Mara ngapi unavaa soksi bila kufua?

Dar es Salaam. Ni jambo la kawaida kuvaa jozi ileile ya suruali, sweta au hata fulana zaidi ya mara moja. Lakini vipi kuhusu soksi zako?

Kama ungejua ni nini hasa huishi kwenye soksi zako baada ya siku moja tu ya kuzivaa, huenda ungefikiria mara mbilimbili kabla ya kuzivaa tena.

Miguu yetu ni msitu mdogo wa vijidudu visivyoonekana kwa macho kama bakteria na fangasi, ambavyo kwa kawaida vinaweza kufikia hadi aina 1,000 tofauti. Miguu pia ina aina nyingi zaidi za fangasi kuliko sehemu nyingine yoyote ya mwili wa binadamu.

Ngozi ya mguu pia ina idadi kubwa sana ya tezi za jasho kuliko sehemu nyingi za mwili.

Bakteria na fangasi wengi wa miguuni hupendelea kuishi katika maeneo yenye joto na unyevunyevu kati ya vidole vya miguu, ambako hula virutubisho vilivyomo kwenye jasho na seli zilizokufa za ngozi. Taka zinazozalishwa na vijidudu hivi ndizo husababisha miguu, soksi na viatu kunuka.

Kwa mfano, bakteria aina ya Staphylococcus hominis huzalisha aina ya pombe kutokana na jasho inalokula, ambayo hutoa harufu ya vitunguu vilivyooza. Bakteria Staphylococcus epidermis huzalisha kemikali yenye harufu ya jibini.

Corynebacterium, kwa upande wake, huzalisha tindikali inayofafanuliwa kuwa na harufu ya mbuzi. Kadiri miguu inavyotoa jasho zaidi, ndivyo virutubisho vinavyopatikana kwa bakteria hao na harufu huwa kali zaidi.

Kwa kuwa soksi zinaweza kunasa jasho, hutengeneza mazingira bora zaidi kwa bakteria wanaozalisha harufu. Zaidi ya hayo, bakteria hawa wanaweza kuishi kwenye vitambaa kwa miezi kadhaa. Kwa mfano, bakteria wanaweza kuishi kwenye kitambaa cha pamba hadi siku 90. Hivyo, ukivaa tena soksi ambazo hazijaoshwa, unaruhusu bakteria zaidi kukua na kustawi.

Aina za vijidudu vinavyopatikana kwenye soksi zako si vile tu vinavyoishi kawaida kwenye miguu. Pia vinajumuisha vijidudu kutoka mazingira yanayokuzunguka kama sakafu ya nyumbani au hata ardhi ya nje.

Katika utafiti uliochunguza vijidudu vilivyomo kwenye nguo zilizovaliwa mara moja tu, soksi zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya vijidudu ikilinganishwa na aina nyingine za nguo. Soksi zilikuwa na kati ya bakteria milioni 8–9 kwa kila sampuli, ilhali fulana zilikuwa na takribani bakteria 83,000 tu kwa sampuli.

Uchambuzi wa aina za vijidudu kwenye soksi unaonyesha kuwa zinahifadhi bakteria wasio na madhara wa ngozi, pamoja na vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa kama Aspergillus, Candida na Cryptococcus, ambavyo vinaweza kusababisha maambukizi ya mfumo wa upumuaji na tumbo.

Vijidudu vinavyoishi kwenye soksi zako vinaweza pia kuhamia maeneo mengine kama viatu vyako, kitanda, sofa au sakafu.

Hii ina maana kuwa soksi chafu zinaweza kusambaza fangasi wanaosababisha fangasi wa miguuni, maambukizi  yanayoathiri ngozi ya vidole vya miguu na maeneo yanayozunguka.

Ndiyo maana ni muhimu sana kwa watu wenye fangasi wa miguuni kutoshirikiana soksi au viatu na wengine, na kuepuka kutembea wakiwa wamevaa soksi tu au pekupeku katika vyumba vya kubadilishia nguo au vyooni.

Kile kinachoishi kwenye soksi zako pia hukaa kwenye viatu vyako. Ndiyo sababu huenda usingependa kuvaa jozi ileile ya viatu kwa siku nyingi mfululizo, ili jasho lipate muda wa kukauka kabisa na kuzuia ukuaji zaidi wa bakteria na harufu.

Ili kupunguza harufu ya miguu na kupunguza idadi ya bakteria wanaokua kwenye miguu yako na ndani ya soksi, ni vyema kuepuka kuvaa soksi au viatu vinavyosababisha miguu kutokwa na jasho sana.

Kuosha miguu mara mbili kwa siku kunaweza kusaidia kupunguza harufu kwa kuzuia ukuaji wa bakteria. Vizuia-jasho vya miguu  pia vinaweza kusaidia, kwa kuwa hupunguza jasho na hivyo kuzuia ukuaji wa bakteria.

Pia inawezekana kununua soksi zenye uwezo wa kuua bakteria moja kwa moja. Soksi hizo za aina mbalimba zinaweza kuua bakteria wanaosababisha harufu ya miguu.

Kwa hiyo, soksi za kuua vijidudu zinaweza zisihitaji kuvaliwa mara moja tu, kutegemea uwezo wake wa kuua bakteria na fangasi na kuzuia mkusanyiko wa jasho.

Lakini kwa wale wanaovaa soksi zilizotengenezwa kwa pamba, sufu au nyuzi, ni bora kuzivaa mara moja tu ili kuzuia harufu ya miguu na kuepuka maambukizi ya miguuni.

Pia ni muhimu kuhakikisha unaosha soksi zako vizuri katikati ya matumizi. Kama miguu yako hainuki kupita kiasi, ni sawa kuziosha kwa maji ya uvuguvugu yenye joto la kati ya 30–40°C kwa kutumia sabuni laini.

Hata hivyo, si bakteria na fangasi wote watakaoangamizwa kwa njia hii. Kwa hiyo, ili kusafisha soksi kikamilifu, tumia sabuni yenye vimeng’enya (enzymes) na osha kwa joto la 60°C. Vimeng’enya husaidia kuondoa vijidudu kutoka kwenye soksi huku joto la juu likiviua.

Kama kuosha kwa joto la chini hakuepukiki, kupiga pasi soksi kwa pasi ya mvuke yenye joto kali (inayoweza kufikia 180–220°C) kunatosha kabisa kuua bakteria waliobaki na kuzima mbegu za fangasi.

Kukausha soksi nje juani pia ni wazo zuri, kwani mionzi aina ya UV kutoka kwenye mwanga wa jua,  ina uwezo wa kuua bakteria na fangasi wengi wanaopatikana kwenye soksi.

Ushauri wa kitaalamu: Badilisha soksi zako kila siku ili miguu ibaki safi na yenye harufu nzuri.