Hekaya za Mlevi: Mbu tumemshindwa, kunguru je?

Dar es Salaam. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Huwa hana majivuno pale anapofaulu. Akifanikiwa hutumia mafanikio yake kwa faida ya jamii. Lakini anapofeli huyaanika madhaifu yake kwa jamii pia. 

Huamini kuwa jamii inaweza kujifunza kwa kuanzia pale alipokaribia kukwama na kurekebisha. Ni kawaida ya watu wasio waungwana kuyaficha maanguko yao ili wachekelee wenzao wakiyapitia.

Kiungwana kama jamii, inatubidi tufundishane kutokana na makosa yetu na ya wenzetu. Wenzetu waligundua umeme kwa hatua, wengine wakipoteza maisha na wengine kupatwa na ulemavu. 

Kuna walioota kuitumia radi kama malighafi ya kufua umeme, wengine upepo na wengine maji. Lakini kwa sababu wote waliota mafanikio, kila mmoja aliweka hadharani taarifa zake hadi walipofanikiwa kuwasha taa.

Watafiti wa Kitanzania wanapaswa kuweka maandishi yao bayana yasomeke na vizazi vyao. Tafiti za mambo mengi zinaishia hewani bila kuonesha matokeo. 

Jamii yetu inapaswa kuelezwa iwapo mambo hayo yameshindikana au utafiti umekwamia wapi. Kama jambo limebuma, ni bora kushirikisha watafiti wa elimu ya mtaani kuliko kukaa kimya. Moja ya mambo haya muhimu ni tiba na kinga ugonjwa wa Malaria. 

Kwa miaka mingi ugonjwa huu umekuwa sugu kama nunda. Mimi ni shuhuda wa harakati za kuufuta ugonjwa huu tangu nilipokuwa mdogo. Nakumbuka tangu enzi za magari ya wafadhili kupuliza dawa mtaa kwa mtaa.

Enzi za kuchemsha muarobaini, enzi za vidonge vya klorokwini, aspirini na kwinini, enzi za sindano za kristapeni na PPF, enzi za dawa za fansida hadi sasa dawa tatu. Hapo sijataja vyandarua vya matundu madogo.

Jitihada zote zimeonesha matokeo hasi, na Malaria inatajwa kuangamiza watu wengi kuliko vita. Nadhani inabidi Serikali na Wizara wakiri kuwa Malaria ni shida, hivyo kuwekeza nguvu kwa wazee wa tiba mbadala.

Mbona kwenye baadhi ya mambo Serikali iliachia nafasi kwa watu binafsi kushughulika nayo? Mengine yanaweza kukuchekesha, kama tulivyozidiwa na kunguru weusi (full suit au ‘kulabu’).

Inasemekana katika kung’arisha Jiji la Dar es Salaam lililoelemewa na uchafu, kuna watu au taasisi fulani iliamua kutoa zawadi ya kunguru wawili watatu hapa Jijini. Lengo lilikuwa kusafisha jiji kwa kuwa tabia ya kunguru hawa ni kula uchafu.

Lakini hivi sasa nafikiria tena juu ya Taasisi zilizotuzawadia kunguru. Ni kweli walitupatia zawadi au nao walikuwa na utafiti wao tofauti?

Walipoingia mjini, kunguru hawa walishindwa kutafsiri jukumu walilopewa. Walianza kuwaona kunguru wa zamani kuwa uchafu. Zamani tulikuwa na kunguru wanaofanana na wachungaji au wainjilisti kimavazi (wana alama nyeupe juu ya kifua).

 Wakawala wote. Walipobaki peke yao ndio wakajua uchafu ni nini. Sasa badala ya kuula wao wakawa wakiutawanya na kuchafua zaidi. Mwisho wakahukumiwa vifo. Lakini unawauaje?

Sifa kubwa ya kunguru weusi ni akili miksa na kiburi. Wamejigawanya kwenye makundi kadhaa, hapa nitakuchambulia kundi la majumbani na lile la machinjioni. Kundi la majumbani linamwelewa vizuri adui yao, binadamu. 

Hawa hupenda sana maudhi, Wakimwona mtu anafagia uwanja, wao huokota taka jalalani na kuzitupia palipofagiliwa. Au ukianika nguo kambani, kwa makusudi huja kucheza kwenye nguo nyeupe ili kuzichafua.

Kunguru wa majumbani hawamwogopi mtoto. Akiona mtoto kaachwa pekee kwenye jamvi, kwanza naye atashuka hapo jamvini kumkagua kama ana chochote kinachofaa kuliwa. 
Akimkuta na kitumbua mkononi anamnyang’anya. Lakini kama hana chochote, atamdonoa ili kuona kama anaweza kulika. Kunguru hawa ni hatari sana kwa watoto, maana ukimsahau mtoto mchanga jamvini unaweza kumkuta hana macho.

Wakimwona mama anapika, wao wanamvizia pale atakapoinuka kufuata chumvi kabatini. Kwa spidi ya umeme wanaweza kulishukia sufuria lililo motoni, kulifunua na kuopoa kidari cha kuku! Wanajua kuchagua kidari na kuacha shingo. 

Muuza samaki mmoja alinichekesha aliponiambia kunguru alimchukulia samaki na chachandu yake! Na ukimwekea sumu anatazama kama msosi unashobokewa na nzi. Kama sivyo anajua kuwa ipo namna, hatakula.

Halafu kunguru anatunza kumbukumbu. Hasahau mahala anapoficha msosi wake, na mtu atakayeutoa mzoga huo atakuwa adui yake milele! Mahasimu wao wakuu ni wagema minazi, maana kunguru hulala minazini ambamo ndimo shambani mwa mgema. Kila mmoja wao (kunguru na mgema) humshutumu mwenzake kwa kuingilia maslahi yake. Kila mgema anapopita barabarani huambatana na kundi la kunguru wanaomzomea

Ajabu ingine ya kunguru ni hii: Hata kama kiota chake kipo Mbagala, kama yeye ni mlaji wa Vingunguti basi kila asubuhi ataelekea huko na kurudi Mbagala jioni. Na yule anayelala Vingunguti hudamkia Mbagala. Wanapishana kila asubuhi na jioni kama usafiri wa anga. 

Fikiria kunguru anayetoka Kigamboni, kwenda kula Pugu na kurudi Kigamboni kulala. Halafu wala hahitaji treni zenu za SGR…  

Hivi sasa kunguru wamekuwa wasumbufu zaidi ya mbu. Kama tunashindwana na mbu, tududu tudogo kama nukta, je tutayaweza ya kunguru? Kama wameshafikia kugombania mboga na wake zetu jikoni, tumuombe Mungu sana asiwajalie ukubwa kama wa bata mzinga. 
Watatumezea mate na tutakosa pa kujificha. Manake kwanza washakuwa wengi kuliko nzi. Pili uchu wao unatosha kabisa kubomoa vibanda vyetu na kutufanya misosi.