Global Publishers
March 12, 2026
0 Comments
Donald Trump amesema mamlaka za usalama nchini Marekani zinachunguza taarifa za uwezekano wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drone) kutoka Iran, yanayoweza kulenga jimbo la California kama kisasi cha vita vinavyoendelea kati ya Marekani na Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika kituo cha kijeshi cha Joint Base Andrews kufuatia mkutano wa kisiasa huko Kentucky, Trump alisema vyombo vya sheria vinafanyia kazi taarifa hizo.
“Inachunguzwa. Kuna mambo mengi yanayoendelea na tunachoweza kufanya ni kuyachunguza kadri yanavyokuja,” alisema Trump.
Hofu ya uwepo wa makundi ya siri ya washambuliaji ilianza baada ya mawasiliano ya siri, yanayodaiwa kutoka ndani ya Iran na kunaswa na Marekani, kuripotiwa kuwa yalitumwa kama ishara ya kuanzisha operesheni.
Siku ya Jumatano, Federal Bureau of Investigation (FBI) pia ilitoa tahadhari kwa vyombo vya usalama vya California kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya drone kwenye pwani ya Magharibi ya Marekani kama hatua ya kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran.
Katika maelezo yake, Trump pia alimlaumu aliyekuwa rais wa zamani Joe Biden kuwa sera zake za uhamiaji, akidai zilichangia uwezekano wa kuwepo kwa watu wanaoweza kufanya mashambulizi hayo ndani ya Marekani.
Wakati huo huo, Trump alisema operesheni za kijeshi dhidi ya Iran zinaendelea na kudai kuwa Jeshi la Marekani limeharibu sehemu kubwa ya uwezo wa kijeshi wa Iran baharini, akisisitiza kuwa hali iko katika mwelekeo mzuri.
Tahadhari hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, huku Iran ikitajwa kutumia sana drones na mashambulizi ya mtandao (cyber attacks) kama mbinu za kujibu mashambulizi ya kijeshi.