Moshi. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likielekeza kila mwananchi kula angalau gramu 400 za mboga na matunda kwa siku, tafiti zinaonyesha kuwa wanawake wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha bado wanakula chini ya kiwango hicho kwa asilimia 75, hali inayoweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya.
Utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2022 hadi 2024 na Chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na World Vegetable Center (WorldVeg), International Food Policy Research Institute (IFPRI) na Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), kupitia mradi wa Better Diets and Nutrition, umebaini kuwa baadhi ya wanawake hupita mwezi mzima bila kula matunda.
Akizungumza leo katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya lishe bora mkoani humo, Mtaalamu wa lishe kutoka SUA, Joyce Kinabo amesema tatizo hilo ni kubwa na linaweza kusababisha changamoto nyingi za kiafya katika jamii.
“Tumegundua ulaji wa mboga na matunda upo chini sana, na hili ni tatizo kubwa hasa kwa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Mapendekezo ni kwamba kila mtu anatakiwa kula angalau gramu 250 za mboga kwa siku au gramu 400 za mboga na matunda kwa siku,” amesema Profesa Kinabo.
Mtaalamu wa lishe kutoka chuo kikuu cha kilimo Sokoine (SUA), Joyce Kinabo akizungumza katika warsha iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa lishe kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, Manispaa ya Moshi Mkoani humo.picha na Janeth Joseph
Amesema, “tumeona kabisa kwamba si watu wengi wanaofikia kiwango hicho. Kuna kina mama wanaweza kwenda mwezi mzima bila kula tunda. Kwa kweli hizi ni takwimu zilizotushtua sana. Mwanzoni niliposikia sikutarajia kwamba kuna mtu anaweza kukaa mwezi mzima bila kula tunda kabisa,” amesema
Profesa Kinabo amesema, baadhi ya matatizo mengi ya kiafya yanayotokea katika jamii yanatokana na upungufu wa virutubisho vya vitamini na madini ya chuma kutokana na desturi ya watu kutokula mboga na matunda.
“Kwa wanawake ambao hawafikii kile kiwango ambacho wanatakiwa kula virutubishi ni zaidi asilimia 75 hadi 80 kwa siku, lakini kuna kiwango kimoja ambacho kinapitiliza asilimia 100.Ulaji wa vyakula vya wanga ni mkubwa sana na ndio maana matatizo ya uzito mkubwa upo Kilimanjaro na Arusha lakini hasa Kilimanjaro.”
Ameongeza, “Ile dhana ya mboga na matunda ni kwa wanawake na watoto zinawaponza wanaume kwa sababu unakuta upungufu wa damu ni mkubwa sana kwao kuliko wanawake ambapo takwimu zinatuonyesha hivyo,”amesema Profesa Kinabo.
Profesa Kinabo amefafanua kuwa, “Hii nayo ni changamoto tunayoiona, na hii inatokana na uelewa hafifu wa jamii kuhusu umuhimu wa mbogamboga na matunda, tumezingatia sana kwenye ulaji wa vyakula vingine hasa vya asili ya wanga kuliko mbogamboga.”
“Mpaka sasa tumefikia sehemu ambayo takwimu zetu zimeshakamilika na tumezifanyia ukokotoaji na tupo tayari sasa kurudi kwenye jamii kuwaeleza matokeo ya utafiti huu, ili tupate mawazo yao kujua nini kifanyike na ushauri wao ili tuweze kuangalia ni jinsi gani tutarudisha afua mbalimbali katika jamii,”amesema Profesa Kinabo
Kwa upande wake, Mratibu wa Taasisi ya Kimataifa ya World Vegetable Centre, Winston Mombeki amesema baada ya kubaini changamoto ya wananchi kutokula mboga na matunda, wameanza kutoa elimu katika halmashauri mbalimbali za mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ili kuwajengea uwezo wananchi kuelewa umuhimu wa lishe bora.
Aidha, amesema ulaji wa matunda na mbogamboga una umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu kwani husaidia kuikinga miili dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Amesema pamoja na tafiti zinazoendelea, takwimu za awali zinaonyesha bado kuna baadhi ya mila na desturi zinazochangia watu kutokula mboga na matunda.