Mtakwimu aonya matumizi mifumo ya akili unde

Dodoma. Zaidi ya vijana 713 na wasimamizi 69 wamepata ajira za muda katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu, huku wakionyeshwa onyo la kutotumia mifumo ya akili unde (AI) kupika takwimu kwa kuwa shughuli zao zinafuatiliwa katika kila hatua.

Onyo hilo limetolewa jana jioni Machi 11, 2026 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Amina Msengwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari akitangaza mpango wa ukusanyaji taarifa za tafiti nne zinazotekelezwa na ofisi hiyo.

Amezitaja tafiti hizo kuwa ni utafiti wa kina wa shughuli za kibiashara, utafiti wa sekta isiyo rasmi, utafiti wa huduma za fedha kwa wafanyabiashara wadogo sana, wadogo na wa kati, pamoja na utafiti wa uzalishaji viwandani.

Kwa mujibu wa Msengwa, tafiti hizo zinalenga kukusanya taarifa sahihi zitakazosaidia Serikali na wadau kupanga na kuboresha sera na mipango ya maendeleo ya kiuchumi.

“Tunatambua uwezekano wa matumizi ya AI, lakini tumeweka mfumo unaotuwezesha kumwona kila muhusika mahali alipo. Mfumo hautafunguka kama mtu hajafika eneo la kazi, na akikaa muda mrefu mahali pamoja tutampigia simu kujua sababu. Naonya vijana wasijaribu kufanya hivyo,” amesema.

Amesema vijana hao wamechaguliwa kupitia mifumo ya usajili wa watu wasio na ajira waliokuwa wamejiandikisha kutafuta fursa za kazi.

Kwa mujibu wake, kazi wanayofanya inalenga kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na zisizo rasmi, zikiwemo uzalishaji viwandani, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Amina Msengwa akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dodoma Jana. Picha na Habel Chidawali.

Amesema taarifa zitakazokusanywa zitasaidia kubaini mwenendo wa ukuaji wa biashara nchini na kutoa msingi wa kufanya maamuzi sahihi ya sera na mipango ya maendeleo ya uchumi.

“Pia zitaisaidia Serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti kubuni programu za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, pamoja na kuhuisha takwimu za thamani ya pato ghafi (Gross Output) ili kubaini mchango wa shughuli za kiuchumi,” amesema.

Amesema katika ukusanyaji wa madodoso, taarifa mtambuka zitakusanywa ikiwemo masoko, usimamizi wa mazingira, teknolojia ya mitambo, uwekezaji na changamoto zinazokabili viwanda.

Msengwa amesema taarifa hizo zitaisaidia Serikali kuboresha sera, mikakati na programu za maendeleo ya ujuzi ili kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa.

Amesema utafiti huo utafanyika kuanzia Machi 11 hadi Mei 10, 2026 katika maeneo 1,518 yaliyochaguliwa.

Katika hatua nyingine amesema kutakuwa na utafiti wa mifugo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Benki ya Dunia na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania.