KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kesho Jumapili anakutana na waajiri wake wa zamani Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara huku akiwa na zigo zito linalomkabili.
Nyota huyo ambaye huu ni msimu wa tatu anaitumikia Azam tangu alipojiunga nayo 2023-2024 akitokea Yanga.
Kwa msimu huu, tayari Fei Toto amevunja rekodi yake ya mabao katika Ligi Kuu Bara aliyoiweka msimu uliopita, ingawa kwa sasa nyota huyo ana deni moja tu la kuzifikia asisti alizopiga msimu wa 2024-2025.
Bao moja aliloifungia Azam katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Machi 11, 2026, limemfanya nyota huyo kufikisha mabao sita ya Ligi Kuu msimu huu, huku akiivuka rekodi ya msimu uliopita aliofunga mabao manne.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma, Fei Toto alifunga bao hilo dakika ya 11, huku akichangia pia lingine moja la Zidane Sereri, aliyefunga mawili dakika ya 5 na 70, akiwaadhibu waajiri wake wa zamani.
Baada ya Fei Toto kuchangia mabao mawili kati ya matatu dhidi ya Dodoma Jiji, nyota huyo kwa sasa amefikisha mabao sita, akiivuka rekodi ya msimu uliopita katika ligi, huku akifikisha asisti tano, ambapo kwa sasa anadaiwa nane.
Msimu wa 2024-2025, Fei Toto alichangia mabao 17 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga manne na kuasisti 13, akiwa ndiye aliyeongoza kwa assisti nyingi, ingawa kwa msimu huu, tayari amechangia 11, kufuatia kufunga sita na kuasisti matano.
Fei Toto ndiye mchezaji aliyefanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024 na alichangia mabao 27 ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga 15 na kuasisti 12, akimzidi Stephane Aziz KI aliyekuwa Yanga akifunga 12 na kuasisti tisa.
Mwaka 2024, Feisal aliongoza kwa nyota waliochangia mabao mengi, akifuatiwa na Stephane Aziz KI ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ittihad SC ya Libya, ambapo hadi anaondoka alichangia 21, baada ya kufunga 12 na kuasisti tisa.
Kiwango bora cha Feisal kilimfanya kumaliza na mabao 19 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024, akiwa ndiye mchezaji mzawa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa kufunga mabao mengi zaidi, nyuma ya Aziz KI aliyekuwa Yanga aliyefunga mabao 21.
Pia, alikuwa mchezaji bora wa Kombe la Shirikisho (FA) msimu wa 2023-2024, kwa kuifikisha Azam fainali na kuchapwa na Yanga kwa penalti 6-5, baada ya suluhu (0-0) ya dakika 120, Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024.
Fei Toto ameonekana kuwa ni mchezaji anbaye ukimpa maagizo anakufanyia kazi yako ipasavyo na unaweza kusema ndiye mchezaji mzawa mwenye namba nzuri katika Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu mfululizo sasa.
Kiungo huo wa ushambuliaji, amekuwa akipewa majukumu tofauti tangu atue Azam ambapo msimu wa kwanza 2023-2024, alitumika zaidi juu kutokana na kuwepo changamoto ya washambuliaji halisi.
Kwa wakati huo, Fei Toto alifunga mabao 19, mawili nyuma ya kinara Aziz KI (21), lakini pia hakuwa nyuma katika kutengeneza mabao akimaliza na asisti saba.
Msimu wa 2024-2025, akarudishwa katika eneo lake la kuchezesha timu, akamaliza kinara wa asisti akiwa nazo 13, huku pia akifunga mabao manne.
Msimu huu pia yupo eneo la kuchezesha timu kutokana na Azam kuwa na washambuliaji wapambanaji na wanaoendelea kufanya vizuri akiwamo Zidane Sereri, Jephte Kitambala na Jean Jaques Ngita.
Hata hivyo, Fei Toto ameendelea kuwa mwiba kwa wapinzani akihusika na mabao 11 akifunga sita na asisti tano.
Katika kipindi cha misimu mitatu sasa Fei Toto akiwa Azam, hadi wakati huu amefanikiwa kuhusika kwenye mabao 54 yaliyotokana na kufunga 29 na asisti 25. Uwiano wa kufunga na akuasisti havipishani sana hali inayomfanya kuwa mchezaji hatari zaidi kwa wapinzani na muhimu ndani ya timu anayoitumikia.
Wakati hali ikiwa hivyo, Fei Toto hakuwa na namba nzuri za kufunga wakati akiwa Yanga kutokana na majukumu aliyokuwa akipewa akicheza zaidi eneo la kiungo na sio ushambuliaji.
Katika misimu mitano aliyokuwa Yanga kuanzia 2018 hadi 2022, ameondoka na jumla ya mabao 23 ambapo misimu mitatu ya mwisho kila mmoja alifunga sita ambayo ni 2020-2021, 2021-2022 na 2022-2023. Kabla ya hapo, 2018-2019 ambao ulikuwa msimu wa kwanza alifunga mabao manne, kisha 2019-2020 bao moja.