Dk Mwigulu awaka, aagiza mnyororo usambazaji dawa uchunguzwe

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kufanyika uchunguzi wa haraka katika vituo vya afya vya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi, kufuatia kubainika wananchi wengi wanaelekezwa kununua dawa katika maduka ya nje, licha ya taarifa za Serikali kuonyesha dawa za kutosha zinapatikana hospitalini.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara eneo la Kibaoni ambako anaendelea na ziara mkoani Katavi, Dk Mwigulu amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa, hivyo haiwezekani wagonjwa waambiwe wakatafute dawa kwenye maduka binafsi kila wanapokwenda hospitali kutibiwa.

Dk Mwigulu amesema katika maeneo mengi aliyopita nchini, taarifa zinazoletwa na wataalamu zinaonyesha kuwa utoshelevu wa dawa unazidi asilimia 90, jambo ambalo linapaswa kuwahakikishia wananchi kupata dawa wanazohitaji wanapofika hospitalini.

“Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na karibu kila mahali nikipita naambiwa utoshelevu ni zaidi ya asilimia 90. Lakini, inapotokea kila mwananchi akienda kutibiwa hospitalini anaambiwa akanunue dawa kwenye maduka ya nje, hapo kuna tatizo,” amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo amesema hata katika ziara yake Mpimbwe ameambiwa wagonjwa wengi, wakiwemo wazee, wanapoenda hospitali hupewa maelekezo ya kwenda kununua dawa kwenye maduka ya nje badala ya kuzipata katika vituo vya afya vya Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Dk Mwigulu alimemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) kutoa maelezo ya kina kuhusu namna ununuzi na usambazaji wa dawa unavyofanyika katika hospitali za wilaya hiyo.

Akijibu hoja hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita utoshelevu wa dawa haujawahi kushuka chini ya asilimia 90, lakini changamoto kubwa imekuwa ikitokana na baadhi ya watumishi kuandika majina ya kampuni zinazotengeneza dawa badala ya majina halisi ya dawa zilizopo kwenye stoo za hospitali.

Ameeleza kuwa katika baadhi ya matukio, watumishi wa afya huandika majina ya dawa kwa kutumia majina ya kampuni fulani, jambo linalosababisha dawa hizo zionekane kana kwamba hazipo hospitalini, ilhali zipo kwa majina ya kawaida.

Kwa mfano, amesema dawa ya paracetamol (panado) wakati mwingine huandikwa kwa jina la kampuni inayozalisha dawa hiyo, jina ambalo halipo kwenye orodha ya dawa zilizopo hospitalini, hali inayosababisha wagonjwa kuambiwa wakanunue dawa hizo nje.

“Changamoto hiyo tunakiri ipo. Baada ya malalamiko kutoka kwa wananchi, tayari tumeshachukua hatua kwa baadhi ya watumishi. Hadi sasa watumishi watatu wamechukuliwa hatua kwa kosa hilo,” amesema.

Hata hivyo, maelezo hayo hayakumridhisha Waziri Mkuu ambaye alieleza hali hiyo inaweza kuwa na viashiria vya mchezo mchafu unaowalazimisha wananchi kununua dawa nje, wakati Serikali imekwisha zipeleka hospitalini.

Kutokana na hali hiyo, amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Katavi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa jambo hilo.

Ameeleza uchunguzi huo uhusishe mtiririko mzima wa fedha na dawa kuanzia hatua ya ununuzi, mapokezi, uhifadhi hadi usambazaji kwa wagonjwa ili kubaini kama kuna upotevu au matumizi mabaya ya dawa hizo.

“Haiwezekani wananchi wanalazimishwa wakanunue dawa kwenye maduka ya nje wakati Serikali inaleta dawa hapa na zinaonekana zipo. Inawezekana kule wanakoambiwa wakanunue ni maduka yao au wanatanguliza biashara zao huko,” amesema.

Amesema michezo ya aina hiyo husababisha Serikali kulaumiwa na wananchi wakati imetekeleza wajibu wake wa kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali za umma.

“Michezo hii inasababisha Serikali itukanwe wakati imefanya wajibu wake. Nataka nipate taarifa kamili ya wote waliohusika na hatua zilizochukuliwa. Kamanda wa Takukuru fuatilia mtiririko wote; fedha zinavyotumika kununua dawa, dawa zinavyonunuliwa, zinavyopokelewa na zinazotolewa zimekwenda wapi,” amesema.

Amesema haiwezekani taarifa za Serikali zionyeshe upatikanaji wa dawa kwa asilimia 90 hadi 95, lakini wagonjwa wote wanaofika hospitalini waambiwe wakatafute dawa kwenye maduka ya dawa ya mitaani.

“Hatuwezi kuwa na taarifa kwamba upatikanaji wa dawa ni asilimia 90 hadi 95 halafu kila mtu anaelekezwa akatafute dawa mtaani. Duka la mtaani linatoa wapi dawa ambayo Serikali inakosa?” amehoji.

Kulimbikiza leseni za madini

Katika hatua nyingine malalamiko ya wananchi kuhusu migogoro kati ya umiliki wa mashamba na leseni za uchimbaji madini yameibuka upya mbele ya waziri mkuu aliposimama kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Sitalike.

Wananchi wamedai baadhi ya wachimbaji wanapewa leseni nyingi katika maeneo ambayo tayari yanatumiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo.

Kwa mujibu wa wananchi hao, ingawa Serikali imekuwa ikitoa leseni za uchimbaji kwa wazawa ili kuwainua kiuchumi, baadhi ya watu wamekuwa wakipata leseni nyingi kwa wakati mmoja katika maeneo tofauti, jambo linalosababisha migongano ya matumizi ya ardhi.

Mmoja wa wananchi amesema kuwa wakati mwingine wachimbaji hupewa leseni katika maeneo ambayo tayari yanamilikiwa na wakulima, hali inayowalazimu wakulima kuondolewa katika mashamba yao.

“Ni kweli watu wa madini wanasema wanatoa leseni kwa wachimbaji wadogo wazawa, lakini utakuta mtu mmoja anapata leseni zaidi ya 10 katika maeneo tofauti. Wakati mwingine wanaingia hadi kwenye mashamba ya watu.

“Unalima shamba lako halafu unaambiwa hapa kuna leseni ya mtu. Unashangaa mimi ndiyo mwenye shamba lakini naambiwa kuna leseni ya mtu. Kisheria mwenye leseni ana nguvu kuliko mwenye shamba,” amesema.

Amesema hali hiyo imekuwa ikijitokeza katika vijiji mbalimbali vikiwemo Mtisi na Magula, huambako wananchi wamekuwa wakilalamika mara kwa mara bila kupata suluhisho la kudumu.

“Watu wakilalamika kwa viongozi, wanaosikilizwa zaidi ni wale wenye leseni. Baadhi ya watendaji wa Serikali hawafanyi kazi yao kwa weledi na ndiyo maana tumefika hapa,” amesema.

Mwananchi huyo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka ya karibuni viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wamefika kusikiliza malalamiko yao, lakini bado hawajapata majibu ya kudumu.

“Leo wewe ni kiongozi wa tatu wa juu kuja kusikiliza changamoto hii katika kijiji kimoja, lakini bado hatupati majibu. Shida iko wapi?” alihoji mwananchi huyo.

Akijibu malalamiko hayo, Dk Mwigulu ameelekeza suala hilo kushughulikiwa haraka na viongozi wa sekta ya madini ili kuondoa migogoro inayowakabili wananchi.

Amesema ni muhimu viongozi wa wizara husika kufika eneo hilo na kukutana na wananchi ili kujadili kwa kina kuhusu changamoto hiyo na kuipatia ufumbuzi wa kudumu.

Kutokana na hali hiyo, amemwagiza Anthony Mavunde, Waziri wa Madini, kufika katika eneo hilo kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge ili kukutana na wananchi na viongozi wa eneo hilo.

“Waziri wa Madini aje hapa kabla ya Bunge kuanza. Mwenyekiti wa kijiji, diwani na mbunge pangeni mkutano na muwasiliane naye (waziri) aje hapa mjadiliane kuhusu hilo suala,” amesema.

Waziri Mkuu amesisitiza mkutano huo unapaswa kuwaleta pamoja wataalamu wote wanaohusika na utoaji wa maeneo ya uchimbaji ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Bunge linaanza Machi 31, nataka kabla ya hapo yeye na wataalamu wake kuanzia wa juu hadi wa chini wawe wamefika hapa. Wote wanaohusika na kutoa maeneo ya uchimbaji waje hapa ili hilo suala limalizike. Haiwezekani mtu mmoja anakuwa na leseni za uchimbaji 100, hii inakuwaje ina maana hii nchi ni yake peke yake?” amesema.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata haki katika matumizi ya ardhi na rasilimali za madini bila kusababisha migogoro katika jamii.