PIGO kubwa ililopata Yanga pale kwenye safu ya ulinzi kutokana na beki na nahodha msaidizi, Dickson Job kuumia, limeendelea kuwa gumzo na kuibua wasiwasi, sio ndani ya timu pekee, bali hata kwa mashabiki wakijiuliza sasa itakuwaje bila uwepo wake.
Job ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti huku taarifa zikibainisha kwamba hadi kufikia Juni 2026 anaweza kurudi rasmi uwanjani kuendelea kucheza, wakati ambao pengine msimu huu ukawa umeshamalizika kwani mechi za mwisho za ligi zimepangwa kuchezwa Juni 18.
Wakati wasiwasi huo ukiwa mkubwa, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amekuja na akili mpya kuhakikisha pale nyuma hakuna kinachoharibika.
Hata hivyo, Pedro amesema: “Tunakwenda kumkosa mchezaji muhimu kwa muda mrefu, tuna kazi kubwa ya kuziba pengo hilo.”
Job ambaye alianza kuitumikia Yanga tangu mwaka 2021, mpaka sasa amekuwa mmoja wa mabeki muhimu kwenye safu ya ulinzi ya klabu hiyo, lakini pia ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao hawana kabisa rekodi ya majeraha ya mara kwa mara na kukaa nje muda mrefu tofauti na sasa ilivyotokea.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema kumkosa beki huyo si suala jepesi kwake na timu kwa ujumla, kwani alikuwa mlinzi bora na imara wakati wote, jambo lililoifanya Yanga kuwa na rekodi nzuri ya ulinzi.
Alisema kumkosa mpaka mwisho wa msimu ni pigo, lakini anashukuru kwa sababu Yanga ina kikosi kipana ambacho kinaweza kubadilika kutokana na mazingira na mechi husika.
“Kumkosa Job ni pigo kubwa kwetu kutokana na utumishi wake, lakini tunamuombea apone haraka, lakini hakuna presha kubwa kwani kuna mabeki watatu wengine, naamini pia watafanya kazi yao ipasavyo na kuwapa furaha mashabiki wa Yanga.”
Alisema kwa sasa wanalazimika kuanza mikakati ya kutengeneza pacha nyingine eneo hilo, ambalo litakwenda kuwa na kiwango kile kile.
“Kuna Mwamnyeto (Bakari), Bacca (Ibrahim) na Assinki (Frank), wote ni mabeki wazuri ambao wanaweza kuisaidia timu kwa ujumla, lakini kazi kubwa niliyonayo ni kuhakikisha wanakuwa na muunganiko mzuri ili kusiwepo na pengo lolote,” alifichua Pedro.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwa Job kuukosa msimu huu endapo Ligi Kuu Bara itamalizika Juni 18, 2026 kama ambavyo ratiba ya sasa inaonyesha, itakuwa ni pigo kwa Yanga kumkosa mlinzi huyo tegemeo.
Ndani ya kikosi cha Yanga, kabla ya Job kuumia, Pedro amekuwa akimtumia sana sambamba na Ibrahim Bacca kucheza pacha beki wa kati, huku nahodha, Bakari Mwamnyeto na Frank Assinki wakipata muda mchache. Mbali na hao, Aboubakar Nizar ‘Ninju’ naye mara moja moja amepata nafasi akicheza eneo hilo.
Kabla ya Job kuumia wakati wa mechi ya Kariakoo Dabi dhidi ya Simba iliyochezwa Machi Mosi 2026, Yanga ilikuwa imeruhusu mabao mawili pekee ikishuka dimbani mara 12 katika Ligi Kuu Bara, ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi.
Kwa sasa Yanga inakabiliwa na mechi ngumu ya dabi dhidi ya Azam itakayochezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:30 usiku ikiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara. Hiyo ni baada ya jana Alhamisi kumalizana na Tanzania Prisons ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Tangu kuumia kwa Job, Mwamnyeto ameonekana kupewa nafasi kubwa ya kucheza sambamba na Bacca kwani hilo lilijidhihirisha siku ya Kariakoo Dabi kwani alipofanyiwa mabadiliko, aliingia nahodha huyo.
