Dar es Salaam. Katika Jiji la Dar es Salaam, ambako shughuli za biashara ndogo ndogo ni mhimili wa maisha ya maelfu ya wananchi, masoko ya umma yanaendelea kuwa kitovu muhimu cha uchumi wa kila siku.
Kwa mujibu wa ofisi ya mkuu mkoa kupitia kitengo cha biashara, jiji hilo lina zaidi ya masoko 60 yanayosimamiwa na halmashauri mbalimbali za mkoa huo.
Pamoja na idadi hiyo kubwa ya masoko, uhalisia unaoonekana katika mengi, ni kwamba nafasi za juu za uongozi zinashikiliwa zaidi na wanaume, huku wanawake wachache wakipata nafasi za uongozi na mara nyingi huishia katika nafasi za ujumbe.
Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti katika Soko la Kigilagila lililopo Kata ya Kiwalani, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam. Miaka tisa iliyopita, wafanyabiashara wa soko hilo walifanya uamuzi usio wa kawaida kwa kumchagua, Neema Charles, kuwa mwenyekiti wao.
Uamuzi huo ulimfanya Neema kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu soko hilo lilipoanzishwa miaka ya 1980 na hadi leo bado anaendelea kuliongoza.
Mwananchi ilifanya mahojiano na Neema, mfanyabiashara wa viungo vya mboga katika soko hilo, akisimulia safari yake ya maisha ya biashara hadi kufikia hatua ya kuwa kiongozi wa wafanyabiashara wenzake.
Neema mwenye umri wa miaka 48 na mkazi wa Yombo Vituka, anasema mapenzi yake kwa biashara yalianza tangu akiwa mdogo. Anasema msukumo mkubwa ulitokana na baba yake ambaye alikuwa mfanyabiashara kijijini kwao Bunda mkoani Mara, akimiliki maduka katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Neema, mazingira hayo ya kukua ndani ya biashara, yalichangia kumjengea hamasa ya kuanza kujifunza mapema.
“Nilianza kujifunza biashara nikiwa bado shuleni. Baada ya kutoka shule nilikuwa nikiuza miwa kwa kupanga barabarani,” anasimulia.
Tabia hiyo ya kujishughulisha na biashara iliiendeleza hata baada ya kuolewa. Mwaka 1992 alihamia jijini Dar es Salaam pamoja na mume wake.
Anasema licha ya mume wake kumshauri abakie nyumbani, yeye aliamua kupingana na wazo hilo kwa sababu tayari alikuwa amezoea kujitegemea kupitia biashara.
Badala yake alianza kufanya biashara ndogo ndogo mbalimbali, safari ambayo baadaye ilimfikisha katika biashara ya soko mwaka 2009. Hapo alianza kuuza viungo mbalimbali vya mboga katika Soko la Kigilagila.
Mwaka 2016, fursa ya uongozi ilijitokeza baada ya kuitishwa uchaguzi wa viongozi wa soko hilo. Ndipo Neema alipoamua kujaribu bahati yake kwa kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti.
Neema anasimulia kuwa katika uchaguzi huo kulikuwa na wagombea watatu waliokuwa wakiwania nafasi ya mwenyekiti. Yeye ndiye alikuwa mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho, huku mmoja wa wagombea akiwa anatetea nafasi yake.
Anasema wakati kampeni zikiendelea, mgombea huyo aliyekuwa anatetea nafasi yake alipoanza kuona ushindani unakuwa mkali, alimshauri Neema akubali kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti badala ya kuwania uenyekiti.
“Alipoona mambo hayaendi vizuri kwake, alinishauri niwe makamu wake. Lakini niliona sina sababu ya kukubali kwa sababu nilikuwa tayari nimeamua kugombea uenyekiti,” anasema Neema.
Anabainisha kuwa kulikuwa pia na mtazamo wa baadhi ya watu kuwa haikuwa rahisi kwa mwanaume kuwa chini ya uongozi wa mwanamke, jambo lililomfanya mpinzani wake aone ni bora aendelee kupambana hadi mwisho na kumpita mgombea huyo kwa kura 16 kati ya kura 70 zilizopigwa.
Akizungumzia namna alivyokuwa akiomba kura, Neema anasema mchakato huo haukuwa mgumu kama alivyotarajia. Wengi wa wafanyabiashara walionyesha kumwamini kutokana na jisi alivyokuwa akijishughulisha na masuala ya soko na kutetea masilahi ya wenzake.
Anasema moja ya mambo yaliyomjengea imani hiyo ni ushiriki wake katika kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo ya masoko. Alikuwa kinara wa shughuli hizo kupitia mradi uliokuwa ukiendeshwa na Shirika la Equal for Growth (EfG), ambao pamoja na mambo mengine, uliwapatia wanawake wa masokoni elimu ya kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Mbali na hilo, Neema anaamini pia kwamba kipaji cha uongozi kiko kwenye damu yake. Anasema katika familia yao yenye watoto 12, licha ya kuwa mtoto wa sita, mara nyingi amekuwa akiongoza ndugu zake katika masuala mbalimbali ya kifamilia.
Sababu nyingine iliyomsukuma kugombea ni kuona wafanyabiashara wa soko hilo wanakosa mtu wa kuwasemea pale wanapokutana na changamoto au wanapokosa fursa mbalimbali.
“Niliona kuna fursa nyingi zinawapita wafanyabiashara wa soko letu, lakini hakuna mtu wa kuzifuatilia au kuwasemea. Nikaona ni bora nijitose ili niweze kusimamia hilo,” anasema.
Anasema katika kipindi chake cha uongozi, baadhi ya mabadiliko yameanza kuonekana. Mojawapo ni kuboreshwa kwa miundombinu ya soko hilo ambalo hapo awali lilikuwa la muda lililojengwa kwa miti, baadaye likaboreshwa na kuwa la kisasa zaidi.
Hata hivyo, Neema anasema anaamini kuwa jitihada hizo ni mwanzo wa safari ndefu ya kuwapa nguvu wafanyabiashara wadogo, hasa wanawake, ili waweze kushiriki kikamilifu katika uongozi na maendeleo ya masoko yao.
Licha ya mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika uongozi wake, anasema bado kuna changamoto kadhaa zinazoendelea kulikabili Soko la Kigilagila na kuathiri maendeleo ya biashara za wafanyabiashara wake.
Kwa muda sasa suala la miundombinu sokoni hapo kuwezesha daladala kufika lilikuwa tatizo. Hata hivyo, Neema anasema baada ya kupaza sauti kwa mamlaka, kwa sasa kuna matengenezo yanaendelea na matumaini ni kuwa siku za usoni biashara itachangamka zaidi katika soko hilo.
Kwa mujibu wa Neema, kukosekana kwa miundombinu hiyo kumesababisha wafanyabiashara wengi kurudi barabarani kufanya biashara zao na kuacha vizimba vyao wazi ndani ya soko, jambo ambalo linaathiri shughuli za biashara kwa ujumla.
Kuhusiana na suala zima la wanawake kuwa viongozi katika masoko, Neema anasema wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza, kwa kuwa kuongoza ni kama unavyoongoza familia yako, tofauti pekee iliyopo ni wale unaowaongoza wapo ambao wa umri mkubwa kukuzidi.
“Hapa ninaongoza watu wazima, wengine ni waasisi wa soko hili, lakini nashukuru tunakaa pamoja, tunapanga mambo yetu na wananisikiliza.
“Hivyo wakina mama wasihofie kujitokeza kuomba nafasi mbalimbali za uongozi katika masoko yao, kwa kuwa wanaweza, kinachohitajika ni kujiamini tu,” anasema Neema.
Akizungumzia matarajio yake siku za usoni, anasema anatamani siku moja kuwa diwani au mbunge anayewakilisha wanawake wa masokoni, akiamini nao watakuwa na mtu wa kuwasemea katika vyombo vya uamuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu.
Walichosema wafanyabiashara wenzake
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya kazi katika soko hilo wamesema wanafurahia uongozi wa mwenyekiti wao.
Suleman Mikolo anasema anajisikia vizuri kuwa na mwenyekiti mwanamke, jambo linaloonyesha namna Watanzania wanavyoendelea kuelimika katika suala la usawa wa kijinsia.
Mikolo ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, akisema kuwa kwa sasa hakuna kazi ya mwanamume wala mwanamke. Anasema hata kumkuta mwanaume akipika vitafunwa si jambo la ajabu tena.
Tatu Sudi anasema mwenyekiti wao amekuwa akipambana kuwatetea na kupigania haki za wafanyabiashara, huku akiendelea kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Akitoa wito kwa jamii, Tatu anasema wanawake wasidharauwe kwa kuwa wanaweza kuwa viongozi wazuri bila kujali kiwango cha elimu walichonacho.
“Kama Rais ni mwanamke kwa sasa na tunaona anavyoiongoza nchi, kwa nini wanawake wengine tushindwe? Naomba kuwapa moyo wanawake wenzangu kwamba tunaweza, hata bila kuwezeshwa,” anasema Tatu.
Kwa upande wake, Juma Bakari anasema licha ya uchaguzi wa viongozi kufanyika kila baada ya miaka mitatu, wafanyabiashara wengi wameamua kumwacha Neema aendelee kuongoza hadi sasa kwa sababu wanaona anawaongoza vizuri.
Naye Godfrey Mngoma anasema Neema ni mchapakazi mzuri. Licha ya kuwa hawezi kumridhisha kila mtu, anasema kwa anayoyafanya wengi wanaridhika nayo.
Edger Mwalimu, mmoja wa wateja wa soko hilo, anasema inapendeza kuwa na mwenyekiti wa soko mwanamke, hasa ukizingatia kwamba wafanyabiashara wengi katika masoko huwa ni wanawake. Hivyo inakuwa rahisi kufikisha changamoto zao na kuzifuatilia zifanyiwe kazi.
“Inapendeza kiongozi wa soko akiwa mwanamke kwa sababu wanawake wengi ndio wapo sokoni. Hivyo ni rahisi kuwazungumzia shida zao na mwanamke anazijua vizuri,” anasema.
