Upendo aliyeachwa na mtoto wa siku tisa, sasa anamiliki nyumba za kupangisha

Iringa. Katika Kijiji cha Ibangamoyo, Kata ya Ulanda, Tarafa ya Kalenga mkoani Iringa, anaishi Upendo Nyanginywa, mama wa watoto watatu.

Hadithi ya Upendo inaanza katika kipindi kigumu cha maisha yake, baada ya kuingia  katika ndoa.

Upendo anasema mambo yalibadilika ghafla, akajikuta akiachwa na mwenza wake wakati tayari alikuwa na mtoto mchanga wa siku tisa tu.

Katika hali hiyo, alilazimika kuondoka kwenye ndoa yake akiwa amembeba mtoto huyo mikononi.

Ni tukio ambalo lingeweza kumvunja moyo mwanamke yeyote lakini kwa Upendo, huo ndio ukawa mwanzo wa safari ndefu ya kujitafuta na kujenga maisha mapya kwa ajili yake na watoto wake.

Akikumbuka siku hizo, Upendo anaisimulia Mwananchi kwa sauti ya utulivu lakini yenye hisia nzito.

Anasema baada ya kuachana na mwenza wake, alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi akiwa hana mahali pengine pa kwenda wala msaada wa kifedha.

Anasema alitarajia kupokewa kwa faraja na msaada wa familia, lakini mambo hayakuwa rahisi kama alivyotarajia.

Mama yake hakumkubali mara moja. Hali hiyo ilimuacha Upendo katika maumivu ya moyo huku akijiuliza mustakabali wake na wa watoto wake, hasa yule mchanga aliyekuwa bado anahitaji uangalizi wa karibu.

Katika hali hiyo ya kukata tamaa, anasema alijaribu kutafuta msaada kwa watu waliokuwa karibu naye kijijini hapo.

Hatimaye Upendo anasema alienda kwa mwenyekiti wa kijiji na kumweleza hali yake. “Mwenyekiti alizungumza na mama akamshauri anipokee na watoto wangu kusudi nianze upya maisha,” anasimulia mama huyo.

Anasema baada ya mazungumzo, mama yake alipokea ushauri na akamruhu arejee nyumbani hapo na wanaye, ndipo safari yake ya kuanza maisha upya ikaanza rasmi.

Baada ya muda mfupi, Upendo anasema alianza kufikiria namna ya kujitegemea ili aweze kuwalea watoto wake bila kumtegemea mtu yeyote. Wakati huo hakuwa na mali nyingi. Kilichokuwapo mikononi mwake kilikuwa ni nguruwe mmoja tu.

Alifanya uamuzi mgumu wa kumuuza nguruwe huyo kwa Sh70,000. Ingawa kiasi hicho kilionekana kidogo, kwake kilikuwa mtaji muhimu wa kuanza maisha mapya ya kujitegemea.

Kwa kutumia fedha hizo, Upendo anasema aliwasiliana na kijana aitwaye Mengi Tagalile kutoka Mtera ambaye alimletea samaki kwa ajili ya biashara. Hapo ndipo safari yake ya ujasiriamali ilipoanza rasmi.

Katika hatua za mwanzo, Upendo anasema alipata msaada mkubwa kutoka kwa shangazi yake, Togela Kalenga ambaye alimshauri kuhusu mbinu za biashara na hata kumtafutia sehemu ya kuuzia samaki.

Kwa mshangao wake, biashara hiyo ilianza kumlipa kwa haraka. Ndani ya siku tatu tu tangu aanze kuuza samaki, tayari alikuwa ameanza kuona faida. Hilo lilimpa moyo wa kuendelea.

Anasema aliongeza mtaji wake na kuagiza samaki wa Sh100,000 na baadaye akapandisha hadi Sh150,000. Biashara ikaendelea kukua polepole kadri wateja walivyoongezeka.

Baadhi ya wateja wake walianza kumwomba kitu zaidi ya samaki wabichi. Walimwambia wangependa apike samaki pamoja na ugali ili waweze kula hapo hapo. Hapo ndipo Upendo alipotambua fursa nyingine ya biashara.

Alianza biashara ya chakula maarufu mama lishe lakini alikuwa akiuza ugali kwa samaki tu na baada ya muda mfupi, biashara yake ikageuka na kuwa mgahawa mdogo uliowavutia wateja wengi.

Hata hivyo, mafanikio hayo hayakudumu kwa muda mrefu katika eneo lile. Baada ya mwenye eneo kumtaka aondoke. Ingawa uamuzi huo ulimuumiza kwa sababu alikuwa ameanza kuongeza wateja, lakini hakukata tamaa. Anasema alitafuta eneo lingine na akaendelea kwa juhudi zilezile na kasi kubwa zaidi.

Anasema baadaye alipata sehemu karibu na nyumba inayohusishwa na Chifu Mkwawa, alikohamishia biashara yake.

Upendo anasema wakati huo hakuwa na vifaa vya kisasa. Usiku alitumia kibatali kwa ajili ya mwanga na wateja walikaa kwenye viti vya kawaida.

Licha ya mazingira hayo ya kawaida, anasema bidii yake iliwafanya wateja kuendelea kuja kwa wingi.

Kadri muda ulivyopita na biashara kuimarika, Upendo anasema alianza kuboresha mazingira. Alinunua viti vya plastiki, vyombo vya kuhifadhi chakula na hata makapeti ili kuweka mazingira bora ya eneo lake la biashara.

Mapato aliyokuwa akipata hayakuishia kwenye biashara pekee, anasema  alitumia pia fedha hizo kuhakikisha watoto wake wanaendelea na masomo bila kukosa mahitaji muhimu, kwa sababu aliamini elimu ndiyo msingi wa maisha yao ya baadaye.

Baadaye alinunua kiwanja eneo la Kalenga na kujenga nyumba ya tope. Nje ya nyumba hiyo alijenga kibanda kidogo cha biashara huku akiendelea kuweka akiba.

Alipoulizwa kwa nini anaweka akiba hapo, alikuwa akijibu kwa utani kwamba anaweka kwa ajili ya mbolea, lakini moyoni mwake alikuwa anajiandaa kutimiza ndoto kubwa zaidi.

Baada ya muda, akiba hiyo anasema ilimsaidia kununua mabati na kujenga nyumba nyingine yenye vyumba vitatu. Upendo anasema hatua hiyo ilikuwa ishara kwamba juhudi zake zilianza kuzaa matunda.

Katika kupanua vyanzo vya kipato, Upendo aliingia pia katika ufugaji wa ng’ombe: “Nilinunua ng’ombe jike na dume nikaenda kuwawekeza kwa mtu mwingine ili wazaliane,” anasema.

Hata hivyo, anasema baadaye aligundua kuwa uwekezaji huo ulikuwa na changamoto nyingi na haukuwa na faida aliyotarajia.

Hivyo, anasema aliamua kuwauza ng’ombe hao na kuhamishia mtaji wake kwenye biashara ya mahindi.

“Biashara hii ilinipa faida nzuri nikapata hela za kununua nyumba ya vyumba sita iliyokuwa inauzwa hapa kijijini,” anasema Upendo.

Anasema haikuwa imekamilika vizuri, hivyo aliwaomba wapangaji walitaka kupanga washirikiane naye kukamilisha matengenezo.

“Niliwaambia kama watachangia kidogo kwa ajili ya ukarabati, fedha hiyo itakatwa baadaye kwenye kodi yao. Walikubali,” anasimulia mama huyo.

Anasema wapangaji wake wengi walikuwa wakulima na vibarua waliokuwa wanalima  kwenye mashamba ya mahindi na nyanya yaliyoko kwenye Bonde la Kalenga.

Anasema nyumba hiyo imeendelea kumuingizia kipato cha kutosha, hali inayomfanya aendelee kuishi maisha ya amani bila kumtegemea mtu, bali baadhi ya ndugu ndiyo wanamtegemea yeye.

“Nasomesha watoto wangu kwa kuwalipia ada mwenyewe, simsumbui mtu, uvumilivu unalipa hasa ukiongeza na juhudi na ubunifu, nimetoboa,” anasema Upendo.

Anasema kwa sasa anapogeuka nyuma na kutazama safari aliyopitia, anaona umbali mkubwa alioutembea, kutoka katika maumivu ya kuachwa akiwa na mtoto wa siku tisa hadi kuwa mwanamke mwenye nyumba, biashara na wapangaji.

Anaamini siri ya mafanikio yake ni kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa.

“Kwa wanawake wenzangu tunapaswa kuelewa kwamba mwanamke hapaswi kukimbia watoto wake hata kama una maisha magumu kiasi gani, wakumbatie na Mungu atakukumbatia na kukuonyesha njia ya kutokea,” anasema Upendo kwa ujasiri mkubwa.

“Baba anaweza kuondoka, lakini mama ndiye mlezi wa kweli,” anasema.

Pia, anawashauri wanawake kuacha makundi yanayopoteza muda badala yake wajikite katika kazi na kujitafutia maendeleo.

Kwa mtazamo wake, anasema mkopo mkubwa ambao mwanamke anaweza kuwa nao si lazima utoke benki au taasisi za fedha, “mkopo wako mkubwa unaweza kuwa juhudi zako mwenyewe. Ukifanya kazi kwa bidii, maisha yanaweza kubadilika.”