Arusha. Mahakama ya Rufani ya Tanzania imebatilisha hukumu ya kifo iliyokuwa imetolewa dhidi ya Richard Bahati, baada ya kubaini kasoro kubwa za kisheria katika mwenendo wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Mahakama imejiridhisha kuwa shahidi muhimu katika kesi hiyo, aliyekuwa mlalamikaji wa jaribio la mauaji, hakuelewa lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya Mahakama, huku rekodi za kesi zikishindwa kuonyesha kuwa mkalimani aliapishwa rasmi kutafsiri ushahidi wake.
Uamuzi huo ulitolewa Machi 9, 2026 na jopo la majaji watatu ambao ni Ferdinand Wambali, Omar Othman Makungu na Agnes Mgeyekwa.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Mgeyekwa alisema Mahakama imefuta hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga na kuamuru kesi hiyo isikilizwe upya, kutokana na kukiukwa kwa utaratibu muhimu wa kisheria kuhusu matumizi ya mkalimani wakati wa ushahidi.
Majaji walibainisha kuwa sheria inamtaka mtu yeyote asiyeelewa lugha ya mahakama apewe mkalimani ili aweze kuelewa kikamilifu mwenendo wa kesi.
Walisisitiza kuwa jukumu la kuhakikisha mkalimani yupo na ametekeleza taratibu zote za kisheria ni la mahakama, si la upande wa mashtaka wala mshtakiwa.
Kutokana na rekodi za kesi kuonyesha kuwa utaratibu huo haukufuatwa ipasavyo, Mahakama ilihitimisha kuwa ushahidi wa shahidi muhimu uliathiriwa na hivyo kuifanya kesi nzima kuwa na dosari.
Hata hivyo, licha ya kufuta hukumu ya kifo, Mahakama iliamuru kesi hiyo isikilizwe upya, ikieleza kuwa kasoro iliyobainika ilikuwa ya kiutaratibu na haimaanishi kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu kiasi cha kumuachia huru mshtakiwa.
Mahakama ilitumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa kufuta hukumu na kurejesha jalada la kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga ili kusikilizwa upya. Mrufani ataendelea kubaki kizuizini wakati kesi hiyo ikiendelea.
Katika kesi ya awali, Bahati alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kumuua Thomas Buluba, Machi 1, 2022 katika Kijiji cha Lutubiga, wilayani Busega mkoani Shinyanga.
Pia alishtakiwa kwa kosa la kujaribu kuua kinyume na kifungu cha 211(a) cha Kanuni ya Adhabu baada ya kudaiwa kujaribu kumuua msichana mmoja katika tukio hilohilo.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi wanne na kuwasilisha vielelezo viwili ikiwemo ripoti ya uchunguzi wa kifo na fomu ya kitabibu ya PF3.
Baada ya kusikiliza ushahidi na utetezi wa mshtakiwa, Mahakama Kuu ilimtia hatiani katika makosa yote mawili na kumhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa.
Katika rufaa yake, kupitia wakili wake, Bahati alipinga hukumu hiyo akidai kuwa kulikuwa na makosa ya kisheria katika mwenendo wa kesi, hasa kuhusu matumizi ya mkalimani kwa shahidi muhimu ambaye hakuelewa Kiswahili.
Upande wa Jamhuri pia ulikiri kuwepo kwa kasoro hiyo, ukieleza kuwa ingawa mkalimani aliwasilishwa mahakamani, rekodi za kesi hazikuonyesha wazi kuwa aliapishwa kutafsiri ushahidi kwa lugha zote zinazohitajika.
Kutokana na kasoro hiyo, Mahakama ya Rufani iliamua kufuta hukumu na kuamuru kesi hiyo kuanza kusikilizwa upya kwa mujibu wa sheria na taratibu.
