Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Benjamin Kikula (61), baba mkubwa wa marehemu Naomi Kivamba (13), kwa tuhuma za kuhusika na ukatili wa kijinsia na mauaji ya mtoto huyo, tukio lililotokea katika eneo la Isakalilo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Machi 12, 2026 katika eneo la Zizi, Manispaa ya Iringa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SCAP Allan Bukumbi, amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa anahusishwa na tukio hilo na tayari anashikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Kwa mujibu wa polisi, Naomi alikuwa mtoto wa mdogo wa mke wa mtuhumiwa, jambo lililoongeza majonzi kwa familia na wananchi waliokuwa wakifahamu ukaribu uliokuwepo kati yao.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa tukio hilo linadaiwa kufanyika katika moja ya nyumba za mtuhumiwa zilizopo eneo la Njiapanda.
Inadaiwa Kikula ana nyumba mbili katika eneo hilo, moja ikiwa ni makazi ya familia na nyingine ambayo haijakamilika ujenzi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya kuvunjwa kwa chumba kimoja kilichokamilika katika nyumba hiyo, baadhi ya vitu vinavyodaiwa kuwa vya Naomi, ikiwemo nguo zake, vilikutwa ndani.
Hata hivyo, katika mazishi ya Naomi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mlolo yaliyopo Manispaa ya Iringa, mtuhumiwa alihudhuria mazishi hayo kabla na baadaye kukamatwa na vyombo vya dola kufuatia uchunguzi wa awali.
Naomi, ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba na mkazi wa Njiapanda, Manispaa ya Iringa, aliripotiwa kupotea Machi 7, 2026 baada ya kutumwa dukani kununua kiberiti, lakini hakurejea nyumbani.
Siku hiyo, mjomba wa Naomi, Benjamin Kikula (ambaye sasa ni mtuhumiwa katika tukio hilo) alimweleza mwandishi wa habari kuwa mtoto huyo alitoweka baada ya kutumwa dukani.
“Naomi alitumwa dukani kununua kiberiti na kaka yake, lakini baada ya hapo hakuonekana tena,” alisema Kikula.
Kwa mujibu wa maelezo yake ya awali, familia haikupata hofu kubwa baada ya mtoto huyo kuchelewa kurejea.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, SCAP Allan Bukumbi akiwa katika mkutano wa hadhara eneo la Zizi Manispaa ya Iringa akizungumza na Wananchi juu ya tukio la mtuhumiwa Baba mkubwa Benjamin Kikula (61) kukamatwa kwa tuhuma za ulawiti na mauaji ya Naomi Kivamba (13). Picha Christina Thobias
Hata hivyo, kadri muda ulivyozidi kupita hadi majira ya saa tisa alasiri bila kuonekana, wasiwasi ulianza kuongezeka.
Mwili wa Naomi ulipatikana Machi 8, 2026 ukiwa na majeraha kadhaa, ikiwamo mkono uliodaiwa kuwa umevunjika na shingo iliyolegea, hali iliyowafanya ndugu na majirani kuamini kuwa alipata mateso makubwa kabla ya kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, pia kulionekana alama za majeraha katika sehemu ya paja huku nguo zake zikiwa zimechanika, jambo lililoibua maswali mengi kuhusu mazingira ya tukio hilo.
Akithibitisha matokeo ya uchunguzi wa kitabibu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Alfred Mwakalebela, alisema hospitali ilipokea mwili wa mtoto huyo na kufanya uchunguzi.
“Tulifanya uchunguzi wa mwili na kubaini kuwa mtoto huyo alifanyiwa ukatili wa kijinsia. Pia tuligundua kuwa alinyongwa na shingo yake ilipata majeraha makubwa,” alisema Dk Mwakalebela.