Mchujo Ukonga Kings si mchezo

MAMBO ni moto! Kama ulidhani kwamba Ukonga Kings kumepoa, sahau. Kinachoelezwa ni kwamba utakuwapo mchujo wa kusaka vipaji kwa ajili ya kuunda kikosi kitakachoshiriki mashindano ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), mwaka huu.

Habari kutoka ndani ya kikosi hicho zinaeleza kwamba, uongozi umepanga kufanya mchujo kwa ajili ya kusaka vipaji vitakavyoongezwa ili kuimarisha timu hiyo kwenye mashindano hayo.

Kwa mujibu wa habari hizo, mchujo huo utahusisha wachezaji wapya chipukizi na wakongwe.   

Akizungumza na Mwanaspoti, nyota wa Ukonga Kings, Mustafa Madondola alisema kazi itakuwepo katika mchujo wa kutafuta wachezaji watakaochezea timu hiyo kwenye BDL.

Madondola alisema mchujo huo pia unatokana na wachezaji wengi kuvutiwa kufanya mazoezi na timu hiyo katika Uwanja wa Ukonga, Magereza.

“Timu ya Ukonga Kings ni moja ya timu inayopendwa katika eneo hilo. Hivyo kwa wachezaji wanaotokea eneo la Ukonga wanapenda kuchezea timu hiyo,” alisema Madondola.

Kuhusu maandalizi ya BDL, mchezaji huyo alisema amekuwa akifanya mazoezi binafsi kila asubuhi katika Chuo cha Ukonga (Magereza), na nyakati za jioni hufanya na timu kwenye Uwanja wa Ukonga, Magereza.

Alisema BDL 2026 inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zilivyojipanga kwa kusajili wachezaji bora na mahiri. Timu ya Ukonga Kings ilishuka daraja 2024 na 2018 iliwahi kufungwa na JKT katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu ya BDL.