Vita Iran yatikisa soko la nishati, Ujerumani, Austria kutoa akiba ya mafuta

Dar es Salaam. Nchi za Ujerumani na Austria zimetangaza kuanza kuachia sehemu ya akiba yao ya mafuta kufuatia ombi la Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IEA) kwa nchi wanachama kutoa jumla ya mapipa milioni 400 ya mafuta, ili kupunguza kupanda kwa bei ya nishati duniani kunakosababishwa na vita vya Iran.

Hatua hiyo inakuja wakati hali ya soko la nishati duniani ikiendelea kuwa tete kutokana na mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati. Pia Japan imetangaza itaanza kuachia sehemu ya akiba yake ya mafuta kuanzia Jumatatu ijayo.

Kwa mujibu wa ABC News mawaziri wa nishati wa nchi za Group of Seven (G7) walikutana Jumanne makao makuu ya IEA mjini Paris, Ufaransa, kujadili hatua za kukabiliana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo muhimu.

Mkurugenzi Mkuu wa IEA, Fatih Birol amesema wamejadili mbinu zote ikiwa ni pamoja na kutoa hifadhi ya dharura ya mafuta ya shirika la IEA na kuruhusu kuingia kwenye soko la dunia.

Kwa mujibu wa IEA, hatua kubwa zaidi kuwahi kuchukuliwa hapo awali ya kuachia akiba za dharura ilikuwa mapipa milioni 182.7 mwaka 2022 kufuatia upungufu wa nishati uliosababishwa na uvamizi kamili wa Russia nchini Ukraine.

Kwa sasa, nchi wanachama wa IEA zinamiliki zaidi ya mapipa bilioni 1.2 ya akiba ya mafuta ya dharura inayomilikiwa na serikali, huku sekta binafsi ikiwa na takriban mapipa milioni 600 chini ya usimamizi wa serikali.

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Katherina Reiche, amesema nchi yake itatekeleza ombi la IEA la kuachia akiba ya mafuta inayofikia mapipa milioni 400 (sawa na takribani tani milioni 54).

Amesema itachukua siku chache kabla ya shehena za kwanza kuanza kuingia sokoni, akisisitiza Ujerumani inaunga mkono kanuni ya mshikamano kati ya nchi wanachama wa IEA.

Wakati huohuo, mvutano umeongezeka baada ya Iran kushambulia meli za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel.

Mashambulizi hayo yameathiri usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, njia muhimu ambayo hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani kutoka Ghuba ya Uajemi kuelekea Bahari ya Hindi.

Ripoti pia zinaeleza Iran imelenga vituo vya mafuta na mitambo ya kusafisha mafuta katika nchi za Kiarabu za Ghuba ili kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Marekani na Israel kusitisha mashambulizi yao.

Katika hatua nyingine, serikali ya Ujerumani imesema itaweka utaratibu mpya wa kudhibiti bei za mafuta katika vituo vya mafuta, ambapo vitaruhusiwa kuongeza bei mara moja tu kwa siku.

Kwa upande wake, Waziri wa uchumi wa Austria, Wolfgang Hattmannsdorfer, amesema nchi hiyo pia itaachia sehemu ya akiba yake ya dharura ya mafuta na kuongeza akiba ya kimkakati ya gesi.

Kuanzia Jumatatu, Austria itaruhusu vituo vya mafuta kuongeza bei mara tatu tu kwa wiki katika jitihada za kuwalinda watumiaji dhidi ya mfumuko wa bei.