Ripoti mpya ya utafiti imeibua taswira ya pande mbili katika sekta ya madini nchini, ikionesha mafanikio ya uwekezaji na uwajibikaji wa kampuni, lakini pia ikifichua mapengo ya ushirikishwaji wa jamii, uwazi wa taarifa na mifumo ya kushughulikia malalamiko.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na HakiRasilimali kwa kutumia viwango vya kimataifa vya Towards Sustainable Mining (TSM), imechambua hali ya uchimbaji unaowajibika nchini kwa kutumia mgodi wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Barrick Gold Corporation kama kielelezo cha utafiti.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, “sekta ya madini hutumika kama injini ya uchumi, lakini uchimbaji huacha athari kubwa kwa mazingira na maisha ya watu wanaouzunguka.” Kauli hiyo inaweka mizani kati ya mchango wa kiuchumi na gharama za kijamii na kimazingira.
Ripoti inaonesha kuwa migodi huchangia ujenzi wa shule, zahanati na barabara, pamoja na kutoa ajira kwa wakazi wa maeneo jirani. Pia umeweka mifumo ya ufuatiliaji wa ubora wa maji na mitetemo ya milipuko.
Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa licha ya uwepo wa mifumo hiyo, jamii nyingi hazipati taarifa za moja kwa moja kuhusu matokeo ya vipimo hivyo. Mkazi mmoja alinukuliwa akisema:
“Hakujawahi kuwa na mkutano wa moja kwa moja kati ya mgodi na sisi wananchi. Vikao vinafanyika kati ya mgodi na viongozi wetu, na hatujui kinachoendelea.”
Ripoti inaeleza kuwa mfumo wa mawasiliano unaotegemea viongozi wa vijiji pekee umeunda kile ilichokiita “bottleneck effect”, ambapo taarifa hubaki katika ngazi ya viongozi bila kuwafikia wananchi wote.
Katika maeneo yanayozunguka mgodi, baadhi ya wakazi wamelalamikia vumbi linalotokana na malori ya uchimbaji, wakihusisha hali hiyo na matatizo ya mfumo wa hewa, hasa kwa watoto.
“Tuna tatizo kubwa la vumbi kutoka kwenye malori ya mgodi. Ukienda zahanati, utaona watoto wanakuja kila siku na matatizo ya kifua,” alinukuliwa mkazi mmoja.
Kuhusu milipuko, wananchi wameeleza wasiwasi juu ya nyufa kwenye nyumba zao, wakihusisha na mitetemo ya milipuko ya miamba.
“Milipuko imesababisha nyufa kwenye nyumba zetu. Serikali ilikuja kupima mitetemo lakini hatukuambiwa matokeo, hivyo hatujui kama nyumba zetu ziko salama.”
Ripoti inasisitiza kuwa hata kama viwango vya kitaalamu vinafuatwa, ukosefu wa uwazi wa matokeo huongeza hofu na kupunguza imani ya jamii.
Vilevile ripoti pia imechambua mfumo wa kupokea na kushughulikia malalamiko, ikieleza kuwa upo kisheria lakini unakabiliwa na changamoto za upatikanaji.
Ripoti inadai kuwa malalamiko hupitishwa kupitia ofisi za vijiji kwenda kwa Afisa Mahusiano ya Jamii (CRO), ambaye ofisi yake ipo ndani ya uzio wa mgodi. Hali hiyo imetajwa kuwa kikwazo kwa wananchi kufuatilia masuala yao kwa urahisi.
Katika ripoti hiyo inapendekezwa kuwa na mfumo wa wazi wa kufuatilia malalamiko hadi yatakapopatiwa majibu badala ya kutegemea viongozi pekee na kutoa hadharani matokeo ya vipimo vya maji, hewa na mitetemo.
Kadhalika imependekezwa kuwa na ofisi ya CRO nje ya uzio wa mgodi ili kurahisisha upatikanaji, kuhakikisha miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) inakidhi mahitaji halisi ya wananchi na kutoa elimu juu ya fursa za wazawa ili kudhibiti matarajio yasiyo halisi.
Inasisitiza kuwa rasilimali zilizopo zinaweza kuimarisha uchumi, lakini bila uwazi na ushirikishwaji wa wananchi, changamoto za kijamii na kimazingira zinaweza kuathiri uendelevu wa sekta hiyo.
“Suluhu la hali hii si kuzingatia viwango vya kimataifa pekee, bali kuvitafsiri katika muktadha wa Tanzania na kutekeleza kwa vitendo,” inasisitiza ripoti hiyo.
Kuhusu yanayoelezwa katika ripoti hiyo Afisa Mawasiliano wa kampuni ya Barrick nchini, Neema Ndossi anasema mgodi huo unaendesha kwa ambazo zinahakikisha hakuna malalamiko kama hayo yaliyoainishwa katika ripoti hiyo.
Kuhusu Suala la vumbi Ndossi anasema malalamiko ya vumbi hayaakisi muktadha halisi wa mgodi wa Bulyanhulu kwani mgodi wao unafanya shughuli zake chini ya ardhi a hakuna hata magari yanayosafirisha malighafi kwenda kijiji jirani.
“Shughuli zinazofanyika juu ardhi ni chache na zimedhibitiwa, ukaguzi wa vumbi hufanyika mara kwa mara kupitia mpango wetu wa kudhibiti vumbi na ulinzi wa mazingira, matokeo ya tathimini tunazozifanya yanapimwa kwa kuzingatia viwango vya udhibiti vya Tanzania na vya kimataifa,” anasema Ndossi.
Suala la mitetemo pia anasema haliwezi kujitokeza kwa wakazi wa meneo la mgodi kutokana na kufanya shughuli zake chini ya ardhi na vilipuzi vyote vinakuwa utaratibu wa udhibiti wa mitetemo.
“Mlipuko imeundwa, kupangwa na hulipuliwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu vilivyowekwa kuhakikisha kuwa mitetemo juu ya ardhi inakuwa kwa kiwango kinachokubalika (ambacho hakiwezi kuleta madhara),” alisema Ndossi.
Ndosi anasema mgodi huo una mfumo wa kupima viwango vya mtetemo mara kwa mara ka kuripoti kwa vyombo vya Serikali kama inavyotakiwa na vyombo hivyo vina mamlaka ya kuangalia uzingatiaji wa viwango kwa kuwanya uchunguzi huru hivyo vinaweza kutoa tathimini ya kuamika.
Kadhalika Ndossi anasema mgodi huo una ofisi ya mahusiano ya jamii nje ya mgodi kwa ajili ya jamii Kituo cha malalamiko na katika kupokea maoni na malalamiko wanafuata misingi ya viwango vya kimataifa inayotaka ufikiaji rahisi na kwa uwazi.