wa Rushine, Simba imefanya uamuzi wa kumuongezea mkataba baada ya kwanza kujiridhisha kwamba beki huyo hana majeraha ya mara kwa mara kama ambavyo awali ilihofiwa kutokana na kukumbwa na hali hiyo wakati akizichezea timu kadhaa ikiwamo Maccabi Petah Tikva ya Israel na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Tangu Rushine atue Simba, haraka aliingia kwenye kikosi cha kwanza ambapo kwa sasa ishu sio Msauzi huyo kuanza, ila atacheza na nani.
Akiwa uwanjani, Rushine ameonyesha ubora mkubwa wa kujua kutibua mashambulizi ya wapinzani kwa utulivu na akili, akifanikiwa kuiongezea Simba ubora mkubwa kwenye ukuta wake.
Mbali na kulinda, pia akipanda juu anaipa Simba kitu kwani mpaka sasa ameshafunga mabao matatu Ligi Kuu Bara akiwa ndiye beki mwenye mabao mengi ndani ya kikosi cha Simba kabla ya jana kucheza dhidi ya Singida Black Stars.
Wakati nyota hao wawili wakiongezewa mikataba, kuna wengine mwisho wa msimu huu wanatarajiwa kuondoshwa baada ya kumaliza muda wao. Mbali na wanaomaliza muda wao, wengine huenda wakasitishiwa mikataba kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo majeraha na nidhamu.
Wachezaji ambao mikataba yao inafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu ni Elie Mpanzu, Djibrila Kassali, Mousa Camara, Shomari Kapombe, Hussein Abel, David Kameta ‘Duchu’, Abdurlazack Hamza, Ladack Chasambi, Chamou Karaboue, Saleh Karabaka, Mzamiru Yassin na Awesu Awesu. Pia Seleman Mwalimu kutoka Wydad na Neo Maema aliyetokea Mamelod, mikataba yao ya mkopo inamalizika.
Kwa upande wa Jonathan Sowah ambaye huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya Simba, kuna taarifa za mwisho wa msimu kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba kutokana na yanayoendelea kwani hivi sasa amesimamishwa kwa madai ya utovu wa nidhamu, huku Mohamed Bajaber ambaye naye ni msimu wa kwanza, majeraha ya mara kwa mara yanamponza, huenda naye akaachwa.
Kwa Mpanzu, alitua Simba 2024-2025 akisaini mkataba wa miaka miwili, siku za karibuni amepoteza nafasi kikosi cha kwanza tofauti na mwanzoni kufuatia usajili wa dirisha dogo, hivyo suala la kutoongezewa muda wa kubaki linaweza kutokea.
Kipa Kassali yupo katika uangalizi, alisaini mkataba wa miezi sita baada ya kuumia kwa Moussa Camara (kipa namba moja) na Yakoub Suleiman (kipa namba mbili), hivyo ubora wake utazingatiwa kama apewe mkataba mpya au la.
Ishu ya Camara ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili 2024-2025, ameondolewa kwenye mfumo wakati wa dirisha dogo Januari 2026 baada ya kuwa na majeraha ya muda mrefu, hivyo msimu ukiisha inaelezwa hataongezewa.
Kapombe ambaye ni mkongwe ndani ya Simba akiwa sehemu ya manahodha wa kikosi hicho, bado anahitajika kutokana na uzoefu wake huku nafasi anayocheza ya beki wa kulia ikiwa bado haija mbadala sahihi licha ya uwepo wa David Kameta ‘Duchu’ ambaye naye mkataba unamalizika mwisho wa msimu huu.
Kipa namba tatu, Hussein Abel naye mkataba unaisha, anaweza kubaki akiendelea kusikilizia nafasi, au akatafuta changamoto sehemu nyingine.
Majeraha ya Abdurlazack Hamza nayo yanaiumiza kichwa Simba, inapiga hesabu za kutomuongezea kwani tangu aumie mwanzoni mwa msimu huu, hajarudi uwanjani.
Wengine ni Ladack Chasambi aliyepoteza nafasi, Chamou Karaboue kwa sasa anaitumikia TRA United kwa mkopo huku nafasi yake ndani ya Simba ikizibwa na Ismael Toure. Saleh Karabaka huenda akabaki mazima JKT Tanzania anapocheza kwa mkopo, huku Mzamiru Yassin aliyepo Tabora United, amepoteza nafasi Simba muda mrefu tangu ujio wa Kagoma wanaocheza wote eneo la kiungo mkabaji, wakati Awesu Awesu yupo zake Kenya akiitumikia Police Kenya kwa mkopo.
Nyota wenye uhakika wa kuendelea kuwa ndani ya Simba kwa msimu ujao hadi sasa ni Yakoub Suleiman, Rushine De Reuck, Wilson Nangu, Shomari Kapombe, Antony Mligo, Yusuph Kagoma, Alassane Kanté, Naby Camara, Hussein Semfuko, Morice Abraham, Vedastus Masinde, Inno Loemba, Anicet Oura, Libase Gueye, Clatous Chama, Baraka Mwangosi na Nickson Kibabage. Valentino Mashaka huenda akatolewa tena kwa mkopo kwani msimu ukimalizika atabakisha mkataba mmoja ndani ya Simba. Kwa sasa anacheza JKT Tanzania kwa mkopo.