KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NAMNA WANANCHI WANAVYOUTUMIA UMEME KUJILETEA MAENDELEO

📌 Umeme umewashwa kwa mara ya kwanza katika vitongoji viwili

📌 Zaidi ya Shilingi bilioni 60 zatumika kusambaza umeme kwenye vitongoji vya mkoa wa Shinyanga

Kahama, Shinyanga📍

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na namna fedha za Bajeti ya Mwaka 2025/2026 zilizoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinavyotumika katika utekelezaji wa Miradi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati pamoja na zoezi la kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kitongoji cha Mine, kata ya Mwakata, Jimbo la Msalala na kitongoji cha Mjimwema katika Jimbo la Kahama wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, amesema ziara ya kamati imelenga kukagua na kujionea utekelezaji wa Miradi ili kuhakikisha fedha zilizotengwa na Bunge zinatumika kwa ufanisi.

“Tumepewa dhamana na Bunge kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatekeleza kusudi lililokusudiwa. Bunge lilitenga bajeti ya shilingi bilioni 400 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya miradi ya kufikisha umeme vitongojini, na tumekuja kuona thamani ya fedha hizo kama imetumika ipasavyo. Kwa kweli tumeridhishwa na kazi inayofanywa na REA,” amesema Mhe. Mgalu.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaonesha mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya umeme.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema ukaguzi wa miradi unaofanywa na Kamati ya Bunge ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Katiba, inayolenga kuhakikisha Bunge linasimamia ipasavyo matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo.

Makamba amesema katika bajeti ya Wizara ya Nishati, ilipanga kuwa kila jimbo nchini litapatiwa vitongoji 15 vitakavyofikishiwa huduma ya umeme ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa Wananchi.

Amesema Miradi hiyo inaendelea kubadilisha maisha ya Wananchi kwa kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na kuboresha huduma za kijamii na kuongeza fursa za maendeleo katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, amesema mkoa wa Shinyanga una jumla ya vitongoji 2,704 ambapo kati ya hivyo vitongoji 1,180 tayari vimefikishiwa huduma ya umeme.

Amesema vitongoji 582 vipo katika Mradi wa HEP II (B); Mradi uliosainiwa Januari mwaka huu ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

“Kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 hadi sasa REA imeidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 61 kwa ajili ya kufikisha umeme katika vitongoji mbalimbali vya mkoa wa Shinyanga,” amesema Mhandisi, Olotu.

Aidha ameahidi kuwa REA itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na Bunge kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme.