Wataalamu wa maabara wajengewa uwezo kukabili kipindupindu

Dar es Salaam. Serikali kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii imejipanga kuimarisha ufuatiliaji na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya nchini ili kuboresha utambuzi wa haraka wa kipindupindu, hatua itakayosaidia kudhibiti ugonjwa huo kabla haujasambaa.

Hayo yamebainishwa Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa maabara hiyo, Ambele Mwafulango, wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa wataalamu wa maabara kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara. Mafunzo hayo yamelenga kutambua mapema ugonjwa wa kipindupindu, kufuatilia wagonjwa kwa karibu na kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga na magonjwa ya mlipuko.

Mwafulango amesema kuwa tamko lililotolewa Februari 25, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, lilikuwa na habari njema kuhusu kumalizika kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini, huku takriban mwezi mmoja uliopita hakuna mgonjwa aliyejitokeza. Hata hivyo, amesema mvua zinazoendelea zinaongeza hatari ya mlipuko, hivyo tahadhari zinahitajika.

“Mvua huleta changamoto mbalimbali ikiwamo kipindupindu. Tahadhari lazima zichukuliwe,” amesema. Pia amesisitiza wataalamu kutumia ujuzi waliopata kikamilifu na kuufikisha kwa wenzao ili kueneza maarifa zaidi. Pia aliwatahadharisha wananchi kuendelea kuepuka uchafuzi wa mazingira, kutumia maji safi na salama, na kuosha mikono ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko.

Mratibu wa mafunzo na mtaalamu wa afya wa maabara hiyo, Emmanuel Magembe, amesema mafunzo yamejumuisha wataalamu kutoka hospitali za mikoa yote, na kipaumbele kilitolewa kwa mikoa yenye hatari ya mlipuko mara kwa mara na mikoa jirani na mipaka ya nchi. Mpango unaoendelea ni kuwafikia wataalamu wa maabara kutoka hospitali za wilaya na zahanati ili kuongeza ufanisi wa kudhibiti kipindupindu.

Mtaalamu Anifa Rwebangila aliyehudhuria mafunzo amesema uharakishaji wa mafunzo ngazi ya hospitali za wilaya na zahanati utaongeza ufanisi wa kudhibiti mlipuko. “Tukitumia maarifa tuliyopata, tutasaidia wananchi kujikinga na kubaini mapema maambukizi ili hatua zichukuliwe haraka,” amesema.