Vodacom Wakabidhi Matundu 10 ya Vyoo Shule ya Mkata

Bakari Mahundu
March 12, 2026
0 Comments

Vodacom Tanzania Foundation, Twende Butiama pamoja na Stanbic Bank Kwenye Picha ya Pamoja Wakizindua Matundu 10 ya Kisasa ya Vyoo Shule ya Msingi ya Mkata, Tanga.

Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na Twende Butiama pamoja na Stanbic Bank wamejenga matundu 10 ya kisasa ya vyoo katika Shule ya Msingi ya Mkata iliyopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

Akipokea matundu hayo 10 ya vyoo kutoka kwa Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kaskazini, Andrew Temu, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Handeni, Yibarila Chiza alisema vyoo hivyo vitasaidia kulinda afya za wanafunzi pamoja na kuwafanya kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya vyoo bora na vya kisasa.

Amesema vyoo hivyo vitachochea ufaulu wa wanafunzi kwa kupunguza changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo katika shule hiyo hivyo kuwawezesha kupata mazingira bora ya kujifunzia.
Ametoa shukrani kwa wadau hao kwa msaada huo walioutoa kwa shule hiyo.

Kwa upande wake, Meneja Mauzo Mwandamizi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kaskazini, Andrew Temu amesema Vodacom Tanzania Foundation inaangazia maeneo matatu makuu ambayo ni afya, mazingira na elimu.

Amesema ili mwanafunzi aweze kusoma vizuri anahitaji kuwa katika mazingira rafiki yasiyokuwa na msongo hivyo ujenzi wa vyoo hivyo utasaidia wanafunzi hasa wenye mahitaji maalum na kuwapa muda zaidi wa kukaa darasani badala ya kupoteza muda kusubiri foleni ya huduma ya choo.
Naye Mwenyekiti wa Msafara wa Twende Butiama, Gabriel Landaamesema wao kama Twende Butiama wameamua kutumia baiskeli kama njia ya kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuhamasisha wananchi kuboresha sekta za afya, elimu na mazingira.

Awali, akitoa taarifa ya shule, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Mkata, Daliana Majatta amesema matundu hayo ya vyoo yamesaidia kupunguza uhitaji wa vyoo katika shule hiyo, ingawa bado wanahitaji jumla ya matundu 28 ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
Mbali na ujenzi wa matundu hayo 10 ya vyoo, Vodacom Tanzania Foundation pia imewahi kutoa misaada mbalimbali katika shule hiyo ikiwemo viti-mwendo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, magodoro, vitanda pamoja na mashuka.