VODACOM TANZANIA FOUNDATION YAKABIDHI MATUNDU 10 YA VYOO SHULE YA MSINGI MKATA.

-Vodacom Tanzania Foundation Imejenga matundu 10 ya vyoo Shule ya Msingi Mkata

Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Twende Butiama pamoja na Stanbic Bank wamejenga matundu 10 ya kisasa ya vyoo katika Shule ya Msingi Mkata iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Akipokea matundu hayo 10 ya vyoo kutoka kwa Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kaskazini, Andrew Temu, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Yibarila Chiza alisema vyoo hivyo vitasaidia kulinda afya za wanafunzi pamoja na kuwafanya kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya vyoo bora na vya kisasa majumbani mwao.

Aidha alisema kuwa vyoo hivyo vitachochea ufaulu wa wanafunzi kwa kupunguza changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo katika shule hiyo, na hivyo kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia. Alitoa shukrani kwa wadau hao kwa msaada huo walioutoa kwa shule hiyo.

Kwa upande wake, Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kaskazini, Andrew Temu, alisema Vodacom Tanzania Foundation inaangazia maeneo matatu makuu ambayo ni afya, mazingira na elimu.

Alisema ili mwanafunzi aweze kusoma vizuri anahitaji kuwa katika mazingira rafiki yasiyokuwa na msongo wa mawazo, hivyo ujenzi wa vyoo hivyo utasaidia wanafunzi hasa wenye mahitaji maalum na kuwapa muda zaidi wa kukaa darasani badala ya kupoteza muda kusubiri foleni ya huduma ya choo.

Naye Mwenyekiti wa msafara wa Twende Butiama, Gabriel Landa, alisema wao kama Twende Butiama wameamua kutumia baiskeli kama njia ya kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuhamasisha wananchi kuboresha sekta za afya, elimu na mazingira kupitia programu mbalimbali za uhamasishaji.

Awali akitoa taarifa ya shule, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mkata, Daliana Majatta, alisema matundu hayo ya vyoo yamesaidia kupunguza uhitaji wa vyoo katika shule hiyo, ingawa bado wanahitaji jumla ya matundu 28 ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

“Pamoja na mafanikio hayo, shule yetu bado ina changamoto mbalimbali zinazoifanya isiwe ya kisasa zaidi, ikiwemo miundombinu ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na upungufu wa madawati 300, wakati idadi ya wanafunzi ni 2,023,” alisema Majatta.

Mbali na ujenzi wa matundu hayo 10 ya vyoo, Vodacom Tanzania Foundation pia imewahi kutoa misaada mbalimbali katika shule hiyo ikiwemo viti mwendo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, magodoro, vitanda pamoja na mashuka.
Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kaskazini, Andrew Temu, akizungumza wakati wa makabidhiano ya matundu 10 ya vyoo vya kisasa vilivyojengwa na Vodacom Tanzania Foundation katika Shule ya Msingi Mkata iliyopo wilayani Handeni mkoani Tanga. Ujenzi wa vyoo hivyo unalenga kutimiza dhamira ya Vodacom ya kuchangia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wote, huku ikiangazia afya na ustawi wa wanafunzi kupitia miradi ya maendeleo ya jamii. Tukio hilo lililofanyika jana lilihudhuriwa na Yibarila chiza, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Handeni (kulia), Meneja Uhusiano wa masuala ya serikali wa Vodacom Tanzania Grace Lyon (Kushoto), Mwenyekiti wa Msafara wa Twende Butiama Gabriel Landa (Wa pili kushoto) pamoja na wazazi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Timu ya Vodacom, Wawakilishi wa Twende Butiama na Walimu wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kufunguliwa kwa vyoo vipya vya kisasa vilivyotolewa na Kampuni ya Mawasiliano na teknolojia ya Vodacom Tanzania Plc katika Shule ya Msingi Mkata, iliyoko wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Bw Yibarila Chiza na Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Plc Kanda ya Kaskazini, Andrew Temu wakikata utepe ikiwa ni ishara ya kufungua rasmi vyoo vya kisasa 10 vilivyojengwa na Kampuni hiyo katika shule ya Msingi Mkata wilayani Handeni mkoani Tanga, Vodacom imetimiza ahadi iliyotolewa kwa shule hiyo wakati wa msafara wa waendesha baiskeli wa ‘Twende Butiama’ uliopita shuleni hapo mwaka jana ikiwa ni ishara ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwl JK Nyerere. Tukio Hilo lilifanyika jumatatu wiki hii mjini Mkata.

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mkata iliyopo wilayani Handeni Mkoani Tanga, wakifurahia uwepo wa vyoo vipya na vya kisasa 10, vilivyotolewa na Kampuni ya Mawasiliano na Teknolojia ya Vodacom Tanzania. Vyoo hivi vinalenga kuboresha mazingira ya kujisomea ya wanafunzi hao.