Dar es Salaam. Watu wa umri kati ya miaka 40 hadi 50, ambao kwa kawaida ndiyo nguvu kazi ya Taifa, wanatajwa kuwa miongoni mwa wanaoathirika zaidi na ugonjwa sugu wa figo nchini Tanzania, huku wakazi wa mijini wakiongoza kwa kiwango kikubwa kuliko wale wa vijijini.
Takwimu zinaonesha takribani asilimia saba ya Watanzania wanaugua ugonjwa sugu wa figo, huku utafiti ukionesha asilimia 15 ya wakazi wa mijini wameathirika ikilinganishwa na asilimia mbili ya watu wanaoishi vijijini.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 12, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Delilah Kimambo amesema ugonjwa huo unaendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya nchini na duniani kwa jumla.
Amesema ongezeko la wagonjwa linahusishwa kwa kiasi kikubwa na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari, pamoja na matumizi holela ya dawa za maumivu na baadhi ya dawa za mitishamba.
“Ni dhahiri uchunguzi wa mapema ni muhimu sana. Kugundua dalili za awali kunasaidia kuzuia madhara makubwa ya ugonjwa sugu wa figo na kupunguza gharama kubwa za matibabu,” amesema.
Alipoulizwa kwa nini mijini ndiyo waathirika wengine, Dk Kimambo amesema watu wa mijini wanaathirika zaidi na magonjwa ya figo kutokana na mtindo wa maisha, ikiwamo unywaji na ulaji usiofaa ikilinganisha na watu waishio vijijini ambao mara nyingi wanakula vyakula kutoka mashambani na visivyo na mafuta kwa wingi.
Kwa mujibu wa Kimambo, kwa sasa zaidi ya wagonjwa 3,000 nchini wanapata huduma ya kudumu ya kuchujwa damu (dialysis), huku Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee ikiwa na zaidi ya wagonjwa 400 wanaotegemea huduma hiyo.
Takwimu za hospitali hiyo zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kuanzia mwaka 2015 hadi 2025, idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya dialysis imeongezeka kwa asilimia 203, kutoka wagonjwa 124 hadi 376.
Aidha, mizunguko ya uchujaji damu imeongezeka kwa kasi kutoka 11,770 mwaka 2015 hadi 30,409 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 158.
Kutokana na mahitaji hayo kuongezeka, hospitali hiyo imeendelea kuimarisha huduma za figo ikiwa ni pamoja na upandikizaji wa figo ulioanza mwaka 2017 na hadi sasa wagonjwa wapatao 100 wamefanyiwa upandikizaji huo.
Kwa sasa hospitali hiyo ina zaidi ya mashine 50 za dialysis zinazohudumia wagonjwa kila siku, huku mashine moja ikigharimu takribani Sh30 milioni bila kujumuisha vifaa vingine tiba vinavyotumika wakati wa matibabu.
Kwa upande wa huduma za wagonjwa wa nje, kliniki za figo katika hospitali hiyo hupokea wagonjwa wapatao 600 kila mwezi, huku kliniki ya watoto ikihudumia takribani wagonjwa 120 kwa mwezi.
Kimambo amesema pamoja na maendeleo hayo, gharama za matibabu ya figo bado ni kubwa duniani kote, hali inayofanya kinga kuwa njia bora zaidi ya kupunguza athari za ugonjwa huo.
Ametaja visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa figo nchini kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari, maambukizi ya VVU, matumizi holela ya dawa za maumivu na dawa za mitishamba, pamoja na baadhi ya saratani za mfumo wa mkojo.
Visababishi vingine ni pamoja na uchafuzi wa hewa, joto kali na upungufu wa maji mwilini.
Katika kuadhimisha Siku ya Figo Duniani mwaka huu yenye kaulimbiu “Afya ya Figo kwa Wote – Kutunza Watu, Kulinda Dunia,” hospitali hiyo imeendesha kampeni za elimu na uchunguzi wa afya kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Hatua hizo zimehusisha utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa seminari kuu ya St Charles Lwanga pamoja na wananchi waliopimwa katika kliniki ya satelaiti ya hospitali hiyo katika Viwanja vya Sabasaba.
Kimambo ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha, kunywa maji ya kutosha, kupunguza matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari na kupima afya angalau mara moja kwa mwaka.
“Gharama za matibabu ya figo ni kubwa sana, lakini tunaweza kuzipunguza kwa kuwekeza zaidi katika kinga,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Figo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Jonathan Mngumi amesema ugonjwa wa figo mara nyingi hauna dalili katika hatua ya kwanza mpaka ya tatu, hivyo kupima mara kwa mara husaidia kubaini ugonjwa mapema.
Aidha amesema kupanda kwa joto la dunia pia kunachochea kusambaa kwa magonjwa ya kitropiki yanayoweza kuharibu figo.
Mkurugenzi wa huduma za uuguzi na ukunga Muhimbili akipanda mti.
Amebainisha matibabu maalumu ya ugonjwa wa figo, hasa dialysis, hutumia rasilimali nyingi.
“Rasilimali nyingi zinahitajika, kiasi kikubwa cha maji, nishati na plastiki zinazotumika mara moja, na huzaa gesi chafuzi za anga. Sesheni moja ya dialysis inaweza kutoa gesi ya kaboni sawa na kuendesha gari kilomita takribani 240,” amesema.
