Lango la Mamire kuchochea utalii Tarangire

Tarangire. Kukamilika kwa ujenzi wa lango la Mamire la kuingilia katika Hifadhi ya Taifa Tarangire unatarajiwa kurahisisha watalii kuingia hifadhini kupitia Wilaya ya Babati, hatua inayolenga kupanua wigo wa ufikiwaji wa hifadhi hiyo na kuchochea utalii.

Akizungumza jana Alhamisi Machi 12, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava, amesema kufunguliwa kwa lango hilo kutasaidia watalii wanaotoka maeneo mbalimbali kufika hifadhini kwa urahisi zaidi.

Alieleza kuwa watalii wanaotoka mikoa ya  Dar es Salaam wanaweza kutumia reli ya kisasa ya SGR hadi Dodoma na kisha kuendelea na safari kwa gari hadi Tarangire kupitia Babati bila kulazimika kupitia Arusha kama ilivyokuwa awali.

“Tunaipongeza Serikali kwa uamuzi wa kufungua geti hili la Mamire kwa sababu litaboresha na kuongeza utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa kurahisisha watalii kuingia hifadhini. Tunaitaka Serikali ihakikishe hadi Aprili kama ilivyoahidi ujenzi uwe umekamilika na lianze kutumika,” amesema Mnzava

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, amesema Serikali  imejipanga kuhakikisha mradi  unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Amesema kukamilika kwa lango hilo kutapanua wigo wa kuingia katika hifadhi hiyo na kutoa fursa zaidi kwa watalii na wananchi wa maeneo ya jirani kunufaika na shughuli za utalii.

“Mradi huu tutahakikisha unakamilika kwa wakati na utakuwa na mafanikio makubwa kwa wananchi wa Babati na Tanzania kwa ujumla.”

Awali Meneja Mradi, Mhandisi Seleman Ntemi, alisema Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), ilitenga bajeti ya zaidi ya Sh3.921bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Alisema mradi huo ulioanza Machi 10,2023 unatarajiwa kukamilika Aprili 14,2026 ambapo mpaka sasa mradi umefikia asilimia 98.

Mhandisi huyo alisema mradi huo wa lango la kuingilia wageni umehusisha ujenzi wa jengo moja la lango vyoo vya wageni, nyumba za maofisa, nyumba za askari, ujenzi wa maegesho ya magari ambapo kwa upande wa kuingia eneo hilo linaweza kupokea magari 56 kwa wakati mmoja na eneo la kutoka lina uwezo wa kupokea magari 28 kwa wakati mmoja.

Nyingine ni uchimbaji wa kisima kirefu, uwekaji wa nishati ya umeme na samani za ofisi na maeneo ya kupumzikia wageni.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Chiku Issa, aliwataka wananchi wa Babati kutumia fursa ya uwepo wa lango hilo kuanzisha shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara za bidhaa za asili na uwekezaji katika huduma za malazi kwa watalii.

“Hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Babati. Tunapopata miundombinu kama hii, maana yake Serikali inatupa nafasi ya kuongeza vipato vyetu, nategemea wanawake wataleta bidhaa hapa na niwaombe wawekezaji pia waje kuongeza malazi kwani bado Tanzania tuna uhitaji wa malazi,” amesema

Diwani wa Kata ya Mamire, Agustino Susia, amesema wananchi wa eneo hilo wanatarajia kunufaika zaidi na mradi huo kupitia kuboreshwa kwa miundombinu ikiwemo ya barabara na kuongezeka kwa wageni watakaotembelea hifadhi hiyo.

“Lango hili limeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Mamire kwa sababu linatarajiwa kuongeza watalii na kukuza uchumi wa eneo letu.”