Usipojipanga BDL imekula kwako | Mwanaspoti

WAKATI timu zikisubiri kutangaziwa tarehe ya kuanza kwa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), timu zitakazoshindwa kujipanga vizuri huenda zikajikuta zikikumbana na vichapo vya kushangaza kutokana na namna ambavyo maanadalizi yanaendelea.

Ugumu kwa baadhi ya timu hizo huenda ukachangiwa na ubora wa timu zoefu zilizopo katika ligi hiyo ambazo husajili wachezaji wazoefu wenye viwango vikubwa kutoka ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya timu zinazotakiwa zijipange kutokana na uwezo wa timu kongwe ulivyo ni pamoja na Magone, Mlimani BC, Mchenga BC, Kurasini Heat na Ukonga Kings.

Timu ya Magone inayoundwa na wachezaji wengi wenye viwango vya kati, inawapasa wasajiri wachezaji wenye uwezo mkubwa, itakayofanya itoe ushindani katika ligi hiyo.

Bila kufanya hivyo, itawafanya wawe na wakati mgumu kuhimili mikikimikiki ya BDL, mwaka huu.

Timu ya Magone, ambayo ni timu ya pili ya Savio, ilipanda daraja mwaka huu baada ya kuifunga timu ya KR One katika michezo 2-0, ikishika nafasi ya tatu.

Mlimani BC ambayo ni timu ya pili ya UDSM Outsiders, inaonyesha itakuwa na wakati mgumu endapo haitaongeza wachezaji wengine katika kikosi chake kwa ajili ya BDL.

Bila kufanya hivyo matokeo ya timu hiyo huenda yakaathiriwa na viwango vya mastaa ilionao ikizingatiwa karibu timu zote zimejimarisha kwa kusajili mastaa wa kimataifa wenye uwezo mkubwa na wachezaji bora wazawa.

Katika Ligi ya Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam, timu hiyo ilikuwa inajivunia kuwa na mchezaji wa kimataifa, Mtala Djedje kutoka DR Congo. Mbali ya kumsajili mchezaji huyo, inawapasa kuongeza wengine wenye uwezo mkubwa wa kuhimili mikikimikiki ya ligi ngumu. Mlimani BC ilipanda daraja mwaka huu baada ya kuifunga Ukonga Kings katika fainali ya Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam katika michezo 2-0.

Ukongwe wa Ukonga Kings unaweza kuisaidia kufanya vizuri katika BDL mwaka huu kutokana na uzoefu wake, licha ya kwamba ilishuka daraja 2024.

Katika maandalizi timu hiyo inapaswa kuwa na uangalifu katika usajili isije ikapotea kirahisi na kurudi Daraja la Kwanza.  Ukonga Kings ilipanda daraja mwaka huu baada ya kushika nafasi ya pili katika ligi hiyo. Timu hiyo ilifungwa na Mlimani BC katika fainali.

Mchenga BC ni kati ya timu zinazopaswa kuwa na tahadhari kwani nayo isipojipanga vizuri katika ligi hiyo inaweza kuiona kuwa ni ngumu.

Ugumu kwa timu hiyo unatokana na kushindwa kusajili wachezaji wenye uzoefu mkubwa, hali iliyofanya ishike nafasi ya 12 kwa pointi 19 katika msimamo msimu uliopita.

Akizungumzia kuanza kwa BDL, Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Kikapu Dar es Salaam (BD), Shabani Mahobonya anasema tarehe ya kuanza kwa ligi hiyo itatangazwa baada ya kamati ya mashindano ya BDL kukutana na uongozi wa chama.