Tanga. Imedaiwa kuwa, miongoni mwa vyanzo vikuu vya migogoro ya ardhi mkoani Tanga ni walinzi waliokuwa wamepewa jukumu la kusimamia mashamba, kujitwalia mali hizo baada ya wamiliki kufariki dunia.
Malalamiko hayo yameibuliwa katika Kliniki ya Sheria, iliyo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, iliyowekwa kambi mkoani Tanga.
Kliniki hiyo ilianzishwa baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kufanya ziara mkoani humo na kubaini uwepo wa migogoro mingi ya ardhi huku akiahidi kuchukua hatua za haraka.
Siku chache baada ya ziara hiyo, jopo la mawakili takriban 40 limepelekwa mkoani humo, miongoni mwa changamoto walizobaini ni walinzi waliokuwa wakisimamia mashamba kujimilikisha mali hizo baada ya wamiliki kufariki dunia.
Kliniki hiyo iliyoanza Machi 9, 2026 inatarajiwa kumalizika Machi 15, 2026, ikiwa na lengo la kuwapatia wananchi ushauri wa kisheria na msaada bila malipo kuhusu changamoto mbalimbali za kisheria wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.
Baadhi ya wananchi wamesema walinzi waliokuwa wakisimamia mashamba ya familia hubadilisha msimamo baada ya wamiliki kufariki dunia na kuanza kudai mali hizo ni zao, wakidai walipewa au kuuziana na marehemu kabla ya kifo chake.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 12, 2026, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Silinde Gumada amesema miongoni mwa migogoro inayojitokeza ni ile inayohusisha walinzi waliokuwa wakipewa jukumu la kusimamia mali, ambao baada ya kifo cha wamiliki huanza kudai kuwa mali hizo ni zao.
“Wapo waliokuwa wamepewa jukumu la kusimamia mashamba au nyumba kwa muda, lakini baada ya mmiliki kufariki, wanaanza kudai eneo ni lao au walipewa na marehemu. Hali hii imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro kati yao na warithi wa marehemu,” amesema Gumada.
Amesema baadhi ya walinzi wanaenda mbali kwa kutengeneza nyaraka bandia za mauziano ili kuhalalisha madai yao.
Gumada amesisitiza umuhimu wa jamii kuweka utaratibu wa kisheria, ikiwamo kuandika makubaliano rasmi ya usimamizi wa mali ili kuthibitisha jukumu la mtu na si kumiliki.
Amesema mengine ni kusajili mali kama ardhi au nyumba kwa mujibu wa sheria, kuandika wosia ili kubainisha urithi wa mali kabla ya kifo, kuhusisha mashahidi wa familia au viongozi wa kijiji pale mtu anapopewa jukumu la kusimamia mali na kuweka kumbukumbu sahihi za umiliki na matumizi na viongozi wa vijiji ili kutatua migogoro mapema.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Tanga, Mariam Rashid amesema amefika katika kliniki hiyo kuomba msaada wa kisheria baada ya kukumbana na mgogoro wa shamba la familia yao lililokuwa likisimamiwa na mlinzi.
“Baada ya baba yetu kufariki, aliyekuwa analinda shamba alianza kudai ni lake akisema alikabidhiwa na marehemu. Tulipomwomba atuoneshe nyaraka za makabidhiano akashindwa kufanya hivyo,” amedai Mariam.
Mkazi mwingine wa Tanga, Salum Heri amesema amewasilisha malalamiko katika kliniki hiyo baada ya kuzuka mgogoro wa shamba la minazi lililokuwa limetolewa kwa mtu kwa ajili ya kugema minazi pekee.
Heri amedai mtu aliyepwa ruhusa ya kugema minazi amefariki dunia na ndugu zake wameanza kudai kuwa shamba lote la minazi ni la ndugu yao.
“Yule mtu alipewa tu ruhusa ya kugema minazi, hakukabidhiwa shamba, lakini baada ya kufariki, ndugu zake sasa wanadai shamba lote ni lao,” amedai Heri.
