Chanzo ajali iliyoua watumishi wa afya Kigoma, Rais atoa pole

Kigoma/Dar. Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kufuatia vifo vya watumishi sita wa sekta ya afya waliopoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kwa mamlaka za uokoaji, chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali uliovuma ziwani na kusababisha mawimbi makubwa yaliyoifanya boti hiyo kupinduka na kuzama.

Tukio hilo lilitokea leo Ijumaa, Machi 13, 2026 saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Kalalangabo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakati watumishi hao wakiwa njiani kwenda kutoa huduma za chanjo kwa wananchi.

Watumishi waliopoteza maisha katika ajali hiyo wametajwa ni Joyce Kandole, Winfrida Bisunga, Rachel Msabila, Paul Lovanda, Amos Sika pamoja na Omar Kalima ambaye hakuwa mtumishi wa sekta ya afya.

Mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma idara ya afya, Rachel Msalila aliyefariki dunia kwenye ajali ya boti.

Taarifa zilieleza miili hiyo itaagwa kesho Jumamosi ili isafirishwe kwanda kwao kwa mazishi.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Michael Maganga amesema pamoja na watu sita waliothibitika kufariki dunia na miili yao kupatikana, bado watatu waliokuwa kwenye boti hiyo ambao hawajapatikana na.

Amesema watu wengine tisa waliokuwamo katika boti hiyo, wameokolewa na walikuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema boti hiyo ilionekana ikikimbia upepo mkali kabla ya kupinduka. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ziwani, Habibu Ibrahim alisema waliona boti hiyo ikiingia karibu na ufukwe ikijaribu kukwepa upepo mkali kabla ya kuzama.

Mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma, Winifrida Bisunga aliyefariki dunia kwenye ajali ya boti.

“Baada ya muda tuliiona boti ikipinduka na kuzama. Tulichukua mitumbwi iliyokuwa karibu na kukimbilia ziwani umbali wa takribani mita 40 kutoka ufukweni kuanza kuokoa watu waliokuwa ndani,” amesema Ibrahim.

Kwa mujibu wa mashuhuda, baadhi ya waliopoteza maisha walikwama ndani ya boti kutokana na turubai lililokuwa limefunika juu ya chombo hicho, huku wengi wao wakiwa hawajui kuogelea.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro ambaye alifika katika eneo la tukio, amesema Serikali itaendelea kutoa msaada unaohitajika kwa familia za marehemu na waathirika wa ajali hiyo huku juhudi za kuwatafuta waliopotea zikiendelea.

Sirro ambaye pia mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taarifa za hali ya hewa pamoja na kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri vinavyotumika katika ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kuepusha matukio kama hayo siku zijazo.

Katika salamu zake za rambirambi zilizotolewa kupitia Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, Rais Samia amesema Taifa limepoteza watumishi jasiri waliokuwa wakitekeleza wajibu wao wa kuhakikisha huduma muhimu za chanjo zinawafikia wananchi.

Boti ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma iliyokuwa imebeba watumishi wa halmashauri hiyo kutoka Kigoma mjini kwenda kijiji cha Kagunga kwa shughuli ya kutoa chanjo.

Alisema Serikali inaungana na familia za marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, ikiendelea kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na Mwenyezi Mungu awape nguvu, uvumilivu na faraja wote walioguswa na msiba huu mkubwa.

Alisema mchango na dhamira ya watumishi hao katika kulinda afya ya wananchi hautasahaulika, Taifa litawakumbuka kama mashujaa wa huduma ya afya waliotoa maisha yao wakiwa mstari wa mbele kuwatumikia Watanzania.

“Natoa pole kwa familia za marehemu, ndugu, jamaa na watumishi wote wa sekta ya afya. Taifa limepoteza watumishi waliokuwa tayari kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kuokoa na kulinda maisha ya Watanzania wenzao,” amesema Rais Samia.

Kabla ya salamu za Rais, Mchengerwa ambaye amezitoa wakati akizungumza na watumishi wa afya Hosptali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dar es Salaam amesema, “Kwa masikitiko makubwa na huzuni nzito, tumepokea taarifa ya vifo vya watumishi sita wa Sekta ya Afya waliopoteza maisha kwa ajali ya kuzama kwa boti wakiwa njiani kwenda kutoa huduma ya chanjo mkoani Kigoma.

“Watumishi hawa walikuwa wakitekeleza wajibu wao wa kulinda afya na maisha ya Watanzania wenzao, wakisafiri kwa dhamira ya kuhakikisha huduma muhimu za chanjo zinawafikia wananchi.”

Vifo hivyo ni pigo kwa mkoa wa Kigomaa unaokabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi.

Julai 13, 2025 Mwananchi ilichapisha habari ya uchunguzi iliyofanywa katika baadhi ya zahanati za Mkoa wa Kigoma za Muhunga na Kitagala wilayani Kasulu, Kalalangabo na Simbo iliyopo Kigoma Vijijini kuwa zina watumishi wawili kila moja, wanaosaidiwa na watumishi wa afya ngazi ya jamii. Kituo cha Afya Bunyambo wilayani Kibondo kilikuwa na watumishi sita.

Hali hii ya uchache wa watumishi imekuwa ikisababisha wananchi kuchukua muda mrefu kupata huduma, moja ya zahanati ikianzisha huduma ya uji wa lishe kwa watoto siku wanapopelekwa kliniki.

Licha ya changamoto hiyo, ilibainika kuwa baadhi ya maeneo mkoani humo kuna zahanati na vituo vya afya katika wilaya ya Kibondo vilikuwa vikifungwa kutokana na uhaba wa watumishi, hivyo kuwalazimu watumishi kutoka halmashauri kwenda kutoa huduma ya mkoba angalau mara mbili kwa wiki.

Makala hiyo ilibainisha changamoto zilizopo, huku uongozi wa mkoa ukitaja chanzo cha tatizo na mikakati iliyopo katika utatuzi.