Sh14.9 bilioni kujenge madaraja mawili Ileje

Ileje. Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi kutoka kampuni ya Jasco anayejenga daraja la Kabalisi na mkandarasi kutoka kampuni ya Gemen anayejenga daraja la Sange kukamilisha miradi hiyo kufikia Machi 30, 2026.

Ujenzi wa madaraja hayo yanatarajia kugharimu jumla ya Sh14.9 bilioni  ambapo inadaiwa pindi yakikamilika yataondoa adha kwa wananchi ya kuvuka kwenda upande wa pili hasa kipindi cha mvua.

Kasekenya ambaye pia ni Mbunge wa Ileje ametoa maelekezo hayo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa madaraja hayo likiwepo la mto Kabhalisi lenye urefu wa mita 40 litagharimu Sh7.9 bilioni ambapo litawasaidia na kuwarahisishia kuvuka kwenda wilayani Rungwe kwa ajili ya shughuli za biashara.

Amesema pia ujenzi wa daraja la Sangwe litakalojengwa kwa Sh7 bilioni likiwa na urefu wa mita 40 hivyo ujenzi huo kuendana na uwekaji wa taa katika madaraja hayo na kuhakikisha mitaro karibu na madaraja hayo inasakafiwa vizuri.

“Hakikisheni ujenzi wa madaraja haya unakidhi ubora uliosanifiwa ili kuwiana na barabara za lami zitakapojengwa”, amesema Kasekenya.

Msimamizi wa ujenzi huo, Jonas Matete kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Barabara cha Tanroads (Tecu), amesema atawasimamia makandarasi hao ili madaraja hayo yaliyojengwa sehemu zenye miinuko yakamilike kwa wakati na ubora ili kuchochea fursa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Madaraja ya Kabalisi na Sange yapo katika barabara itokayo Ibungu- Kalembo-Kafwafwa hadi Kimo yenye urefu wa kilomita 46.1 na inaunganisha Wilaya ya Ileje mkoani Songwe na Rungwe mkoani Mbeya.

Zaidi ya Sh7.9 bilioni zimetumika katika ujenzi wa daraja la Kabalisi wakati Sh7 bilioni zikitumika kujenga daraja la Sange.

Joseph Mwashiuya mkazi wa Ileje amesema kabla ya kuanza ujenzi wa madaraja hayo walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuwasiliana na wananchi wa Wilaya ya Rungwe kutokana na mito hiyo kujaa maji.

Naibu waziri wa ujenzi mhandisi Godfrey Kasekenya Msongwe akiwa kwenye ukaguzi wa madaraja kwenye mto Sange na Kabhalisi yanayojengwa kwa gharama ya Sh14.9bilioni

Anita Mwasenga amesema kinamama ambao wanategemea soko la Kiwira na Mbeya  kwa ajili ya kuuza ndizi walikuwa wanapata shida  ya magari kukwama hasa kipindi cha masika, hivyo kukamilika kwa madaraja hayo ni mkombozi.