…….
Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga
Chakula, mavazi na malazi ni mahitaji muhimu ya binadamu (basic needs). Ni mahitaji ambayo maisha ya binadamu hayawezi kwenda bila kuwa nayo, ndiyo maana watu wanapambana kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi kama kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, ujasiriamali kuhakikisha mahitaji haya yanapatikana katika ngazi ya familia ili kufurahia maisha. Katika muktadha wa makala hii, msisitizo ni umuhimu wa chakula shuleni ili kuwafanya wanafunzi waweze kujifunza vizuri na kupata kile kilichoandaliwa na walimu wao hasa maarifa, ujuzi na stadi za maisha.
Wanafunzi wanaanza safari ya kwenda shule asubuhi sana. Wakifika shule hufanya usafi madarasani na katika mazingira mengine ya shule, ndipo ratiba ya vipindi madarasani huanza mnamo saa moja na nusu asubuhi. Husoma hadi saa tisa na nusu alasiri na wengine huendelea kwa ratiba nyingine za kujisomea.
Hivyo baadhi ya wanafunzi hao hujikuta wakitoka shule jioni. Baadhi yao kutokana na hali nzuri za kimaisha hunywa chai nyumbani au hupewa fedha ya ajili ya kula shuleni. Wengine wasio na uwezo hukosa chai nyumbani na hata shuleni, hivyo hushinda njaa huku wakikabiliwa na kazi ya kuelewa kile kinachofundishwa na walimu wao.
Ni ukweli usio na chembe ya shaka kuwa mwanafunzi mwenye njaa hawezi kuelewa anachofundishwa na walimu wake. Haelewi. Anaweza akaelewa masomo yaliyofundishwa vipindi vya asubuhi lakini ikishafika saa sita mchana na kuendelea, kasi ya uelewa hupungua kutokana na tumbo kudai chochote kitu (chakula). Mwanafunzi anaweza akalaumiwa kwa kutoelewa darasani lakini tatizo la msingi linaweza kuwa njaa.
Mathalani, mwalimu anafundisha mada ndogo ya Serikali za Mitaa (Local Government) katika somo la Uraia (Civics), lakini mwanafunzi anayefundishwa mada hiyo kama ana njaa hataelewa mada ya Serikali za Mitaa, yeye atawaza namna angepata chai na maandazi au na mihogo ili apoze njaa yake.
Binafsi, linapokuja suala la wanafunzi kula chakula shuleni, natamani kila mzazi na mlezi alichukulie kwa uzito wake badala ya baadhi yao kuwa kikwazo kwa kutotoa ushirikiano kwa walimu wanaoratibu suala hilo kwa mustakabali mwema wa wanafunzi ambao ni watoto wao.
Uongozi wa shule kwa kushirikiana na Kamati na Bodi za shule wakati mwingine wanashindwa kufanikisha suala la wanafunzi kula chakula shuleni kutokana na kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wazazi na walezi.
Serikali imechukua jukumu la kugharamia Sera ya Elimumsingi Bila Ada, jambo lililopunguza mzigo mkubwa kwa wazazi. Wazazi na walezi kwa upande wao wanalo jukumu la kugharamia chakula ambacho watakula watoto wao wenyewe ili kupata utulivu wakati wa ujifunzaji darasani.
Machi 12, 2026, Jijini Dodoma, kuliadhimishwa Siku ya Afrika ya Chakula Shuleni na Siku ya Kimataifa ya Chakula Shuleni ambapo kaulimbiu yake inasema “Chakula Bora, Maji Safi Shuleni: Ni Wajibu wa Pamoja.”
Kaulimbiu hii inatoa hamasa kwa wazazi na wadau kushirikiana kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula ili waweze kujifunza vyema na kutimiza malengo yao ya kielimu.
Wanafunzi wanapaswa kula chakula bora na kunywa maji safi shuleni. Hawapaswi kula chakula kwa lengo la kujaza tumbo na kutuliza njaa zao bali pia wajenge afya zao na kuchochea ujifunzaji kupitia chakula na maji.
Katika maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir alitoa rai kwa wadau kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja ili wanafunzi wale chakula shuleni kwani ni haki yao.
“Nawahimiza wazazi kushirikiana na shule kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya chakula wakiwa shuleni kama inavyoelekezwa katika Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016,” amesema Ameir.
Kimsingi, wanafunzi kula chakula shuleni kunaongeza ari ya wanafunzi kuhudhuria shule kwani pia wanapata uhakika wa kula na kuendelea kujifunza. Naamini hata baadhi ya wanafunzi wanaweza kuacha utoro pale watakapopata uhakika wa kula chakula pindi wawapo shuleni.
Ni vyema wazazi, walezi, jamii na wadau kwa ujumla kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha kila shule iwe ya Awali, Msingi au Sekondari, programu ya lishe shuleni iwepo na iwe endelevu yenye kutekelezwa kikamilifu ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza wakiwa na utulivu baada ya kupata chakula.
Serikali imebeba jukumu la kujenga shule, kuajiri walimu, kugharamia Sera ya Elimumsingi Bila Ada. Kwa upande wa wazazi, walezi na wadau tusimame kwa umoja kuhakikisha wanafunzi wanakula shuleni. Jamii tuone tukumu la wanafunzi kula shuleni ni letu sote badala ya kuiachia serikali pekee. Chakula shuleni si tu ni muhimu kwa afya za wanafunzi lakini pia ni miongoni mwa mkakati wa kukuza ufaulu mashuleni. Tafakari.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
Maoni : 0620 800 462.