Tanga. Migogoro ya ardhi inayohusisha umiliki wa viwanja na urasimishaji wa makazi imekuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa Jiji la Tanga, wakilalamikia taratibu za utoaji wa hati na usimamizi wa ardhi unaofanywa na halmashauri.
Malalamiko hayo yameibuliwa katika Kliniki ya Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyoweka kambi ya siku saba mkoani Tanga, kufuatia ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba aliyebaini wingi wa migogoro ya ardhi katika mkoa huo. Baada ya ziara hiyo, aliziagiza Wizara ya Ardhi, Tamisemi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kushughulikia changamoto hizo na kutafuta suluhisho.
Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu katika Kliniki ya Sheria, Ipyana Mlilo amesema malalamiko mengi yanahusu umilikishwaji wa viwanja kuanzia upimaji, urasimishaji hadi utoaji wa hati za umiliki. Amesema migogoro mingi inaonekana kuhusisha mamlaka za ardhi, ikiwemo Wizara ya Ardhi kupitia Kamishna wa Ardhi na maofisa mipango miji, hali inayosababisha sintofahamu kati ya wananchi na Serikali.
Wakazi wa Tanga wakiwa wamejitokeza katika Kliniki ya Sheria inayoendelea jijini humo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu tayari imeanza utafiti kubaini namna bora ya kukabiliana na migogoro ya ardhi na kuchunguza iwapo kuna haja ya kufanya mabadiliko ya sheria. Hatua hiyo pia inatekelezwa kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu ya kushirikiana na Wizara ya Ardhi kutafuta suluhisho la kudumu.
Mlilo amesema hata katika kliniki za sheria zinazofanyika maeneo mbalimbali nchini, migogoro mingi inayowasilishwa na wananchi ni ya ardhi. Katika Tanga, malalamiko makubwa yanahusu urasimishaji wa makazi katika maeneo yenye wakazi ambao hayajapimwa.
Amesema katika mchakato huo kamati maalumu za mitaa hukusanya michango ya upimaji na kushirikiana na kampuni za upimaji chini ya usimamizi wa halmashauri. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanalalamika kulipia upimaji lakini kushindwa kupata hati, huku viwanja vikidaiwa kupewa watu wengine.
Mkazi wa Kwa Kayeza, kata ya Mabawa, Mkuka Langson amesema wakazi wa eneo hilo wameishi zaidi ya miaka 50 na walishalipia upimaji wa ardhi yao, lakini wanashangaa kuona imechukuliwa na kupewa watu wengine bila taarifa rasmi.
Amesema walipohoji, waliambiwa eneo hilo lilitwaliwa kwa ajili ya kuwahamishia watu walioathiriwa na mafuriko, jambo ambalo limezua sintofahamu kwani hawakupewa taarifa wala fidia.
Mawakili wa Serikali wakiwasikiliza wananchi waliofika katika Kliniki ya Sheria katika viwanja Tangamano, jijini Tanga.
Langson amesema walilazimika kufika katika Kliniki ya Sheria baada ya kukosa majibu ya kuridhisha kutoka halmashauri. Ameeleza kuwa wahusika tayari wametumiwa wito wa kufika Machi 13, 2026 kutoa maelezo kuhusu mgogoro huo.
Amesema wanataka kuona nyaraka rasmi zinazothibitisha utwaliwaji wa ardhi yao, na kama hazipo, hatua zichukuliwe ili wapate haki yao.
