Msando amekabidhi magari hayo leo wilayani Ubungo mkoani Dar es Salaam, kwa Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kinondoni Kusini, ambako amesema usafiri huo utaenda kuongeza chachu ya utoaji hudu ikiwemo kuwawezesha watumishi kufika kwa wakati katika maeneo yenye changamoto.
Amesema hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuendelea kuboresha huduma ya umeme, na kwamba ili shirika liendelee kutoa huduma bora ni lazima liwe na vitendea kazi vitakavyowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Tunaishukuru serikali chini ya Rais samia kwa kuliwezesha shirika kupata vifaa hivi muhimu katika utendaji wao, sisi kama Wilaya ya Ubungo tutahakikisha vifaa hivi vinasimamiwa vizuri ili viweze kuleta tija katika eneo letu, ikiwemo kufika kwa haraka kwenye maeneo ya utoaji huduma kwa wananchi,” amesema Msando.
Ameongeza kuwa vifaa vyenye ubora na ufanishi ni muhimu sana katika utendaji na usimamizi wa shughuli za TANESCO, na kwamba wanaamini kuwa watendaji wataenda kusimamia vizuri vifaa hivyo na kuwawezesha kuongeza tija kwenye utoaji huduma kwa jamii.
Aidha, ameeleza kuwa hayo yote yanafanyika kwasababu serikali iliahidi kuendelea kuboresha huduma ya umeme, mijini na vijijini, akisema Rais anathibitisha hilo kwa vitendo kufikia malengo ambayo wamejiwekea kama taifa.
“Nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange na timu yake kwa namna ambavyo wanaendelea kufanya kazi nzuri ya utoaji huduma kwa wananchi, malalamiko mengi kuhusu shirika hilo katika wilaya hetu yameondoka, pale inapotokea changamoto wamekuwa wepesi sana kufika kwa wakati eneo la tukio,” amesema Msando.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kusini, Adam Abdullah, ameishukuru serikali kwa kuwapatia magari hayo, akisema yatawasaidia katika utekelezaji wa miradi yao na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora ya umeme kwa wananchi.
“Tutoe ahadi kwamba magari haya tutayatunza na kuhakikisha tunafikia malengo yetu hasa katika mkoa wetu wa Kinondoni Kusini,” amesema Abdullah.


