Mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel yameendelea kuilenga Tehran, mji mkuu wa Iran ikiwa ni siku ya 14 tangu vita hivyo vilipoanza Februari 28, 2026. Mashambulizi hayo, pia, yameilenga miji ya Kashan, Isfahan, Qom na Arak nchini humo.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetoa taarifa kuhusu mashambulizi yake ya kulipiza kisasi, likisema kuwa yalikuwa ni wimbi la 44 la mashambulizi yake yanayoilenga Israel.
Kwa ujumla, hali inazidi kuwa mbaya. Zaidi ya watu 1,400 wamepoteza maisha nchini humo huku jumla ya vifo vilivyotokea Mashariki ya Kati nzima katika mapigano hayo vikiwa zaidi ya watu 2,000. Maeneo mengi ya makazi yamelengwa katika mashambulizi hayo.
Aidha, kuna uchafuzi wa hewa unaotokana na maghala ya mafuta yanayoteketea kwa moto. Sehemu kubwa ya wakazi wa Tehran wameanza kuhama na kuondoka katika jiji hilo kutokana na hali tete inayoendelea.
Wakati Iran ikishambuliwa, nayo imeendelea kulipiza kisasi kwa kuishambulia Israel na ngome za kijeshi za Marekani zilizopo katika ukanda wa Mashariki ya Kati, hali inayofanya vita hiyo kuendelea kwa muda zaidi.
Bei ya mafuta duniani imeendelea kupaa hasa baada ya kukosekana kwa uhakika wa kumalizika kwa vita hivyo huku Marekani na Iran, kila moja ikijigamba kwamba ndiyo ina uamuzi wa mwisho wa kumaliza vita.
Kwa mujibu wa Reuters, Iran imesema itaendelea kupigana na itaendelea kuufunga Mlango Bahari wa Hormuz kama njia ya kuishinikiza Marekani na Israel, kiongozi mpya wa juu wa nchi hiyo, Mojtaba Khamenei alisema Alhamisi Machi 12, 2026 katika hotuba yake ya kwanza tangu alipomrithi baba yake aliyeuawa.
Saa chache baadaye, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitumia mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu kuanza kwa vita hivyo kutoa kauli kali, akitoa kitisho kisicho cha moja kwa moja cha kumuua Khamenei huku akitetea mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuyumba kwa masoko ya nishati na hisa.
“Sitochukua jukumu la kutoa bima ya maisha kwa yeyote kati ya viongozi wa shirika la kigaidi… sina nia ya kutoa ujumbe wa moja kwa moja hapa kuhusu tunachopanga au tutakachofanya,” alisema Netanyahu, akiwa amesimama kati ya bendera mbili za Israel na kujibu maswali kupitia mawasiliano ya video.
Nchini Iran, Khamenei hakuonekana hadharani na hotuba yake ilisomwa na mtangazaji wa televisheni ya taifa. Hakuna picha yake iliyotolewa tangu shambulizi la Israel mwanzoni mwa vita hivyo, lililoua sehemu kubwa ya familia yake, akiwemo baba yake na mke wake.
Kauli ya Khamenei ilizitaka nchi jirani za Iran kufunga vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko katika maeneo yao na kuonya kwamba Iran itaendelea kuvishambulia.
“Nawahakikishia wote kwamba hatutapuuza kulipiza kisasi kwa damu ya mashahidi wenu,” alisema mwanazuoni huyo mwenye msimamo mkali wa kidini, ambaye ana uhusiano wa karibu na vikosi vya juu vya kijeshi vya Iran.
“Matakwa ya wananchi ni kuendelea na ulinzi wetu madhubuti na kumfanya adui ajute. Njia ya kuzuia Mlango Bahari wa Hormuz lazima iendelee kutumika,” aliongeza Khamenei, akimaanisha njia hiyo ya usafiri wa meli ambapo kwa kawaida karibu theluthi moja ya mafuta ya dunia hupitia kando ya pwani ya Iran.
Televisheni ya taifa ya Iran haikutoa maelezo kwa nini ujumbe huo ulisomwa na mtangazaji badala ya kutolewa na kiongozi mwenyewe. Maofisa wa Iran wamesema Khamenei alijeruhiwa kidogo katika mashambulizi ya anga ya Februari 28, lakini kiwango halisi cha majeraha yake hakijulikani.
Hofu ya uwezekano wa usumbufu katika usambazaji wa nishati duniani, ilisababisha bei ya mafuta kupanda kwa takriban asilimia tisa hadi kufikia dola 100 kwa pipa, baada ya kushuka mapema katika wiki hiyo kutokana na matumaini ya kumalizika haraka kwa mzozo huo.
Wakati mashambulizi ya Marekani na Israel yakiendelea huko Iran, inaonekana kuna mkakati wa kijeshi wa Israel wa kuongeza shinikizo kubwa nchini Lebanon, si tu dhidi ya Hezbollah bali pia dhidi ya serikali ya nchi hiyo.
Katika saa 24 zilizopita, maofisa wa Israel wametoa kauli kali dhidi ya Serikali ya Lebanon. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema kwamba ikiwa Serikali ya Lebanon haitakabiliana na Hezbollah na kusitisha mashambulizi yake, basi Israel itadhibiti sehemu ya ardhi ya Lebanon.
Pia, Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu, amesema Serikali ya Lebanon imeonywa kuwa “inacheza na moto” ikiwa haitachukua hatua dhidi ya Hezbollah.
Tangu kuanza kwa mzozo huo, Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam amerudia mara kadhaa kuwa serikali yake imejitoa kurejesha mamlaka kamili ya dola.
Baraza lake la mawaziri limechukua uamuzi ambao haujawahi kufanyika hapo awali wa kupiga marufuku tawi la kijeshi la Hezbollah. Hata hivyo, amesema ni vigumu kutekeleza hatua kama hizo wakati vita vinaendelea.
Aidha, kumekuwa na maswali mengi kuhusu msimamo wa Mkuu wa Jeshi la Lebanon, Rodolphe Haykal. Amekosolewa kwa kuonekana kuwa mpole au mwenye msimamo wa maridhiano dhidi ya Hezbollah.
Katika kauli zake, Haykal amesisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa, akimaanisha kuwa ikiwa jeshi litakabiliana moja kwa moja na Hezbollah, kuna hatari ya nchi kugawanyika kwa misingi ya kidini au makundi ya kijamii.
Kwa hiyo, uongozi wa kisiasa wa Lebanon unasema unataka kuchukua hatua dhidi ya Hezbollah, lakini jeshi linaonekana kuwa na tahadhari na kusita kufanya hivyo.
Ndege ya Marekani yaanguka
Mapema leo, Jeshi la Marekani limesema juhudi za uokoaji zinaendelea kwa ajili ya wafanyakazi waliobaki wa ndege ya kujaza mafuta angani ya Boeing KC-135 Stratotanker iliyodondoka magharibi mwa Iraq.
Mbali na kuthibitisha vifo vya wanajeshi wanne waliokuwa kwenye ndege hiyo, jeshi hilo limesema kupotea kwa ndege hiyo “hakukutokana na mashambulizi ya adui wala kushambuliwa kimakosa kutoka kwa vikosi vyao wenyewe”.
Majina ya wanajeshi hao hayajatangazwa kwa sasa hadi saa 24 zipite baada ya familia zao kuarifiwa rasmi.
Katika taarifa ya awali, Jeshi la Marekani lilisema kuwa ndege mbili zilihusika katika tukio hilo, huku ndege ya pili ikifanikiwa kutua salama.
Wakati hali hiyo ikiendelea Mashariki ya Kati, Rais wa Marekani, Donald Trump amewashambulia kwa maneno makali viongozi wa Iran akiwaita “watu waliopoteza akili na wahalifu” na kwamba ni heshima kubwa kwake kuwaua.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii Ijumaa usiku, Trump alisema Marekani “inaangamiza kabisa utawala wa kigaidi wa Iran”.
“Tuna nguvu ya kijeshi isiyo na kifani, risasi zisizo na kikomo, na muda wa kutosha – tazameni kitakachowapata hawa wahalifu waliopoteza akili leo,” alisema Trump.
“Wamekuwa wakiua watu wasio na hatia duniani kote kwa miaka 47, na sasa mimi, kama Rais wa 47 wa Marekani, ninawaua. Ni heshima kubwa kiasi gani kufanya hivyo!”
