Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, ametaja faida nane zitakazopatikana kupitia kituo kipya cha pamoja cha kuwezesha manunuzi na mauzo ya nje, akisema kitawarahisishia wajasiriamali kupata mitaji na teknolojia za kisasa za uzalishaji.
Amesema matokeo chanya ya kituo hicho yanatarajiwa kuanza kuonekana mwaka 2030, ambapo programu hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji na biashara.
Kituo hicho kinatarajiwa kutoa mafunzo kwa vijana 50 kila baada ya miezi miwili na kitawawezesha kuzalisha bidhaa mbalimbali, kupakia na kuuza nje ya nchi, lengo kukuza uchumi wa viwanda nchini.
Profesa Mkumbo ameyasema hayo leo Machi 14, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha pamoja cha kuwezesha manunuzi ya vifaa vya uzalishaji na mauzo ya nje pamoja na programu ya mafunzo kwa wawekezaji vijana, iliyofanyika katika eneo la Uwekezaji la Benjamin William Mkapa, Mabibo jijini Dar es Salaam.
Amesema huduma zitakazotolewa katika kituo hicho ni pamoja na utoaji wa elimu ya ujasiriamali na uwekezaji, ikiwemo namna ya kukidhi vigezo vya masoko ya kimataifa na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Pia, kituo hicho kitaunganisha wazalishaji wa ndani na wasambazaji wa kimataifa wa mitambo ili kurahisisha upatikanaji wa teknolojia za uzalishaji.
Profesa Mkumbo ameongeza kuwa kituo hicho pia kitaonesha na kushirikisha taarifa za fursa za masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania katika masoko ya nje, pamoja na kutoa huduma za uhakiki wa wasambazaji wa kimataifa.
“Pia, kutakuwa na uratibu wa huduma za usafirishaji wa mizigo, kurahisisha taratibu za kuuza bidhaa nje ya nchi, pamoja na kutoa huduma za ushauri na uangalizi baada ya uwekezaji.
Hii ni pamoja na kuwaunganisha wajasiriamali wanaochipukia na wale waliobobea na kufanikiwa katika biashara na uwekezaji,” amesema.
Amesema ifikapo mwaka 2030, vijana kati ya 50,000 hadi 100,000 wanatarajiwa kuwa wamewezeshwa kuanzisha na kuendesha biashara ndani ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZ) nchini kote.
Aidha, takribani biashara 5,000 za vijana zinatarajiwa kuanzishwa kupitia shughuli za uzalishaji, usindikaji na huduma zinazohusiana na viwanda.
Kwa upande wa ajira, amesema zaidi ya nafasi za ajira kati ya milioni 1 hadi milioni 3 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinatarajiwa kuzalishwa kupitia biashara hizo.
Profesa Mkumbo amesema Serikali inalenga kuona sekta binafsi ya Tanzania inaingia katika ushindani wa kikanda, akitaja soko la pamoja la Africa Free Trade Area (AfCFTA), akisema wafanyabiashara hawawezi kunufaika na soko hilo bila kujipanga na kuwa tayari kushindana.
Akizungumzia kituo hicho, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Fred Msemwa amesema uzinduzi wa kituo hicho ni kielelezo cha kuanza kwa utekelezaji wa mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dk Msemwa amesisitiza kuwa sekta ya uzalishaji ndiyo moyo wa mageuzi ya kiuchumi nchini kuelekea mwaka 2050, na kwamba uzinduzi wa kituo hicho ni hatua muhimu ya kuijenga sekta hiyo ili iweze kushindana katika soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri, amesema jukumu lao si kuvutia uwekezaji pekee, bali pia kuhakikisha uzalishaji unaongeza thamani ya bidhaa na kuzifikisha katika masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema katika mwaka wa fedha uliopita, Tiseza ilisajili miradi 940 yenye thamani ya dola za Marekani 11 bilioni, iliyotarajiwa kuzalisha ajira 342,000.
“Takwimu hizi zinaonyesha kuwa viwanda vinaendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi, huku maeneo yetu maalumu ya kiuchumi yakizidi kuwa kitovu cha shughuli za uzalishaji,” amesema.
Teri amesema wamebaini vijana wengi wana hamu ya kufanya biashara na uwekezaji, lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu ya uzalishaji, kushindwa kufikia viwango vya kimataifa na kukosa uhusiano na masoko.
“Vijana wanaweza kuwa na mitaji lakini hawajui jinsi ya kuanza, kwa programu hii tunatarajia kuwapa mafunzo na kuwawezesha kutumia miundombinu tuliyonayo ili waweze kuingia kwenye uzalishaji. Kupitia kituo hiki tutaanza na bidhaa za kilimo zinazochakatwa na kuongezwa thamani, na baadaye tutapanua wigo kulingana na mahitaji ya soko,” amesema.
Akizungumzia manufaa ya kituo hicho, Amani Daniel, mjasiriamali eneo la Ubungo amesema kituo hichoni fursa kubwa kwao.
“Mara nyingi tuna wazo la kuanzisha biashara lakini tunakosa mtaji, masoko na teknolojia ya kisasa. Sasa naona tutapata msaada wa kuunganisha mitaji, mafunzo na vifaa vya kisasa vya uzalishaji,” amesema.
