LICHA ya ushindani mkali uliopo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama, anaamini kikosi chao kina uwezo na ubora wa kutwaa ubingwa msimu huu.
Chama amesema kikubwa kwa sasa ni wachezaji kuendelea kupambana katika kila mchezo na kuhakikisha wanatumia vizuri nafasi wanazozipata ili kuendelea kukusanya pointi muhimu.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kiungo huyo kuwa sehemu ya ushindi muhimu wa Simba ilipowafunga Singida Black Stars kwa mabao 2-1 katika mchezo wa ligi uliochezwa Machi 11, Singida.
Katika mchezo huo, Chama alitoa pasi ya mwisho iliyozaa bao la ushindi lililofungwa na kiungo mshambuliaji Elie Mpanzu na kuisaidia Simba kuondoka na pointi tatu muhimu.
Nyota huyo wa kimataifa wa Zambia amesema ushindi huo umeongeza morali kwa wachezaji wa Simba katika kuendelea kupambana katika mechi ijayo dhidi ya TRA United FC ambayo itachezwa leo, Arusha.
“Ushindani uliopo msimu huu ni mkubwa kwa sababu kila timu inapambana kutafuta matokeo mazuri, jambo linalofanya kila mchezo kuwa mgumu,” alisema na kuongeza:
“Simba ina kikosi chenye wachezaji wenye ubora wa kutosha kupambana katika mazingira hayo ya ushindani.”
Aliongeza kuwa siri kubwa ya mafanikio siku zote ni wachezaji kufanya kazi kwa bidii, kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kucheza kwa ushirikiano mkubwa uwanjani.
Kiungo huyo pia alisisitiza umuhimu wa wachezaji kubaki na umoja ndani ya timu, akisema hilo limekuwa moja ya nguvu kubwa ya Simba katika kipindi chao cha mafanikio misimu kadhaa iliyopita.
Tangu arejee tena ndani ya kikosi cha Simba, Chama ameendelea kuonyesha kiwango kizuri na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika safu ya kiungo ya timu hiyo.
Katika vipindi vyake viwili vya awali akiwa Simba, kiungo huyo alicheza jumla ya mechi 183 katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Ndani ya michezo hiyo, Chama alifunga mabao 42 huku akitoa asisti 60, takwimu zinazoonyesha mchango wake mkubwa ndani ya kikosi hicho.
Asisti aliyotoa katika mchezo dhidi ya Singida Black Stars imeongeza idadi ya pasi zake za mabao hadi kufikia 61 tangu aanze kuitumikia Simba.
Chama alisema ataendelea kujituma ili kuhakikisha anaisaidia timu yake kupata matokeo mazuri na kurejesha heshima ya Mnyama ambayo imepotea kwa misimu minne iliyopita.
Kwa sasa Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 27, sawa na Azam FC. Wapo nyuma kwa pointi nane dhidi ya Young Africans SC ambayo inaongoza msimamo wa ligi na pointi 35 ikiwa imecheza mechi moja zaidi.
