Tahadhari utegemezi wa akili unde kama mbadala wa mawasiliano ya binadamu

Dar es Salaam. Wataalamu wa saikolojia wameonya juu ya hatari inayoweza kujitokeza ikiwa watu wataanza kutegemea teknolojia ya akili unde (AI) kama mbadala wa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya ya binadamu na mwingine.

Ingawa teknolojia ya AI imeleta urahisi katika kupata taarifa na majibu ya haraka, wataalamu wanasema matumizi yake kupita kiasi yanaweza kudhoofisha mahusiano ya kijamii, kuongeza upweke na kupunguza uwezo wa watu kujenga uhusiano wa karibu na wenzao.

Wataalamu wanasema endapo watu wataanza kuitegemea sana AI kwa mazungumzo au ushauri wa maisha, kuna uwezekano wa kupungua kwa mawasiliano ya kijamii na kuongezeka kwa hisia za upweke.

Mwanasaikolojia Amina Hassan amesema mawasiliano ya ana kwa ana yana nafasi muhimu katika kujenga uhusiano, kuimarisha uelewano na kusaidia watu kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za maisha.

 “Teknolojia inaweza kusaidia kupata taarifa au majibu ya haraka, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya hisia za kibinadamu kama huruma, upendo au uelewa wa kina unaotokea katika mazungumzo ya watu wawili,” amesema.

Mtaalamu mwingine wa saikolojia, Josephine Mallya amesema vijana wako hatarini zaidi kwa kuwa bado wanajifunza jinsi ya kujenga uhusiano wa kijamii.

“Ujuzi wa kijamii unajengwa kupitia mazungumzo ya ana kwa ana, ambapo mtu anajifunza kusoma lugha ya mwili, sauti na hisia za mwenzake. Utegemezi mkubwa wa akili unde unaweza kuathiri ukuaji wao wa kijamii na kihisia,” amesema.

Baadhi ya vijana wameripoti kutumia programu za akili unde mara kwa mara kupata ushauri kuhusu masomo, kazi na mahusiano.

Kelvin Joseph (24), mkazi wa Sinza, amesema: “Nikitumia AI napata maelezo ya kina yanayonisaidia kufikiria zaidi.”

Halima Abdallah, mwanafunzi wa chuo kikuu, amesema: “Teknolojia inasaidia masomo yangu na kunipa mawazo mapya.”

Hata hivyo, wataalamu wanatabiri kuwa utegemezi wa akili unde unaweza kuathiri uhusiano ndani ya familia.

Mwanasaikolojia wa jamii, Peter Mrema amesema mazungumzo ya familia ni muhimu katika kujenga uaminifu na mshikamano.

“Ikiwa watu wataanza kuzungumza na akili unde badala ya wanafamilia, uhusiano wa kifamilia unaweza kudhoofika zaidi,” amesema.

Aidha, wataalamu wanasema baadhi ya vijana wanavutiwa zaidi na AI kwa sababu hayahusishi hukumu au ukosoaji.

Mwanasaikolojia Grace Lwakatare amesema: “Wakati mwingine vijana wanahisi ni rahisi zaidi kuzungumza na AI kwani hawahisi kuhukumiwa, lakini hatari ni kwamba wanaweza kukosa kujifunza kukabiliana na maoni tofauti au changamoto zinazotokea katika mazungumzo ya kawaida.”

Pia, utegemezi wa AI unaweza kuathiri maamuzi muhimu ya maisha.

Mchambuzi wa teknolojia, David Mushi amesema: “AI inatoa majibu kulingana na taarifa ilizofundishwa. Haina uwezo wa kuelewa hali halisi ya mtu au changamoto anazokutana nazo. Si salama kuitumia kama mshauri pekee katika maamuzi muhimu.”

Mtaalamu wa usalama wa mitandao, Jenita Mwakalobo amesisitiza kuwa watumiaji wanapaswa kuwa waangalifu wanapoweka taarifa binafsi kwenye majukwaa ya kidijitali, kwani kuna hatari ya taarifa hizo kuhifadhiwa au kutumika kinyume na mapenzi yao.

Wataalamu wanahimiza kutumia akili unde kwa uwiano, kama chombo cha kujifunza na kupata mawazo mapya, bila kuathiri mahusiano ya kijamii.

“AI ni nyenzo nzuri ya kujifunza, lakini bado tunahitaji mazungumzo ya ana kwa ana. Teknolojia inapaswa kusaidia maisha ya binadamu, si kuchukua nafasi yake,” amesema Mushi.