Maandalizi ya sikukuu yapamba moto, bei za bidhaa zachangamka

Dar/Mikoani. Zikiwa zimebaki siku kadhaa kabla za sikukuu ya Eid al-Fitr na Pasaka, hekaheka za maandalizi zimeanza kuonekana wazi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo soko maarufu la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambapo mamia ya watu wameanza kumiminika madukani kununua mahitaji ya sikukuu, hususan nguo na viatu kwa ajili ya watoto na familia zao.

Wazazi wengi wameonekana wakitembea na watoto wao wakichagua mavazi watakayovaa siku ya sikukuu huku wafanyabiashara wakijitahidi kuvutia wateja kwa kuonyesha bidhaa mpya na kutoa matangazo ya punguzo la bei.

Harakati hizo zinajitokeza wakati waumini wa Kiislamu wakijiandaa kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr inayotarajiwa kuwa kati ya Machi 20 na 21 kutegemea na mwandamo wa mwezi, mwaka huu huku Wakristo nao wakitarajia kusherehekea Pasaka ifikapo Aprili 5, 2026.

Katika mitaa maarufu ya biashara ikiwemo Aggrey, Congo na Msimbazi, maduka ya nguo na viatu yanaonekana kuwa na wateja wanaochagua bidhaa huku baadhi ya wazazi wakifika sokoni wakiwa na watoto wao ili wachague mavazi wanayoyapenda.

Wafanyabiashara wengi wameweka bidhaa mpya madukani wakiamini kuwa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ni miongoni mwa misimu yenye faida kubwa kwa biashara za mavazi na viatu.

Rehema Mussa, mkazi wa Ilala aliyekutwa katika moja ya maduka Kariakoo akimchagulia mtoto wake viatu, amesema huwa anapenda kwenda na watoto wake madukani ili kuchagua mavazi wanayoyapenda wenyewe.

“Watoto wakiona wenzao siku ya sikukuu, wanapenda kuvaa vizuri. Ndio maana nimemleta mwenyewe achague viatu na nguo. Lakini ukweli ni kwamba bei zimepanda kidogo ukilinganisha na mwaka jana,” amesema Rehema.

Amesema kwa kuwa ana watoto watatu, analazimika kupanga matumizi yake kwa makini ili aweze kununua mahitaji ya kila mtoto.

“Nina watoto watatu, hivyo lazima nipange vizuri matumizi. Kila mmoja anahitaji angalau nguo na viatu vipya kwa ajili ya sikukuu,” ameongeza.

Mzazi mwingine, Juma Abdallah amesema licha ya changamoto za kiuchumi, wazazi wengi hujitahidi kuhakikisha watoto wao wanafurahia siku ya sikukuu kwa kuvaa mavazi mapya kama ilivyo desturi katika familia nyingi.

“Unajua mtoto akiona wenzake wamevaa nguo mpya naye anataka. Hivyo hata kama hali ni ngumu lazima ujitahidi kumfurahisha mtoto,” amesema Juma.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi wanasema maandalizi ya sikukuu mwaka huu yanakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, hasa mavazi na viatu vya watoto.

Neema Joseph, mkazi wa Temeke, amesema bei za baadhi ya bidhaa zimeongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa miezi michache iliyopita.

“Nilinunua viatu vya mtoto wangu mwaka jana kwa Sh25,000 lakini hapa nimeambiwa vinauzwa hadi Sh35,000. Inabidi uzunguke maduka kadhaa ili upate bei nafuu,” amesema.

Kwa upande wa wafanyabiashara, baadhi yao wanasema ingawa wateja wameanza kuonekana madukani, bado kiwango cha ununuzi hakijafikia matarajio yao.

Mmiliki wa duka la nguo Kariakoo, Salum Said, amesema kwa sasa wateja wengi wanakuja kuangalia bidhaa na kuulizia bei lakini hawafanyi manunuzi makubwa.

“Wateja wanakuja wanaulizia bei na kuangalia bidhaa lakini mauzo si makubwa sana. Labda kadiri sikukuu zitakavyokaribia ndipo biashara itachangamka zaidi,” amesema.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara wengi wameagiza bidhaa mpya wakitarajia ongezeko la wateja kadiri siku zinavyosogea.

“Kipindi cha sikukuu huwa muhimu sana kwa wafanyabiashara wa nguo na viatu. Tunatarajia siku moja au mbili kabla ya sikukuu hali itakuwa nzuri zaidi,” amesema.

Mfanyabiashara mwingine, Asha Mwakalebela, amesema changamoto ya uchumi imepunguza uwezo wa baadhi ya wateja kufanya manunuzi makubwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

“Zamani kipindi kama hiki watu walikuwa wanachukua hata seti mbili au tatu za nguo. Lakini sasa wengi wanachukua moja tu au wanaishia kuulizia bei,” amesema.

Tofauti na hali hiyo kwa wafanyabiashara wa madukani, baadhi ya wamachinga wanaouza bidhaa pembezoni mwa barabara wanasema biashara zao zimeanza kuimarika kutokana na wateja kutafuta bidhaa za bei nafuu.

Mohamed Ali, ambaye huuza viatu vya watoto katika eneo la Kariakoo, amesema wateja wengi wanakimbilia kwao kwa sababu bei zao ni nafuu kuliko madukani.

“Watu wengi wanakuja kwetu kwa sababu bei zetu ni nafuu kuliko madukani. Unaweza kupata kiatu cha mtoto kwa Sh15,000 hadi Sh20,000,” amesema Ali.

Amesema katika siku za hivi karibuni ameanza kuona ongezeko la wateja, hasa wazazi wanaonunua bidhaa za watoto.

“Nina uhakika kadiri sikukuu zinavyokaribia wateja wataongezeka zaidi,” amesema.

Mbali na wafanyabiashara wa mavazi, pia, kuna wanaonufaika na ongezeko la watu wanaofika Kariakoo kufanya ununuzi.

Halima Bakari, mama lishe anayefanya biashara ya chakula karibu na soko hilo, amesema kipindi cha maandalizi ya sikukuu huongeza wateja katika biashara yake.

“Watu wengi wanaokuja kununua wanachoka wakizunguka maduka, hivyo wanakuja kula hapa. Kwa hiyo nasi tunafaidika na msimu huu,” amesema.

Wakati hali ya maandalizi ya sikukuu ikionekana kuanza kuchangamka jijini Dar es Salaam, baadhi ya wafanyabiashara katika maeneo mengine nchini wanasema hali ya biashara bado ni ngumu.

Katika Soko Kuu la Mwanza, baadhi ya wafanyabiashara wamelalamikia kupungua kwa wateja na ugumu wa kupata baadhi ya bidhaa.

Mfanyabiashara Adelina Alphonce amesema biashara kwa kipindi hiki si nzuri kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

“Si unaona tumekaa tu, hakuna wateja. Soko limelala, yaani halina biashara. Mfungo wa mwaka huu umekuwa tofauti sana na tulivyozoea,” amesema Adelina.

Naye, mfanyabiashara wa ndizi anayefahamika kwa jina la Mama Wawili amesema upatikanaji wa ndizi aina ya mzuzu umekuwa mgumu na bei yake imepanda.

“Ndizi mzuzu zimepanda sana, moja nauza Sh1,000 na mkungu unauzwa Sh30,000. Sasa nimeanza kuuza ndizi matoke kwa sababu ndizo zinazopatikana,” amesema.

Mfanyabiashara mwingine, Joseph Lyang’ombe amesema changamoto ya gharama za kodi na upangishaji wa vibanda imeendelea kuwa mzigo kwa wafanyabiashara wadogo.

“Biashara ni ya kawaida sana na faida haipatikani kama zamani. Kodi na gharama nyingine ni kubwa sana,” amesema Lyang’ombe.

Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara hao wameiomba Serikali kuangalia upya baadhi ya tozo na kodi ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi.

Wakati huohuo, katika Kisiwa cha Unguja, wafanyabiashara wamesema hali ya biashara inaendelea vizuri kuelekea sikukuu ya Eid al-Fitr.

Mfanyabiashara kutoka Soko Kuu la Mwanakwerekwe, Muslim Harith amesema bei za baadhi ya bidhaa muhimu bado ziko katika kiwango cha kawaida licha ya kuongezeka kwa mahitaji.

Amesema kilo moja ya siagi au samli inauzwa kati ya Sh6,500 na Sh7,000, huku bei ya mayai ikiwa kati ya Sh9,500 na Sh10,000 kwa trei.

Aidha, amesema nyanya zinauzwa kati ya Sh1,500 hadi Sh1,600 kwa kilo huku vitunguu vikiuzwa takribani Sh2,600 kwa kilo.

“Kawaida kadiri sikukuu zinavyokaribia mahitaji ya bidhaa huongezeka na wakati mwingine bei hupanda, lakini kwa sasa hali bado ni ya kawaida,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa muhimu unaimarika na bei kubaki katika viwango vinavyoweza kumudu na wananchi.