Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara imeamuru kufungwa kwa kampuni ya Sahara Media Group Limited, iliyojishughulisha na vyombo vya habari, matangazo na huduma za uchapishaji, kutokana na hali mbaya ya kifedha.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Dk. Mwajuma Kadilu baada ya kuridhia ombi la kufilisi lililowasilishwa na kampuni yenyewe. Ombi hilo liliungwa mkono na kiapo cha Afisa Mkuu wa kampuni, Steven Diallo, pamoja na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Memorandum na Articles of Association, azimio la Bodi ya Wakurugenzi, notisi za madai ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mwanza, na taarifa za fedha zilizokaguliwa za miaka 2023 na 2024.
Katika uamuzi wake, Jaji Kadilu alisema kuwa ushahidi uliowasilishwa unaonyesha kuwa kampuni imepata hasara kubwa na haiwezi kulipa madeni yake:
“…ikiwa imethibitika kuwa mwombaji anapata hasara kubwa na hana uwezo wa kulipa madeni yake, basi hatua sahihi ni kufungwa kwa kampuni hiyo,” alisema Jaji Kadilu.
Mahakama pia iliteua Wakili Alex Mgongolwa wa Excellent Attorneys na Wakili Frank Mwalongo wa Apex Attorneys kuwa wasimamizi wa pamoja wa mchakato wa kufilisi kampuni hiyo. Wasimamizi hawa watachukua udhibiti wa mali zote za kampuni, kusimamia ulipaji wa madeni na kuwasilisha ripoti ya mwisho mahakamani baada ya mchakato kukamilika.
Aidha, mahakama ilipiga marufuku uhamishaji wa mali, uhamishaji wa hisa, au mabadiliko yoyote ya wanachama wa kampuni kuanzia kuanza kwa mchakato wa kufilisi.
Ushahidi mahakamani ulionyesha kuwa kampuni hiyo ina deni la kodi la takribani Shilingi milioni 97.7 kwa TRA, huku taarifa za fedha zikionesha hasara ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.9 mwaka 2023, pamoja na hasara nyingine katika miaka iliyopita. Takribani asilimia 80 ya mapato ya kampuni yalitumika kulipa madeni ya kodi, hali iliyosababisha kushindwa kuendesha shughuli zake na kutimiza majukumu ya kifedha.
Mahakama ilibainisha kuwa wasimamizi walioteuliwa watahakikisha mali za kampuni zinadhibitiwa ipasavyo, madeni yanafutwa au kulipwa kwa mujibu wa sheria, na ripoti ya mwisho itawasilishwa kwa mahakama baada ya kukamilika kwa mchakato wa kufilisi.