Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga amewataka watumishi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Singida kutambua kuwa sekta ya barabara ni kiungo muhimu cha maendeleo ya sekta nyingine kama elimu, afya na uchumi, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa bidii na weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Ameyazungumza hayo leo 13 Machi 2026, katika kikao kazi cha TARURA kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Ukaguzi mkoa wa Singida ambapo Dkt. Mganga amesema TARURA ni taasisi mtambuka na inategemewa na sekta nyingi, hivyo utekelezaji mzuri wa majukumu yao ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.
Amesema moja ya changamoto kubwa inayowakabili wananchi ni uwepo wa barabara zisizopitika, hivyo watumishi wa TARURA wanapaswa kuhakikisha wanakuwa karibu na maeneo ya kazi hasa katika kipindi cha mvua ili kufuatilia hali ya barabara na kuhakikisha zinaendelea kupitika.
Pia, amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuwa na mawasiliano mazuri na kuwahudumia wananchi kwa heshima akisisitiza kuwa “mteja ni mfalme”.
Aidha, amewakumbusha watumishi kupambana na vitendo vya rushwa, kuheshimu muda wa kazi na kujaza taarifa katika mfumo wa PEPMIS ili kufikia malengo ya utendaji kazi.
Dkt. Mganga pia amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kutunza afya zao kwa kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi, akieleza kuwa serikali inawekeza rasilimali nyingi katika kuwajenga watumishi wake hivyo wanapaswa kulinda afya zao ili kuendelea kulitumikia taifa.
Awali, Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Claver Mwinuka, amesema kikao kazi hicho kinalenga kujadili mipango ya kazi, bajeti ya mwaka ujao wa fedha pamoja na mikakati mipya ya utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia maelekezo ya Bodi ya Barabara mkoa wa Singida.
Ameongeza kuwa kikao hicho pia kitatoa fursa ya kuimarisha mahusiano na mawasiliano kati ya watumishi, hususani wapya pamoja na kujadili matumizi ya teknolojia ya mawe katika ujenzi wa barabara ili kupunguza gharama na kuboresha ubora wa miundombinu.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wakiwemo Meneja wa TARURA Wilaya ya Iramba Mhandisi Evance Kibona na Meneja wa TARURA Wilaya ya Mkalama Mhandisi Rahabu Thomas, wamesema kikao hicho kitasaidia kuboresha utendaji kazi na kuongeza ubunifu katika ujenzi wa barabara, hususani kwa kutumia rasilimali za mawe zinazopatikana kwa wingi mkoani Singida ili kuongeza ubora wa barabara na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)