Mbeya. Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imewataka wavuvi mwambao mwa Ziwa Nyasa kuchukua tahadhari kufuatia kuwepo kwa vipindi vya radi na upepo mkali wenye uwezo wa kusababisha ajali au kupinduka vyombo vya uvuvi majini.
Mbali na wavuvi pia imewataka wananchi waishio mabondeni kuchukua tahadhari kubwa kufuatia udongo kufyonza maji mengi na kuweza kusababisha mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Wakati TMA ,ikitoa tahadhari hiyo, bei ya dagaa imetajwa kupaa kutoka Sh20,000 hadi Sh50,000 kwa ndoo.
Meneja wa TMA Kanda, Elius Lipiki ametoa tahadhari hiyo leo Ijumaa Machi 13, 2026 ili wananchi waweze kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
“Utabiri unaonyesha kutakuwa na mvua kubwa mwishoni mwa wiki hususani Jumapili na zitapungua Jumatatu Machi 16, lakini tunasisitiza waishio mabondeni na wavuvi kuchukua tahadhari,” amesema.
Lipiki ametaja miongoni mwa sababu za kutoa tahadhari kwa wavuvi ni kutokana na ziwa kuchafuka kufuatia mvua zinazoendelea hususani kuwepo kwa radi na upepo mkali ambao utaweza kusababisha ajali na kupinduka vyombo vya uvuvi majini.
“Licha ya changamoto ya mvua na upepo mkali, pia kuna tatizo la mito kuingiza maji yenye tope ziwani, jambo ambalo limesababisha maji kuchafuka na kuathiri shughuli za uvuvi na upatikanaji wa samaki,” amesema.
Katika hatua nyingine, ameonya baadhi ya wazazi kutoruhusu watoto kuvuka katika maeneo yasiyo rafiki, hususan vijito, mifereji na mito mikubwa, kwani hali hiyo inaweza kuhatarisha usalama wao.
“Kipindi hiki cha mvua za mwishoni tunatoa wito kwa wazazi kupunguza majukumu kwa watoto na kuhakikisha wanapelekwa mashuleni au wanavushwa katika maeneo hatarishi,” amesema.
Wakati huohuo, amewataka wakulima kutumia fursa ya kipindi hiki cha mvua kuhudumia mazao yao, akieleza kuwa hali ya hewa iliyopo ni rafiki kwa uzalishaji.
Hata hivyo, ametaja sekta ya ujenzi kuwa miongoni mwa zilizoathirika, baada ya baadhi ya miradi kukwama kutokana na mvua.
Mvuvi wa eneo la Matema, wilayani Kyela, Festo Wille amesema hali ya uvuvi ziwani kwa sasa ni mbaya kutokana na maji kuchafuka kiasi cha kufanya ziwa liwe vigumu kuingilika. Hali hiyo imesababisha samaki na dagaa kupungua au kutopatikana kabisa.
“Kwa sasa hali ni mbaya, samaki hawapatikani kabisa kutokana na uchafu wa maji, jambo ambalo limesababisha pia mfumuko wa bei,” amesema.
Ameongeza kuwa bei ya dagaa kwa plastiki la kilo 20 imepanda kutoka Sh20,000 hadi Sh50,000, huku upatikanaji wake ukiendelea kuwa mgumu.
“Wavuvi wenye vyombo vya kisasa ndio wanafanikiwa kupata vitoweo hivyo, tofauti na sisi tunaotumia mitumbwi. Kwa sasa hali zetu kiuchumi ni ngumu,” amesema.