Yanga yaikimbiza Simba Bara | Mwanaspoti

TUZO zinazotolewa kila baada ya mechi za Ligi Kuu Bara, ukiangalia katika vikosi vya Simba na Yanga, wageni ndio wamekuwa vinara wa kuchukua mara nyingi na idadi kubwa ya wachezaji mbele ya wazawa.

Tuzo hizo zimeelezwa na wadau pamoja na makocha kuibua ushindani wa timu pamoja na kupandisha thamani ya wachezaji.

Kama kawaida ya utani wa jadi, hakuna kitu wakawa nyuma, kila eneo wanashindana. Katika tuzo hizo Yanga imefunika kwa kuchukua 11 katika mechi 12 kabla ya jana kucheza na Tanzania Prisons, huku Simba ikinyakua nane katika mechi 12.

Kocha wa zamani wa makipa wa Namungo FC, Emmanuel Kingo, anasema: “Asilimia ya wachezaji wanaocheza mbele wana nafasi kubwa ya kunyakua tuzo hizo, kwa sababu wanahusika zaidi kufunga mabao yanayotoa pointi kwa timu, inatokea mara moja moja kwa nafasi kama ya kipa, mfano Diarra (Djigui) alichukua dhidi ya Simba kwa sababu aliisaidia Yanga isifungwe.”

Kuhusu wachezaji wa kigeni, kocha huyo anasema: “Asilimia kubwa inategemeana na mikataba yao, wengine inakuwa ni ya kuanza kikosi cha kwanza, hivyo wao ndiyo wanaocheza mara nyingi, hilo linawapa nafasi.”

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Mtibwa Sugar, Said Bahanunzi, anasema kuchukua wageni inaegemeana na viwango vyao na siyo kila mtu.

“Anayecheza kwa kiwango ndiye anayepewa nafasi ya kuzichukua, lakini kuhusu kupata wanaocheza nafasi ya mbele ni kutokana na hao wanafunga na kutoa asisti, mwisho wa siku lazima upatikane ushindi,” anasema.

Mchezaji mwingine aliyechangia hilo ni kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Mohamed Said ‘Nduda’ anasema: “Ukiona kipa ama beki kachukua tuzo ujue siku hiyo timu ilishambuliwa sana, wamejitahidi kuzuia, ama timu ililemewa na beki kafunga, ila ukweli wanaocheza nafasi za mbele wana nafasi kutokana na kufunga mabao. Kuhusu wageni wengi kuchukua wameonyesha kiwango wanastahili, hilo liwape chachu wazawa kupambana zaidi.”

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni anasema japokuwa tuzo hizo ni kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu, lakini klabu kongwe nchini haziwezi kuachana kushindana kwa kila sekta.

“Simba na Yanga haziwezi kuachana kushindana na kutaniana, na huo ndio utani wa jadi wenyewe, mmoja anapofanya vizuri lazima atamtambia asifanya vizuri, kila timu inatamba kwa wakati wake, ingawa ninachokisisitiza utani wa jadi siyo ugomvi wala uadui,” anasema Kibadeni.

Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally anasema: “Tuzo zinawapa motisha wachezaji kuongeza bidii kuona mchango wao unatambuliwa zaidi uwanjani, hicho ni kitu kizuri zaidi.”

Beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua anasema: “Kuna hisia ya furaha mchezaji anaipata anapopewa tuzo ya kutambuliwa kufanya vizuri katika mechi, inamuongezea morali ya kupambana kwa lengo la kuchukua zaidi na zaidi.”

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Shaban Kisiga anasema: “Tuzo ni heshima kwa mchezaji, ukiacha tu ile ya kila mechi zipo nyingi, hilo linampa nguvu mchezaji na kujiona anathaminiwa, kuhusu Simba na Yanga zina ushindani ambao hauwezi kuisha.”

WASIKIE MASTAA SIMBA, YANGA

Kwa upande wa Gueye, anasema: “Ushindani wa Ligi Kuu Tanzania ni mgumu, jambo la msingi ni kupambania ubingwa, lakini nafurahi kuchukua tuzo hizo.”

Vivyo hivyo kwa Rushine anasema anashukuru kwa sapoti wanayoipata kutoka kwa mashabiki wao, hao ndio wanawapa nguvu ya mapambano, huku akibainisha kwamba, kubwa zaidi anatamani kuona Simba inahukua ubingwa.

Kwa upande wa kipa wa Yanga, Diarra anasema: “Nina furaha, nashukuru mashabiki wanaotusapoti, tutapata moyo wa kupambana.”