Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza sababu za kuihifadhi Hifadhi ya Ngorongoro huku akiahidi kufanya marekebisho katika uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka ndani ya hifadhi hiyo kama ilivyopendekezwa na Tume alizoziunda.
Rais Samia amebainisha hayo leo Machi 12, 2026 wakati akipokea ripoti kutoka kwa Tume mbili alizoziunda, moja ikichunguza matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro na nyingine ikichunguza uhamaji wa hiari kutoka ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia amesema Ngorongoro ni urithi wa dunia, siyo tu wa Tanzania na uko kwenye vitabu vya dunia chini ya Unesco (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni). Kwa hiyo ni lazima Watanzania ambao wameshushiwa Ngorongoro na Mwenyezi Mungu walinde urithi huo wa dunia.
“Ni eneo pekee ambalo lina kina cha mita 600 kwenda chini na ikazuka hiyo crator kwa miujiza ya Mungu na leo mambo yale yako Tanzania lakini si tu matokeo yale, bali na utajiri uliomo ndani yake.
“Ni eneo ambalo baioanuai yake ni nzuri na haina ushindani duniani, kuna wanyama wa aina zote, walao nyama na majani, ndege wazuri. Kuna vivutio vingi ambavyo sio rahisi kuvikuta kwingineko duniani kwenye bonde moja,” amesema.
Ameongeza kuwa kuna ushahidi wa uwepo wa binadamu wa zamani pale olduvai, ni sehemu muhimu ya kuhifadhiwa. Ngorongoro ni eneo lenye misitu mingi, pia, kuna maeneo ya volcano.
“Kwa hiyo, ni eneo la kuhifadhiwa, ni eneo la kunyeyekewa, kwa faida ya Taifa, lakini kwa faida pia ya ulimwengu au dunia yetu.
“Ni eneo la utalii wa aina nyingi, pale kuna utalii wa game reserve, kuna utalii wa driving, kuna utalii wa kupiga picha, kuna utalii wa aina tofauti tofauti ndani ya eneo moja,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amebainisha kwamba Tume zimetoa mapendekezo ambayo wanakwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha shughuli ya uhamaji wa hiari.
“Taarifa za Tume zimeonyesha umuhimu wa kulinda mifumo ya ikolojia inayounganisha na hifadhi ya Ngorongoro, pori la akiba Pololeti na maeneo ya Ziwa Natron. Haya maeneo ni muhimu sana kwa nchi yetu.
“Maeneo haya ni muhimu kwelikweli, kuna madini yanayotafutwa ulimwenguni, yapo katika maeneo haya. Kwa hiyo ni maeneo ya kuyalinda, ni maeneo muhimu kwa nchi yetu,” amesema kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa: “Tumesikia kwamba Serikali tulifanya shughuli hii kwa nia njema lakini tulikosea baadhi ya maeneo na hayo ndiyo maeneo ya kukaa na kutafakari na kurekebisha. Kwa hiyo tutaedelea na shughuli hii baada ya kurekebisha.”